Skip to content

Mabavu ya CCM yanapoteswa na diplomasia ya Maalim Seif

Uongozi ni hikma, maarifa na busara. Ni kuangalia mambo kwa mtazamo mpana wenye kubeba maslahi ya jamii unayoitumikia. Uongozi si maagizo na maamrisho yasiyo na tija. Si kujikweza na kujionyesha kwa watu kwamba nawe upo. Si kupalilia fitna na farka za kuifarakanisha nchi na jamii yenye kufuka moshi kama hii ya Kizanzibari. Si kutovuka adabu au kuonyesha ufundi wa kutokuwa kwako na heshima kwa wakubwa wa umri kwako na wakongwe wenye kuheshimika kimataifa. Ukifika hapo, juwa huna hunani na uongozi wako ni wenye kutia shaka.

 

Maalim Seif Sharif Hamad
Maalim Seif Sharif Hamad

 

Nimeketi kwenye baraza ya kijumba changu cha chumba kimoja. Ghafla anatokea mzee wangu ambaye kutokana na kukuwa kwake na baba yangu mzazi, kimalezi na maadili ya kwetu, huyu mimi namuita ami au baba mdogo au mkubwa.

Ami ananiambia anahitaji neno langu kuhusu maendeleo ya siasa za kwetu, licha ya kwamba mimi ni mdogo mara zote na kwa yote kwake. Kisha nikagundua kuwa hakuwa akitaka neno kutoka kwangu, bali alikuwa anataka kunipa neno lake. “Ami, nakuhakikishia hawa hawana manusura!”. Kisha ananionesha namna alivyojengeka imani isiyotetereka kiasi cha kuamini kwamba muda si mwingi ujao, wale anaowaita waporaji wa uchaguzi wa Oktoba 25 ya mwaka jana “watairejesha haki waliyoipora kwa mwenye kuistahiki.” Masikini, ami yangu! Kumbe alikuwa hataki dripu kutoka kwangu, bali alikuwa ananiona labda mimi imani yangu imeshuka kidogo na hivyo, akaja kunipiga tashdidi kidogo. Na lazima niseme kuwa hili lilikuwa faraja kwangu na naamini ni mkuki mkali kwa waporaji wa haki hiyo.

Kuna kitu ambacho leo napenda nikijadili kwa faida ya wengi. Hiki ni namna Wazanzibari wadhaifu wanavyotumia silaha dhaifu na kukiumiza kichwa cha mtawawala mwenye vifaru na mizinga! Siku nyengine ya hivi karibuni, nikiwa kwenye baraza ya kahawa ya Magomeni Kwa Najim, kando kidogo ya Mjini Unguja, baada ya swala ya magharibi, ghafla mmoja wetu akapaza sauti kwa hadhira iliyokusanyika kwenye baraza hio. Akatowa salamu kisha akaifahamisha hadhira kwamba mahali pale pamefikiwa na ugeni maalumu wenye neno maalumu kwa watu maalumu. Mgeni wetu akaanza kuelezea hadhira hile kuhusu neno la kiongozi wao mpendwa ambalo alilitowa kwenye Msikiti wa Biziredi mara baada ya Swala ya Ijumaa. Bwana huyu akasherehesha kauli ya mpendwa wake kiasi cha kuziteka na kuzikonga nyoyo za hadhira ile ambayo ni wazi kwamba ilikuwa imejaa ghera na matumaini yasiyokatika! Mpendwa wao huyo alikuwa ni Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), na ambaye CUF wenyewe wanaamini kuwa ndiye mshindi halali wa uchaguzi wa Oktoba 25.

Nilibaki kimya kumsikiliza bwana yule ambaye lazima nikiri kwamba anao uwezo na kipaji cha aina yake katika kuelezea na kujibu masuali kwa ustadi na ufundi mkubwa. Mmoja miongoni mwa wasikilizaji alitaka kujuwa ni lini Maalim Seif atakabidhiwa serikali aliyoporwa? Bwana yule akajibu kwa ustadi na kujiamini kwamba muda si mrefu toka sasa! Furaha na matumaini yaliyoibuka baada ya maelezo ya bwana yule kwa hadhira ile yaliniwacha hoi bin taabani. Nilibaki najiwazia moyoni kwamba hivi watawala wetu wataifanya nini jamii hii ambayo kamwe haijui kuvunjika moyo na wanachokiamini? Kweli watawala wetu wataendelea kuwa madarakani ilhali watawaliwa hawako radhi nao? Nini itakuwa mustakbali na mwisho wa utawala huu na maisha ya wanaotawaliwa viwiliwili lakini kiroho wakimtii kiongozi wanayemuamini kwa udhati wa nafsi zao?

Baada ya siku mbili kisiwani Unguja, nilisafiri hadi kisiwani Pemba. Huko nako ndio hakusemeki. Kisiwa hiki siasa hulimwa shambani, ikavunwa kwa makapu, ikachambuliwa, ikatiwa nazi watu wakala wakashiba. Hapa nikakutana na mashamsham ambayo yalinipa somo, linaloongeza lile la Unguja. Hapa nakuta wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiwa wao ndio hawana raha kutokana na shindi na kujiamini kwa wenye kisiwa chao. Hapa wafuasi wa CCM ni mithili ya mayatima. Pamoja na kwamba wana dola yenye mizinga, vifaru na mabunduki, hawana raha na dunia imewanamia. Wamejinyweza vibarazani kana kwamba wao ndio walioporwa haki yao! Wamekata tamaa na wamekosa chembe ya nguvu na kujiamini.

Hili, inavyoonekana, limewatia khofu viongozi wa CCM na sasa wanaweka mikakati makhususi ili gwiji wa siasa za diplomasia, Maalim Seif, azuwiwe kuzungumza na Wazanzibari kwa namna yoyote ile. Naibu Katibu Mkuu wa CCM upande wa Zanzibar, Vuai Ali Vuai, aliingia kisiwani Pemba kwa kishindo. Akapita mtaa hadi mtaa, kijiji hadi kijiji, kubwa akiwasihi wafuasi wake wasikatishwe tamaa na maneno ya wapinzani! Ndipo nikajuwa kuwa kumbe wamekata tamaa ilhali serikali wanayo! Pamoja na wao kuwa na serikali yenye mizinga, mabomu na vifaru, bado wamejinyweza vibarazani mithili ya mayatima!

Nimekuwa mfatiliaji wa siasa za Zanzibar kwa kipindi kirefu sasa. Kubwa ambalo nimeweza kulibaini ni uwezo na ufundi wa raia wanyonge ambao hutumia silaha za kinyonge dhidi ya mtawala mwenye kila aina ya silaha za kisasa. Hali hii ya Wazanzibari kutokata tamaa imekuwa pigo baya lenye kuuteteresha utawala usio na ridhaa zao. Umadhubuti wa watu hawa, ndio chimbuko la kiongozi wao kupata nguvu za kuweza kuwasambaratisha waumini wa utawala wa mabavu na wafuasi wao.

Hata kama CCM ipo madarakani kwa njia za mabavu, kitendo cha jumuiya za kimataifa kuwafungia vioo kwenye kila nyanja wahitajio msaada, ni ishara ya wao kupigwa pande na dunia. Hali imekuwa mbaya kiasi cha wanafunzi wa elimu ya juu kutolewa mbavuni. Hali imekuwa mbaya kiasi cha watu wa CCM kuingia barabarani kama kiongozi fulani wa upinzani hakukamatwa! Hali imekuwa ngumu kiasi cha waziri mmoja wa serikali ya CCM kuwakemea maimamu wanaompa kipaza sauti Maalim Seif Sharif kuwasalimia Waislamu wenziwe! Haya yote ni ishara ya utawala kukosa mbinu na sasa wanalialia ili kupata huruma ya vyombo vya dola. Jee, iko wapi mizinga na mabunduki waliyodai kuwa nayo? Au mbele ya siasa za kidiplomasia hayo hayafuwi dafu?

Pale mwanzo, wafuasi wa CCM walikusanywa Kibandamaiti na Gombani ya Kale kuambiwa kuwa Maalim Seif ni muongo ambaye hujifungia hotelini Dar es Salaam, kisha akadai kwamba alikuwa Ulaya! Punde tukamsikia huyo huyo aliyesema hayo, akifyatuka kuwa Maalim Seif ni mtu mbaya sana, anawashawishi wahisani wasitowe misaada kwa Tanzania! Mwananchi wa kawaida anayetumia akili yake anajiuliza ashike lipi – la kujifungia hotelini pale Manzese au kwenda Ulaya kushawishi wahisani wasitowe misaada?

Jambo moja liko wazi kwamba Tanzania, kwa ujumla wake, ina hali mbaya kiuchumi. Zanzibar ndiko hakusemeki. Vilio kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa, wa kati na hata wadogo vimezidi kushika kasi. Wengi miongoni mwa wafanyabiashara wa kati, hali zao kiuchumi zimekuwa mbaya kiasi cha wengi kuwaza kuhamishia biashara zao nchi nyingine. Mmoja alipata kunidokeza wiki iliyopita kwamba pamoja na kuwa na mali nyingi kwenye maghala yake, hurudi nyumbani mweupe kama alivyokwenda kwenye biashara yake.

Sanjari na mengi yenye kuisibu Tanzania leo, suala la Zanzibar lililopelekea wafadhili kusitisha misaada yao ni chagizo jingine. Hali imekuwa mbaya na sasa lipo pia tishio la Umoja wa Mataifa kuiwekea Tanzania vikwazo. Hii imetokana na ripoti ya hivi karibuni ambayo imeonyesha uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu na uvizaji demokrasia. Hili ni pigo ambalo linatowa ishara ya namna siasa za mabavu za CCM zinavyozidiwa kete na siasa za diplomasia za Maalim Seif.

Inaonekana, kuliko mara nyengine zote huko nyuma ambazo CUF ilidai kushinda na kuibiwa ushindi wake na CCM, mara hii CUF imeamua kutembea na ushindi wao huo mfukoni. Wanapokwenda wanakwenda nao. Wanautoa, wanawaonesha wawaonao na wauowano, wanaushangiria, kisha wanautia tena mkobani wanaambaa nao. Kwamba kinachofanyika mwaka huu ni watu kulipiga joka kichwani! Na kwa wao, wana-CUF, ni kwamba tayari joka liko hoi kiasi cha kuomba msaada kwa nchi zenye njaa kupita Tanzania!

TANBIHI: Mwandishi wa  makala hii, Ahmad Abu Faris, anapatikana kwa simu nambari +255 774 581 264.

Leave a Reply