Zimebakia siku 65 tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kufanyika hapo tarehe 28 Oktoba 2020. Wananchi wa Zanzibar watapata fursa nyengine ya kumchagua Rais wa Zanzibar wanayemtaka, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani. Hii itakuwa ni mara ya sita tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Siasa za Zanzibar zina raha zake na wakati huo huo hujaa pia karaha. Raha ya siasa za Zanzibar hudhihirika hasa wakati wa kampeni, misafara na misururu ya magari, wananchi wanaojazana barabarani kushangiria misafara ya wanaokwenda na kutoka mikutanoni. Siasa zinazotawaliwa zaidi na ushabiki wa uumini wa kivyama kuliko kumtegemea mtu. Ni siasa zinazojengwa katika msingi madhubuti wa kiitakadi. Mzanzibari hahongwi kilo ya chumvi kumbadilisha msimamo wake. Kwa Zanzibar ni kazi kubwa kuibadilisha kura moja kutoka chama A na kuipeleka chama B.

Ama karaha za siasa za Zanzibar hushitadi pale fujo zinapotawala, baadhi ya wanasiasa kuishiwa na hoja na kujikita katika matusi ya nguoni, na hata kutumia makundi ya kihalifu kudhuru wapinzania wao. Wakati mwengine hata kusababisha mauaji au majeruhi makubwa na vilema vya maisha. Kubwa zaidi ni pale umma unapotilia shaka kuwa maamuzi yao hayaheshimiwi na vyombo vinavyosimamia haki. Mara zote Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imekuwa ikibebeshwa lawama za kutokusimamia uchaguzi huru na wa haki.

Hussein Mwinyi
Mgombea urais wa Zanzibar kwa CCM, Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, akiwa na baadhi ya viongozi wa chama chake Zanzibar.

Nauona uchaguzi huu wa mwaka 2020 nao hautakosa raha za kisiasa bali pia na karaha zake zimeshaanza mapema. Huu ni uchaguzi unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kati ya vyama viwili vikuu hapa Zanzibar (ACT Wazalendo na Chama changu cha Mapinduzi, CCM).

Kwa wanaofuatilia siasa za Zanzibar, kuna jambo linajidhihirisha kila uchao, jambo lenyewe ni kuwa chama changu cha CCM kimeshakubali kushindwa mapema kabla hata Oktoba 28 kufika.

Mapokezi ya Maalim Seif, Membe yalivyotuchanganya

Chama changu kilitangulia kupasha misuli pale kilipotangulia kumteuwa Mgombea wa Urais, Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, anayesifika kwa upole bali mgeni mno machoni mwa Wazanzibari walio wengi. Dk. Hussein alipokelewa kwa shangwe Zanzibar, kote Unguja na Pemba. Baada ya mwezi mmoja kupita, ACT nao walifuata kwa mapokezi makubwa, Unguja na Pemba.

Mapokezi ya wagombea urais wa Muungano kwa ACT Wazalendo, Benard Membe, na wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, kisiwani Unguja.

Ukitizama kwa jicho la uchambuzi, ni ukweli usio shaka kuwa mapokezi ya ACT hayakutarajiwa kuwa makubwa kwa kiasi kile. Jambo lile limetutiribuwa sana wana-CCM Zanzibar na Bara. Tulijilemaza kwa kudhani kuwa kusambaratika kwa CUF ni kusambaratika kwa Maalim Seif. Umri wa Maalim Seif nao hatukuutegemea kuvutia tena rika la vijana walio wengi Zanzibar. Tulijiaminisha kuchuka kwa Maalim Seif hasa baada ya kugombea mara tano mfululizo bila mafanikio.

Lakini sasa ni wazi kuwa Maalim ametushangaza sana. Wengi tunajiuliza nini siri ya mafanikio haya ya Maalim Seif kuwa kiongozi anayeungwa mkono na mwenye ushawishi kwa Wazanzibari kuliko kiongozi mwengine yeyote? Mapokezi ya Maalim Seif yametutia kiwewe. Yamekiacha Chama Changu kikiwa kimechanganyikiwa.

Nasema Chama Changu kimechanganyikiwa kwa  sababu hizi zifuatazo:

Kumuombea mauti Maalim Seif

Moja, hivi sasa Chama Changu sasa kinakesha mitandaoni kumuombea ugonjwa na kifo Maalim Seif. Wengi mutakuwa munashuhudia picha na ujumbe huo ukisambazwa. Unatoka kwenye Chama Changu, ambacho kutokana na kuchanganyikiwa kwetu, tumejisahau kuwa Maalim Seif ni binaadamu kama mwengine yeyote.

Anaweza kuumwa na kufa muda wowote kama alivyo binadamu mwengine yeyote. Karibuni tu, Tanzania imemzika rais wake wa tatu, Mzee wetu Benjamin Mkapa, ambaye hata hakuwa mgonjwa kiasi hicho, ila tu ahadi yake ilishafika.

Kwa utamaduni wa Kizanzibari, si jambo linalotarajiwa kwa mtu kukesha kumuombea mwenzako ugonjwa au kifo. Hii imenishtua  na tafsiri yake ni moja tu. Maalim katushika pabaya. Salama yetu ni kumuombea ugonjwa au kifo.

Najiuliza: hivi tukifika Oktoba 28 na Maalim Seif bado mzima kasimama mbele yetu na kwenye kipande cha kura yumo, tutakimbilia wapi? Hivyo Kisiwandui sasa kumekuwa na Israel tu, hakuna tena akili za kupanga mikakati ya ushindi?

Patashika-nguo chanika ya Kisiwandui

Pili, Kisiwandui kumeingia tafrani. Sasa Komredi Dk. Abdallah Mabodi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, anaonekana hatoshi tena. Fununu zilizopo sasa yupo njiani kufunga virago. Kijana machachari, Ayoub Mahmoud, ndiye anayetajwa kuchukuwa nafasi yake.

Napata tabu kuzifanyia kazi hesabu hizi. Kama Mabodi aliyejipanga kwa zaidi ya miaka minne sasa anaonekana hafai kukipa ushindi chama, ataweza Ayoub mwenye siku 65 tu?

Kuangushwa kwa wanakindakindaki wa Unguja

Tatu, kuna tafrani majimboni. Eti tunaamini kuwa Maalim Seif sasa ana wapambe ndani ya CCM na kwa hivyo jitihada zinafanyika kuhakikisha hawarejeshwi majimboni.

Mohamed Seif Khatib, mmoja wa wanasiasa wakongwe waliotupwa nje ya uteuzi.

Waheshimiwa kama Jaku Hashim Ayoub, aliyekuwa muwakilishi wa Paje na Mohamed Raza (Uzini) na Nadir (Chaani), wote hawa eti ni wafuasi wa Maalim Seif. Komredi Mohamed Seif Khatib na Mahadhi naye kaadhibiwa eti ni mfuasi wa Maalim Seif, muumini wa serikali tatu.

Hawa wote ni wanasiasa wa Kiunguja kindikindaki. Unawagawa ili iweje? Badala yake tumeletewa watu kama Abdallah Ali Hassan Mwinyi ambaye hata hakuwa wa pili wala wa tatu kwenye kura za maoni na kuachwa walioshinda. Je, hatuoni kwamba tunapaswa kwanza kujenga nyumba yetu iliyobomoka, kabla ya kuwekeza nguvu zetu kutengeneza vifurushi vya uzushi kusambaza mitandaoni dhidi ya Maalim Seif?

CCM Zanzibar kwenye ufunguzi wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015.

Lakini hizi ndio siasa za Ayoub anayetarajiwa kuchukuwa uongozi wa Chama kukipa ushindi chama kwenye uchaguzi wa mwaka huu. Kama ameanza kutugawa sasa, na akitumia mbinu za kitoto hivi mitandaoni, nani atatuunganisha na kuweza kupambana na Maalim?

Kiongozi wa Usalama wa Taifa aondoshwa Zanzibar

Nne, majuzi kumetokea kituko chengine. Aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa Zanzibar, ndugu yangu Said Shaibu (Chai) aliondolewa afisini katika hali isiyo ya kawaida. Said kanyanyuliwa kwenye kiti na kutakiwa kumpisha Ndugu Mussa Chigelo, mteule mpya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala. Najiuliza kitu hapa, ikiwa mwenye nyumba imemshinda kuilinda, ataiweza mpangaji?

Kuna na mengine mengi, leo sitaki kuyasema. Nataka kuacha ujumbe mfupi tu kwangu binafsi na kwa wana-CCM wezangu kuwa kwa mtindo huu, chama chetu kimekubali kushindwa mapema. Sioni njia ya kutokea kupambana na Maalim Seif, huku tukimsubiri afe.

Sina shaka yoyote kwa Maalim tumjuaye, atakuwa yupo pahala na vijana wake wamejifungia kujipanga, tusibiri kishindo chake. Kama cha mapokezi tu kimetufikisha hapa, cha kampeni sijui kitatufikisha wapi?

Nikishauri chama changu, turudi kwanza kuzima makundi yanayotula. Tupambane kwa pamoja. Kwa wenyeji wasimng’ong’e mgeni tuliyemkaribisha juzi. Ndio tumeshaletewa kutoka kuumeni huyo, hatuna jengine la kufanya zaidi ya kumuonesha vichochoro vya kupita.

Tumuweke pembeni kwanza Maalim. Maalim ana umma uliopo nyuma yake. Hii ndio jeuri yake. Dua ya mwewe haimpati kuku! Vyenginevyo tujiandae kisaikolojia kukabiliana na kipigo kuliko cha mwaka 2015.

Kisha tumlazimishe tena Mwenyekiti wa ZEC afute uchaguzi.

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kama Mkereketwa wa CCM, Kisiwandui. Maoni yake hayana uhusiano na mtazamo au msimamo wa mtandao wa Zanzibar Daima. 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.