Viongozi wawili waandamizi wa chama cha ACT Wazalendo, Nassor Mazrui na Ismail Jussa, wamechukuwa fomu hivi leo (19 Julai) kuomba ridhaa ya chama chao kuwania uwakilishi kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.

Mazrui, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa chama chake kwa upande wa Zanzibar, alichukuwa fomu asubuhi ya leo kwenye ofisi za jimbo la Mwera, ambalo ndilo analoomba kuliwakilisha kwenye uchaguzi huo.

Kwa upande wa Jussa, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo, amechukuwa fomu kuwania uwakilishi wa jimbo la Malindi. Jussa aliwahi kuwa mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe (2010-2015) na kisha kuwania na kushinda uwakilishi wa jimbo la Malindi kwenye uchaguzi wa Oktoba 2015 uliokuja baadaye kufutwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha, kwa madai ya ukiukwaji wa taratibu.

Hali ni sawa kwa Mazrui, ambaye naye aliwahi kuwa mwakilishi wa jimbo la Mtoni (2010-2015) na baadaye kuwania na kushinda jimbo jipya la Mtopepo kwenye uchaguzi mkuu wa 2015.

Hatua ya ZEC kuyakata tena majimbo ya uchaguzi miaka mitano baada ya kuyakata mwaka 2015 kumelifuta tena jimbo la Mtopepo na kuifanya sehemu ya jimbo la Mwera kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Viongozi hawa wawili wenye ushawishi mkubwa kwenye siasa za Zanzibar wamechukuwa fomu katika kipindi cha lala salama, ikiwa imesalia siku moja tu kabla ya muda uliopangwa na chama chao haujamalizika.

Uchaguzi mkuu wa mwaka huu unatazamiwa kuvikutanisha vyama vya ACT Wazalendo na chama tawala CCM kwenye ushindani mkubwa, kama ilivyokuwa ikitokea wakati viongozi na wanachama wa sasa wa ACT Wazalendo walipokuwa kwenye chama cha CUF baina ya 1995 na 2015.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.