Micheweni – PEMBA: Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepoteza wanachama wake saba Micheweni kisiwani Pemba kwa kukihama chama hicho na kuhamia ACT-Wazalendo.

Hivi leo (Julai 1), akiwa kwenye ziara ya kuimarisha chama chake, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Taifa), Maalim Seif Sharif Hamad, aliwapokea wanachama saba mashuhuri wa CCM na kuwakabidhi rasmi kadi za chama chao kipya.

Wanachama hao wamekabidhiwa kadi hizo katika mkutano wa ndani uliofanyika Konde Mkoa wa Micheweni kichama ikiwa ni muendelezo wa ziara ya Maalim Seif ya kuimarisha chama chake kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2020.

Waliokabidhiwa kadi hizo ni Asha Juma Mjaja, Laila Rashid Haji, Rashid Haji Juma, Kombo Said Kwale, Bakame Juma Mjaja, Rashid Ali Juma.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Taifa), Maalim Seif Sharif Hamad, akionesha moja ya kadi za waliokuwa wana-CCM waliojiunga na ACT Wazalendo kutoka Micheweni kisiwani Pemba, siku ya Jumatano ya tarehe 1 Julai, 2020.

Akizungumza na wanachama wa ACT-Wazalendo mara baada ya kuwakabidhi kadi wanachama hao wapya, Maalim Seif alisema kitendo cha wanachama hao kujiunga na ACT-Wazalendo ni ishara kuwa CCM imechokwa kisiwani Pemba na haikubaliki kwa wananchi.

“CCM inajidanganya bure. Pemba hawana lao na sisi tutahakikisha tunachukua majimbo yote licha ya mikakati yao miovu wanayoipanga,” alisema makamu huyo mstaafu wa Rais wa Zanzibar.

Aidha Maalim Seif amezitaka kamati za uongozi kisiwani Pemba kuhakikisha wanajipanga vyema ili kukipa ushindi chama hicho kwa kuongeza idadi ya wanachama wapya.

Kwa upande wao waliokabidhiwa kadi hizo, wamesema wamechoshwa na madhila ya ubaguzi yanayoendelea kufanywa na CCM, ukosefu wa ajira na umasikini ambavyo kwa muda mrefu imekuwa ni sehemu ya maisha ya wananchi wa Pemba.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.