Mwanasiasa wa siku nyingi visiwani Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, amechukuwa fomu kuwania uongozi wa juu kabisa wa chama cha ACT-Wazalendo, chama ambacho alijiunga nacho mwaka jana baada ya kukihama chama alichoshiriki kukiasisi cha CUF, kufuatia mgogoro wa kiuongozi kati ya kambi ya Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba na ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Jussa, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mikakati, Usimamizi na Ufuatiliaji kwenye ACT, alikabidhiwa fomu ya kuwania nafasi hiyo na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, mwanasheria Omar Said Shaaban katika Ofisi ya ACT Vuga, mjini Zanzibar, mapema leo (Februari 25).

Mwenyekiti wa Kamati ya Habari na Uenezi ya ACT Wazalendo, Salim Bimani (kushoto) akikabidhiwa fomu ya kuwania ujumbe kwenye Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho na Katibu wa Uchaguzi, Muhene Said Rashid, siku ya Jumanne (Februari 25, 2020) ofisi za Vuga, Zanzibar.

Jussa anakuwa mwanachama wa tatu wa ACT Wazalendo kuomba ridhaa ya kuwania nafasi hiyo, akitanguliwa na kiongozi anayetetea nafasi yake, Zitto Kabwe, na Joseph Mona, ambaye hivi sasa ni Katibu wa mkoa wa Katavi.

Akisindikizwa na wanasiasa wengine mashuhuri kwenye uchukuwaji fomu huo, Mohamed Ahmed Mugheir (Eddy Riyami), Salim Bimani na Mansour Yussuf Himidi, Jussa aliwaambia waandishi wa habari kuwa ana imani chama chake kitamruhusu kuwania na pia kumchaguwa kukiongoza kwenye nafasi hiyo ya juu kabisa, kutokana na uwezo na uzoefu wake mkubwa kwenye masuala ya siasa.

Kwenye shughuli ya kukabidhiana fomu, Mwenyekiti wa sasa kamati ya Habari na Uenezi ya ACT Wazalendo, Salim Bimani, naye pia alichukuwa fomu ya kuwania nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho kwenye uchaguzi unaotazamiwa wakati wowote kutoka sasa.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.