Waafrika na Waarabu: “Sisi Wazuri, nyinyi Waovu” au “Sisi Wazuri, na nyinyi Wazuri?”

Wengi tumeshuhudia katika mitandao tarehe 16 Oktoba, 2019, vinyago vya kustaajabisha sana kwa mtu yoyote ambaye anao uwezo wa kutumia akili yake vizuri. Tumeona ya mtu mmoja kavaa mavazi ya Kiarabu/Kiomani na kumchukua mtu aliyevaa winda na minyororo kama mtumwa wake na huku wakipita sehemu za Kariakoo, Dar es Salaam, wakitangaza kuwa asiyejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa atakuwa kama mtumwa wa Waarabu/Womani! Kwani atakuwa hana uwezo wa kuchagua viongozi wake. Kuyakoroga hayo mawili ni kufilisika kwa akili.

Bado nashindwa kuelewa maudhui ya hii picha na video; je, kura ni kwa manufaa ya mtumwa au ya huyo bwana wa Kiarabu/Kiomani? La kustaajabisha ni kuwa Waarabu na utumwa na kupiga kura kunakhusiana nini, ila kwa mtu asiyeweza kutumia akili yake vizuri?

Iwapo lengo la waliobuni uzembe huo ni kuteka fikira za wapumbavu basi huenda wakafuzu, lakini kwa mwenye akili zake timamu huwa anaona waziwazi kuwa hayo mawili hayana alaka yoyote ile ila ya kuzidi kutia chuki baina ya Watanzania na wananchi na dola za Kiarabu, na baina ya nchi na Serkali zao.

Ni ushenzi wa hali ya juu kabisa khasa ukielewa pia ukweli wa historia inayowakhusu Waarabu Waislam (si Waarabu wote Waislam) na biashara ya utumwa na kulinganisha na waliyofanya makabila ya Kiafrika na mengineyo; ni kudhihirisha pia kuwa propaganda ya sumu inayosomeshwa katika shule za Tanzania kweli imewaingia na kujaa katika bongo za waliosomeshwa historia shuleni. Historia iliyojaa yasiyokuwa ya kweli yenye kutapakaza chuki dhidi ya Waarabu na khasa Waomani kwa kusudio la kuuchukiza Uislamu, kwani maneno hayo mawili: “Mwarabu” na “Mwislamu” na “Muafrika” na “Mkristo” hutumiwa na Wamishinari na wafuasi wao kama maneno mbadala. Bahati mbaya hata baadhi ya Waislamu wamelishwa na kuathiriwa na sumu hio.

Katika dhambi kubwa waliyoifanya Wamishinari na wakoloni wao katika Afrika Mashariki na Kati ni kuwafundisha wanafunzi wa Kiafrika taarikhi ya biashara ya utumwa yenye ukweli finyu na uwongo mwingi. Ukweli ulio mchache ni kuwa biashara hiyo kweli ilifanywa Afrika Mashariki na Kati. Ya uwongo ni kuwa biashara hiyo ilifanywa na Waarabu au Waislamu peke yao – kuanzia ukamataji wa makabila dhaifu, usafirishaji wa miguu wa wanyonge hao kutoka bara hadi pwani ya Afrika Mashariki, uuzaji wa mateka hao sokoni, hadi utumiaji wa watumwa mijini na mashambani – Walisomesha Wamishinari na wakoloni wao wakati wa ukoloni na leo warithi wao, wafuasi wao wa Kiafrika, wanaendelea kusomesha katika shule za Afrika Mashariki upotofu huohuo. Walifika hadi ya kuiita biashara hiyo ya utumwa “Biashara ya Utumwa wa Kiislamu” na pia “Biashara ya Utumwa wa Kiarabu” wakati hatujapatapo kusikia “The Atlantic Slave Trade” kuitwa “Biashara ya Wazungu” au “Biashara ya Wakristo.”

Hayati Samuel Sitta, aliyekuwa spika wa bunge la Tanzania akizungumza na Watanzania wanaoishi nchini Uingereza kabla ya kifo chake.

Wamishinari walioanzisha usomeshaji wa propaganda hii walifanya hivyo kwa sababu walijiona kuwa bado wamo katika Vita vya Msalaba na Waislamu na kuwa lengo lao ni kuwasomesha wanafunzi wa Kiafrika (ambao baadhi yao walikuja kuwa viongozi wa juu) kuwa wao Wakristo ni watu wazuri sana na Waislamu ni watu wabaya sana. Hii nembo ya “sisi ni watu wazuri sana na nyinyi watu wabaya sana” ndiyo inayotumiwa mpaka leo katika siasa chafu zilioko katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Tanganyika na Zanzibar – Ni siasa zilizojaa chuki dhidi ya watu fulani na vyama fulani na ni siasa za upotofu na udanganyifu uliolenga kuzidi kujipotosha na kuwapotosha wale ambao tayari wameshapikwa na sumu za chuki waliposomeshwa shuleni na kwenye taasisi za kivyama na za kipropaganda.

Kongo imepakana na Tanzania na wakati wa ukoloni Wabilgiji waliwatia mamilioni ya Wakongo utumwani na zaidi ya milioni kumi ya Wakongo waliuliwa kinyama kabisa na Wabilgiji. Inasemekana kuwa mauwaji hayo ya kimbari ndiyo yaliyokuwa makubwa kabisa duniani; lakini wamishinari haohao hata siku moja hawakusomesha utumwa huu wa Wakongo na mauwaji hayo ya kimbari. Jee, umepata kusikia utumwa huo na mauwaji hayo kuitwa ya “Kikristo” au ya “Kizungu.” Utumwa huo na mauwaji hayo kutaja hawayataji katika shule za Tanzania. Una shaka yoyote juu ya sababu za kutokusomesha ukweli huu?

Lakini, hakuna kiongozi mkweli au mwana historia wa kweli ambaye hajui kuwa biashara ya utumwa ilitendwa kwanza na makabila makubwa yaliyokuweko Afrika Mashariki na Kati kama Wayao, Wangoni, Wanyamwezi, Wamanyema, Wasukuma na wengi wengineo walikamata watu wa makabila madogomadogo na kuwatia utumwani na kuwatumia wao wenyewe na wengi wengine kuwauza kwa atakaye kuwanunua.

Watekaji hao wa Kiafrika walisafirisha kwa miguu mateka wao wengi sana si Bagamoyo na Zanzibar bali waliwapeleka Maputo (Lorenzo Marques), Msumbiji na sehemu nyeginezo ambazo zilikuwa chini ya utawala wa Kiportugizi; ndiyo mana leo kuna watu wenye asili za Kiafrika wasiopungua mia milioni katika lililokuwa koloni lao la Brazil na mpaka leo vizazi vyo wanaonekana ni watu duni huko, na wenyewe wanajiita na wanaitwa “Afro-Brazilians.” Kutoka Agentina mpaka Kanada kuna vizazi vya watumwa wa Kiafrika kama milioni mia mbili. Iwapo Waarabu peke yao ndio walioifanya biashara hiyo, watumwa hao kwa mamilioni wako wapi leo Arabuni? Mbona, kwa mfano, hatuwaoni wala hatusikii kuna watu wanaojiita kwa mfano “Afro-Omanis”? Muomani awachukue watumwa wa Kiafrika awapeleke Omani, kwenye ardhi ya majabali, mawe na jangwa wakafanye nini?

Hali kadhalika, makabila ya Kiafrika yalipigana wenyewe kwa wenyewe na walioshindwa walichukuliwa mateka na wengi wao kuwauza utumwani. Hakuna Mwarabu aliyekwenda bara katika Afrika mashariki kuwakamata watu na kuwaleta pwani kuwauza. Hata Tipu Tip – amabaye ni mzaliwa wa bara na mama yake ni Mwafrika – katika hiyo mara yake moja ya kuwakamata wanyonge hakuwapeleka pwani mateka hao; aliwauza hukohuko Bara. Narejelea kusema tena, hakuna Mwarabu hata mmoja aliyekwenda bara kwa mapana na marefu kukamata watumwa na kuwapeleka pwani kuwauza. Waarabu waliokwenda bara katika Karne ya Kumi na Tisa, akina Rumaliza na Al-Bushiri walikuwa wakiwasaidia ndugu zao wa Kiafrika kupigana dhidi ya wakoloni wa Kijarumani. Hawa wenye kuzipepea chuki hata mchangayiko baina wa Waafrika na Waarabu basi hupewa jina chafu la “Machotara.”

Vidio hii ilichukuliwa katika miaka ya mwanzoni kabisa baada ya kuangushwa serikali ya Zanzibar.

Nimeambatanisha video zenye kudhihirisha kuwa hata wakuu wa serikali wanapalilia siasa za kibaguzi na chuki dhidi ya Waislamu msikie maneno yao wenyewe, ili yasiwe ya kuhadithiwa.

Propaganda hii ya “sisi Wakristo ni watu wazuri sana na nyinyi Waislamu/Waarabu ni watu waovu sana” ndiyo iliyotumiwa katika siasa za Zanzibar na kusababisha vifo vya kimbari (genocide) vya watu wasiokuwa na hatia yoyote katika mavamizi ya makatili kutoka Tanganyika mnamo Januari 1964. Wanawake wengi waliingiliwa kwa nguvu na kuraruliwa, watu wengi walifungwa bure na kuadhibiwa, wengi walinyang’anywa mali zao, wengi walifukuzwa makazini, yote haya yalifanywa na wanaodai kuwa “sisi ni watu wema”. Katika siasa zao walizitumilia sana, tena sana, nganu zao za utumwa na kila kukicha walikuwa wakiongeza na kukhubiria hadithi mpyampya walizozitunga wenyewe kwa lengo la kuzidisha chuki.


Katika siasa za Tanzania za jana na za leo, baada ya zaidi ya nusu karne ya kujitawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) hakiwezi kujiepusha na siasa za chuki khasa ukikurubia uchaguzi na mkipeleleza mtaona kuwa wanapokhubiri hawawezi kuepukana na hiyo siasa yao moja isemayo “sisi ni wazuri kwa sababu nyinyi ni waovu”. Sisi ni wazuri tumejijengea shule kwa sababu nyinyi ni waovu hamkutujengea shule. Sisi ni wazuri tumejijengea hospitali kwa sababu nyinyi ni waovu hamkutujengea hospitali. Sisi ni wazuri tumejijengea barabara kwa sababu nyinyi ni waovu hamkutujengea barabara, na kadhalika na kadhalika, ambayo mantiki yake ndiyo hiyohiyo moja tu tuliyoitaja. Haiwi kwao kuwa tumejenga uwanja wa ndege, kwa mfano, kwa sababu umefika wakati wa kujengwa huo uwanja mpya kwa sababu ya mahitaji ya leo. La, lazima pawe na majisifu ya kibinafsi na kichama na majisifu hayo lazima yawatweze waliokwisha kutangulia mbele ya haqi zamani pamoja na wale wanaowanyooshea kidole cha lawama milele – Waarabu na khasa Waomani, na Waislamu kwa jumla.

Waziri Mwandamizi kwenye Serikali ya Muungano, William Lukuvi, akizungumza na waumini wa Kikristo kanisani, Dodoma Tanzania.

Fikra na hisia potofu za aina hii ambazo zinapewa uhalali na Chama na Serikali ni ishara ya utumwa wa kiakili katika karne ya 21 kuliko hapo biashara ovu ya utumwa ilipofikia kilele katika karne ya 19. Hebu kaa uzingatie. Leo tuko mwaka 2019 viongozi na uongozi wa CCM na vyama vyengine vya upinzani na hata Serikali yenyewe ya Tanzania hawakemei ujinga, chuki, na fitina, ambazo zinatanganwa na kuuzwa waziwazi Kariakoo! Ni chama kimoja tu cha ACT ambacho kimetoa kauli ya wazi ya kupinga fitna na uovu huo.


Baada ya kuzingatia haya jiulize: Nini athari ya propaganda chafu na fikra finyu dhidi ya Waarabu na khasa wakikusudiwa Waomani, juu ya miradi mikubwamikubwa kama:
• Mradi wa Bagamoyo wa China na Oman
• Mradi wa bwawa la Stiegler’s Gorge la kutoa umeme liliopo Rufiji ambalo linasimamiwa na Waarabu kutoka Misri
• Mradi wa Ras el Khaima wa kuchimba mafuta Zanzibar
• Mradi kutoka Abu Dhabi wa kuwasaidia vijana wa Kizanzibari
• Mradi wa Oman wa mitambo ya uchapishaji
• Mradi wa Oman wa ukarabati wa jumba la Beit-al-Ajaib
• Mahusiano baina ya Waislam na Wakristo Tanzania na mahusiano ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki na Kusini ambazo zina mahusiano mazuri na CCM na Serikali ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania?

Safari zisokwisha za Arabuni na kauli za uwepo wa udugu wa kidamu na wa kidhati baina ya Tanzania na Oman na nchi za Kiarabu na khasa za Ghuba hazitotufikisha kunako masikilizano na neema mpaka pale kauli mbiu ya “Sisi Wazuri, Nyinyi Waovu” itakapobadilishwa kwa vitendo kwa kauli mbiu ya “Sisi Wazuri, Nyinyi Wazuri.”

Tuwacheni ujinga. Sisi ni waumini wa Nabii Issa, Nabii Muhammad, na Nabii Musa. Sote ni watoto wa Mungu. Tujichunguze na tuachane na fikira za kishetani na tuangalie wapi tulipokosea katika kujiletea maendeleo. Kuendelea kuwalaumu Waarabu, Waomani, na Waislam, ni jitihada na dalili za kutosha za kukosa kujitathmini kisawasawa na kujiamini katika kujiletea manedeleo bila ya msingi wa chuki au kumchukia mtu au watu fulani kwa ajili ya asili au dini zao.
Tukumbuke msimu wa chaguzi umeshaanza kwa kujiandikisha katika uhaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara ambao utafanyika rasmi tarehe 24 Novemba, 2019. Oktoba/Novemba ya mwakani (2020) kutakuwa na Uchaguzi Mkuu Tanzania Bara na Zanzibar.

Tunamuomba Mungu wetu Mmoja atuweke hai tushuhudie kudhoofika na kutoweka kwa chuki na fitina za Kimishanari na Kikoloni Tanzania na kuimarika kwa mahusiano ya mapenzi ya kweli baina ya wananchi na Serikali zetu.
Hapana shaka kuna siku yatakwisha.

Imeandikwa na Ibrahim Noor
Ijumaatatu, tarehe 23 Oktoba, 2019

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.