YUKO jela kama hayuko jela. Ndivyo tunavyoweza kumuelezea Omar Hassan al Bashir, rais wa zamani wa Sudan, aliyetawala kwa miaka 30 hadi Aprili mwaka huu wanajeshi wenzake walipomwondoa madarakani. Siku hizi, akiwa amefungwa katika gereza la Kober, ana mizaha mingi na anasema kama chiriku, pengine akiwa anashindana na mbu wanaohanikiza gerezani humo.

Al Bashir ni mtu wa soga na mizaha lakini siku hizi hashikiki. Anapenda kupiga soga na wafungwa wenzake pamoja na wanaomzuru alikofungwa kaskazini mwa Khartoum.

Hayo na mengine yalianikwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye mtandao wa Arabi21.

Na Ahmed Rajab

Inasemekana kwamba hali yake ni nzuri na hakuchanganyikiwa kiakili. Kila siku anapelekewa chakula kilichopikwa nyumbani kwake. Al Bashir hana uchoyo kwani anakila pamoja na mwenzake aliyefungwa naye chumba kimoja Hamid Siddiq, kaimu katibu mkuu wa Vuguvugu la Kiislamu la Sudan lililoasisiwa 1999.

Vuguvugu hilo lilikuwa kama chanda na pete na chama cha al Bashir cha National Congress (al- Mu’tamar al Watani).

Ingawa jela ni jela lakini mambo ya al Bashir na mwenzake si mabaya. Chumba chao kina mtambo mdogo wa kuyafanya maji ya kunywa yawe baridi na kuna kijifriji cha kuwekea dawa za al Bashir.  Bafu moja limeunganishwa na chumba hicho. Na kila siku wanapewa magazeti ya kusoma. Kwa hivyo, ya nje wanayajua.

Inatazamiwa kwamba mwishoni mwa mwezi huu al Bashir atafikishwa mahakamani Khartoum akishtakiwa kwa makosa ya kuzitakasa fedha zilizopatikana kwa njia chafu.   Atabidi pia aieleze mahakama alizipata wapi fedha chungu nzima alizokamatwa nazo akiwa hana uthibitisho wa kisheria.

Vile kwamba al Bashir haonekani kuwa na wahaka kunathibitisha maoni ya wengi wenye kuamini kwamba Baraza la Kijeshi la Mpito linalotawala sasa limemhakikishia yeye pamoja na vigogo wengine waliokuwa kwenye serikali yake kwamba hakuna kubwa litalowafika. 

Tayari Baraza hilo lilikwishatangaza kwamba halitompeleka kwenye Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) jijini Hague kuyakabili mashtaka aliyoshtakiwa na ICC ya kuhusika na uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan.

Mahakama ya ICC yalitoa waranti ya kwanza Machi 4, 2009 ya kutaka al Bashir akamatwa popote alipo na afikishwe mbele ya Mahakama hayo.  Waranti ya pili ilitolewa Julai 12, 2010. Al Bashir ni rais wa mwanzo aliyekuwa madarakani kukabiliwa na waranti kama hiyo. Hadi sasa amekwepa asikamatwe alipokuwa ziarani katika nchi kadhaa zikiwa pamoja na Afrika Kusini na Kenya.

Watawala wa sasa wa kijeshi wanamkinga al Bashir kwa sababu baadhi yao pia huenda wakakabiliwa na mashtaka kama hayo yanayomkabili al Bashir.

Ukweli wa mambo ni kwamba al Bashir alipoangushwa Aprili mwaka huu, aliyeangushwa alikuwa ni yeye binafsi lakini si utawala wake. Na huo utawala wake, au mabaki ya utawala wake, ndio unaomkinga hivi sasa. Unamkinga yeye na, wakati huohuo, unajikinga wenyewe.   Ndio maana wenye kuuongoza wanafanya ukaidi kuondoka madarakani moja kwa moja.

Ni miezi saba sasa tangu wananchi wa Sudan waanze kumiminika barabarani wakipinga muongezeko wa bei ya mkate. Hatimaye wakaanza kuupinga mfumo mzima wa utawala nchini mwao.  Dai lao kubwa lilikuwa kutaka al Bashir auache uongozi wa nchi.

Wakidai demokrasia halisi, demokrasia ya kweli.  Miaka yote hii tangu al Bashir anyakue madaraka 1989 hawakuishuhudia demokrasia aina hiyo.

Demokrasia aliyojigamba al Bashir kuileta alipoipa Sudan katiba mpya 1998 na aliporuhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa ilikuwa ni demokrasia laghai, demokrasia ya kuudanganya ulimwengu.

Ukakamavu wa waandamanaji na wa kambi nzima ya upinzani, kwa jumla, uliwatikisa watawala wa kijeshi kiasi cha kuwafanya wawe tayari kumtoa mhanga al Bashir ili wanusurike pamoja na mfumo wao wa utawala.

Na ndivyo ilivyokuwa Aprili 11. Walifanya al Bashir kafara walipomwangusha siku hiyo na badala yake wakaunda Baraza la Mpito la Kijeshi kuendesha nchi.  Wapinzani hawakuridhika na waliapa kwamba hawatosita na harakati za vuguvugu lao Muungano wa Uhuru na Mageuzi mpaka jeshi litapoyaacha madaraka na kuwakabidhi raia.

Mvutano baina ya pande hizo mbili uliendelea kwa muda wa wiki kadhaa.  Katika “vuta n’kuvute” hiyo wanajeshi walituhumiwa kuwaua waandamanaji wasiopungua 200, wengi wao waliuliwa wakati wa migomo mikuu ilioifanya takriban nchi nzima ife ganzi. Zaidi ya mia moja waliuliwa Juni 3 pale wanajeshi walipowavamia waandamanaji na kuwatawanya.  Inasemekana kwamba watu wasiopungua 70, wanawake na wanaume, walibakwa siku hiyohiyo moja.

Jitihada za usuluhishi za waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed hazikufanikiwa. Mapendekezo yake ya kuleta suluhu yalikataliwa na wanajeshi walioshauri kwamba Abiy ashirikiane na Muungano wa Afrika (AU) uliokwishapeleka ujumbe wake wa usuluhishi Khartoum, ukiongozwa na  Profesa Mohamed el Hacen Lebatt, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Mauritania mwenye uzoefu mkubwa wa migogoro ya kisiasa ya nchi kadhaa za Kiafrika.

Hatimaye mapema Ijumaa iliyopita watawala wa kijeshi na wapinzani walitangaza kwamba walifikia mapatano. Makubaliano hayo yalipatikana kwa upatanishi wa Kiafrika uliofanywa na Abiy pamoja na AU.  Huo ni mfano wa karibuni kabisa wa Waafrika kuyatanzua wenyewe matatizo yanayozuka katika nchi za Kiafrika.

Hata hivyo, tumepashwa habari pia kwamba Marekani na mataifa ya Kiarabu yaliyo na urafiki mkubwa na Sudan yalizishinikiza pande hizo mbili zifikie makubaliano ya haraka.

Mapatano yaliyofikiwa yana dosari kadhaa. Ukiyachunguza kwa makini utaona kwamba ingawa upinzani haukuondokea patupu, hata hivyo umeshindwa kuyapata baadhi ya madai yake makuu. Kubwa kabisa ni lile lililowataka wanajeshi waondoke madarakani halan, bila ya kuchelewa na madaraka wapewe raia.

Ilivyo, kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa, ni kwamba jeshi litaendelea kuwa na nguvu za uongozi. Ingawa Baraza la Mpito la Kijeshi litavunjwa Baraza Kuu la Nchi litaloundwa kushika mahala pa Baraza la Mpito litakuwa na wajumbe wa kijeshi wa tano, na wa kiraia watano pamoja na mwengine aliye huru atayeteuliwa kwa ridhaa ya makundi hayo mawili.

Kwa muda wa miezi 21 ya mwanzo Baraza hilo litakuwa chini ya mwanajeshi.  Kwa miezi 18 itayofuata litaongozwa na raia na wanajeshi wameahidi kwamba wakati huo watarudi kambini.  

Serikali itayowajibika kwa Baraza Kuu itaundwa na raia ikiongozwa na waziri mkuu aliye raia wa kawaida. Serikali hiyo itaiendesha nchi kwa muda wa miaka mitatu na itafanya matayarisho ya uchaguzi mkuu.

Baraza la Kutunga Sheria litaundwa miezi mitatu kutoka sasa.

Walikubaliana pia kwamba uchunguzi huru ufanywe kuhusu mauaji ya waandamanaji waliouliwa Juni 3.  Wanajeshi hawataki pawepo na mkono wowote kutoka nje ya nchi katika uchunguzi huo. Watu wanajiuliza: kwanini?

Jambo la kushangaza ni kwamba kiongozi wa kijeshi anayeonekana kuzidi kupata nguvu ni naibu wa mkuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi, Jenerali Mohamed Hamdan Dagolo, maarufu kwa jina la Hemedti.

Wanajeshi wa Sudan hawaaminiki. Kuna wengi wenye hofu ya kwamba watayaendea kinyume makubaliano yaliyofikiwa licha ya kusisitiza kwa mkuu wa Baraza la Kijeshi, Jenerali Abdel Fattah al Burhani na naibu wake Hemedti kwamba watayaheshimu na kuyatekeleza.

Kwa vitendo na hatua walizochukua wanajeshi wanaonesha kuwa na lengo la kuyasoza mapinduzi, kuyahilikisha na kuyaangamiza moja kwa moja. Kwa sababu ya hiyo dhamira yao wanaungwa mkono, kwa kiwango kikubwa, na Saudi Arabia, Misri pamoja na Muungano wa Tawala za Kifalme katika Ghuba (UAE). 

Nchi zote hizo tatu, na zaidi UAE na Saudi Arabia, hazitaki kabisa iibuke serikali ya kidemokrasia iliyochaguliwa na wananchi nchini Sudan.  Hazitaki kwa sababu zinaona huo utakuwa mfano mbaya utaoweza kuigwa na wananchi wa nchi zao.

Kwa kuyakubali mapatano yaliyofikiwa upande wa upinzani nao umedhihirisha udhaifu wake. Udhaifu huo umesababishwa na mambo kadhaa. La mwanzo kabisa ni kushindwa kutimiza lengo lake kuu la kutaka livunjwe halani, bila ya kukawia Baraza la Mpito la Kijeshi.

Kibarua kikubwa kinachowakabili sasa wapinzani ni kukubaliana kuhusu muundo wa serikali na hasa nani awe waziri mkuu wake.

Tunasikia kuna nyufa ndani ya jeshi na pia kwenye mwavuli wa upinzani wa Vuguvugu la Uhuru na Mageuzi. Jeshi litajaribu kuzitumia tofauti zilizopo miongoni mwa wapinzani ili lizidi kuwagawa lipate kuendelea kuwakalia vichwani na kuwatawala. Likifanya hivyo litakuwa linacheza na moto.

Pakiripuka tena Sudan huenda ikenda arijojo.  Hata bila ya mgogoro huu uliopo sasa, jeshi linakabiliwa na kazi kubwa ya kuyamaliza mapigano katika majimbo ya Darfur, Nuba Mountains na Blue Nile.  

TANBIHI: Makala hii ya Ahmed Rajab ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Raia Mwema la Juni 11-16, 2019. Mwandishi anapatikana kwa baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.