WAKATI fulani miaka mitano hivi iliyopita, nilikuwa nazungumza na rafiki yangu ambaye ni mtaalamu wa benki. Wakati huo alikuwa mkurugenzi wa mikopo kwenye benki moja ya kimataifa.

Nikamuuliza ni kwa nini mabenki hayawapi ubalozi mastaa wa Kibongo wakati wanafanya biashara na Wabongo? Nilimtolea mfano Wema Sepetu. Ni maarufu sana. Anapendwa sana. Hakuwa balozi wa taasisi yoyote ya kibiashara.

Alinijibu kwamba biashara ya benki ni nyeti sana na huhitaji uangalizi wa hali ya juu. Huwezi kutangaza bidhaa za benki na mtu ambaye hujui kesho ataandikwa nini na vyombo vya habari. Habari moja ya skendo inaweza kusababisha watu wajae benki kuhamisha fedha zao na kupeleka kwingine.

Luqman maloto
Na Luqman Maloto

Hapa nikaelewa kuwa kumbe inawezekana kuna taasisi nyingi za kifedha zingetamani kufanya kazi na mastaa wengi Bongo, lakini zinaogopa lifestyle zao. Kwamba mastaa hawaaminiki. Hawakawii kuzalisha skendo. Taasisi zinaogopa kuharibu brand zao kwa kujifunga na watu waliozungukwa na wingu la kashfa.

Hii inanikumbusha pia stori moja ya mwaka 2013. Mwanamuziki mmoja maarufu sana Bongo, alikosa dili la ubalozi wa kampuni ya simu za mkononi baada ya kushauriwa na kiongozi serikalini kuwa angechafua brand kutokana na mikashfa kibao aliyokuwa nayo.

Tunabaki hapa; lifestyle huweza kumjenga au kumharibu mtu kibiashara. Mtu ambaye hawezi kuwekewa dhamana kama anaweza kumaliza siku salama bila kuzua jambo, ni vigumu kwa taasisi zenye kulinda heshima zao kumpa mkataba wa matangazo.

TUNA WEMA NA ZARI

Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ni Mganda. Ni mwanamke mrembo, mzuri. Ni staa. Jinsi maisha yake anavyoyaendesha unaona kwamba ana kila kitu ambacho kila mwanamke wa Tanzania angependa kuwa nacho.

Ongeza kuwa Zari ana uzazi mzuri. Ni mama wa watoto watano. Ukimwangalia ni kama akiamua anaweza kuongeza. Jinsi anavyojiweka, ukiambiwa hajawahi kuzaa huwezi kupinga. Anaishi kileo, lakini yupo imara sana kulinda heshima yake.

Wema ni mrembo wa Tanzania. Taji la Miss Tanzania 2006 ni halali yake. Ni maarufu na anapendwa. Wanamwita Tanzania’s Sweetheart. Kwa miaka mingi amekuwa shauku ya wanaume wengi. Hupigiwa misele mingi. Hili si la uongo wala mapambio.

Umaarufu wa Zari Bongo ulianza mwaka 2014 alipoanza kutoka na supastaa Diamond Platnumz. Wema ni maarufu Bongo kabla ya Diamond. Hata wakati Diamond anaanza kudeti na Wema, ilionekana pasipo shaka kuwa mrembo huyo alikuwa anampa busta Diamond.

Bongo ndiyo himaya ya Wema. Zari kamkuta Wema ni staa sana. Ndani ya miaka mitano ya Zari kusimika maguu yake Bongo, amegeuka na thamani kubwa kuliko Wema. Zari alishaachana na Diamond zaidi ya mwaka sasa, lakini anaingia Bongo, anatengeneza pesa na kusepa zake. Swali; Wema anakwama wapi?

Je, Zari anatumia kizizi gani ambacho Wema hana? Wema umaarufu wake si wa kubebwa. Ni nyota yake mwenyewe. Zari umaarufu wake Bongo ni wa kubebwa na Diamond ambaye wameshaachana. Sasa mbona Zari wa kubebwa anatusua kuliko Wema mwenye nyota yake? Zari ana kizizi.

Tuje hapa; Ni kweli Zari ana kizizi. Lifestyle ndiyo kizizi chenyewe. Kupitia mtindo wa maisha wa Zari utakiona kizizi chake katika maeneo manne. Mosi, anavyojitambua. Pili, anavyojiweka. Tatu, anavyojilinda. Nne, jicho la fursa.

Zari anajikubali sana. Anajitambua yeye ni nani na anataka nini kwenye maisha. Namna anavyojiweka inakulazimisha umheshimu. Umwone ni mwanamke mwenye hadhi kubwa. Brand safi. Hana njaa na ametosheka. Anajipambanua kuwa hategemei mwanaume kuishi.

Yupo tayari kuutesa na kuushinda moyo wake ili kulinda heshima yake. Alimwacha Diamond akimpenda na tayari alikuwa ameshamzalia watoto wawili. Sababu alimwona anamdhalilisha. Kosa la Diamond lilikuwa kumkumbatia Wema na picha kusambaa mitandaoni.

Zari alihoji: “Kwa nini akumbatiane na ex girlfriend wake?” Inafahamika kuwa kuna nyakati Zari alikuwa akivutana na kurushiana madongo mitandaoni na Wema. Sababu ikiwa Diamond. Sasa kitendo cha Diamond kukumbatiana na Wema ilikuwa sawa na kuuza mechi. Akasema imetosha na hakurudi nyuma.

Kabla ya hapo Diamond alikuwa ameshazaa na modo Hamisa Mobeto lakini alimsamehe. Pamoja na manyokanyoka mengine, Zari akampiga chini. Zimefanyika jitihada nyingi za kuwasuluhisha, Zari aligoma katakata.

Huyo ndiye Zari, anapoamua kuidai heshima yake, yupo tayari kupoteza chochote chenye thamani. Na hicho ndicho kinamfanya abaki kuwa mwanamke bei mbaya. Amejipambanua kuwa maisha yake hayategemei nguvu ya mwanaume. Mwenyewe anajiweza mpaka chenji inarudi ya kutosha.

Tuje kwa Wema; mwaka 2012 kwenye shoo ya Diamonds Are Forever, Mlimani City Dar, Diamond aliwahi kumchoresha Wema vibayavibaya mbele ya malfu ya watu na kamera za vyombo vya habari. Wema alienda jukwaani kumtuza Diamond ambaye alimpuuza. Wema akaganda kusubiri Diamond apokee lakini wapi! Baada ya muda, Wema na Diamond walirejea tena mapenzini.

Mwaka 2013, Wema alimpigia simu Diamond kumwomba wamalize tofauti zao. Diamond alimrekodi sauti kisha akaisambaza mitandaoni na kwenye vyombo vya habari. Sauti ya Wema ikasikika akishushuliwa na zilipendwa mwingine wa Diamond, Penniel Mwingilwa ‘Penny’. Haukupita muda mrefu, Wema na Diamond walirejea kwenye penzi zito.

Hapo ndipo unaona tofauti ya Wema na Zari. Kimsingi Wema hajui kutetea heshima yake. Alimwacha Diamond amgeuzegeuze kama chapati. Diamond kwa Zari ameshika adabu. Ameona muziki wake. Zari si mwanamke wa kuchezewa.

Pamoja na Diamond, bado Wema amekuwa ni malkia wa skendo. Kashfa nyingi na wanaume. Amekuwa akijipambanua kuwa mwanamke tegemezi kwa wanaume. Hili linamshushia thamani.

ZARI NA FURSA

Juzi Zari alitua Bongo kama malkia fulani hivi. Mapokezi aliyopata ni ya ki-5Star. Alikuja kwa ajili ya mradi wa nepi (diapers) za watoto, brand ya Softcare. Yaani Zari alishampiga chini Diamond na bado anaendelea kukusanya mikwanja ndani ya Bongo. Wema yupo wapi? Kizizi?

Zari akiwa na Diamond alichungulia fursa. Shoo mbili za Zari All White Part Uganda na Mlimani City, Dar, zilimuingizia pesa kwenye mgongo wa Diamond, maana alikuwa msanii mwalikwa na alipafomu.

Zari amepata mikataba mingi ya matangazo akiwa na Diamond. Anzia Vodacom, GSM, Danube na kadhalika. Watoto wake pia wakawa mabalozi.

Wema akiwa na Diamond, lini walipata mkataba mmoja wa matangazo? Wote masupastaa. Tatizo lilikuwa nini? Kizizi? Mtindo wao wa kimapenzi ulisababisha. Drama nyingi na kuvujisha picha za faragha. Kampuni gani itavutiwa kutangaza na wacheza michezo ya blue?

Zari akiwa na Diamond, kwanza alimfanya Diamond kuwa mwanaume mwenye hadhi na katika mwonekano wa baba wa familia. Pamoja na watoto, wakawa familia bei mbaya na yenye kuvutia. Makampuni yalijipeleka yenyewe kutangaza na familia nzima.

Tukubaliane; Zari ana kizizi. Ni ile lifestyle yake. Kazi kwake Wema kukichimba hicho kizizi kimfae. Akiwa na lifestyle bora, itamfanya aongeze thamani. Pesa zitamfuata. Asipobadilika, ataendelea kumshuhudia Zari akitua Bongo na kufikia Hyatt Regency, The Kilimanjaro. Anachukua mapene yake na kusepa Afrika Kusini anakoishi au nyumbani kwao Uganda.

Ndimi Luqman MALOTO

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.