Rais John Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewaambia wafanyakazi nchini humo kwamba kwa sasa bado gharama za kuendesha shughuli za kila siku za serikali ni kubwa sana na hivyo waendelee kuvuta subira kupandishiwa mishahara yao, licha ya kwamba mwaka jana aliwaahidi kuwa angeliwapandishia.

“Gharama za kuendesha serikali bado kubwa kwa mfano kila mwezi tunatumia takribani bilioni 580 kulipa mishahara, na bahati nzuri siku hizi tunalipa mishahara kuanzia tarehe 19 swala ambalo lilikuwa halipo.” Aliwaambia maelfu ya wafanyakazi waliokuwa wamekusanyika kwenye maadhimisho ya Mei Mosi, akiendelea kwamba hata kiongozi wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi alimkumbusha kuhusu ahadi yake lakini “ninasema muda wangu bado nipo madarakani, ninachoomba muwe na subira.”

Vile vile, kiongozi huyo anayetimiza mwaka wa nne madarakani aliwahimiza wafanyakazi kuendelea kujituma kwa nguvu ili baadaye waje washuhudie matunda ya kazi yao, akitahadharisha kuwa kupandisha mishahara pekee kunaweza kupandisha gharama za huduma nyengine.

“Kuna usemi usemao kabla ya kuvuna ni lazima upande, ninaweza kutangaza kuongeza mshahara lakini kesho tu kila kitu kitapanda, mahindi yatapanda, mafuta yatapanda kwa hiyo ni lazima tuweke mazingira mazuri. Ahadi yangu bado ipo na kipindi changu hakijaisha.” Alinukuliwa akiwaambia wafanyakazi hao.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.