Upo msemo wa Kiswahili usemao “Ukitaka kumuua paka anza kwa kumpa jina baya”, ambao huelezea namna watu wanavyoharamisha au kuhalalisha jambo kwa kuanza na kukivunjia hadhi yake.

Wagonjwa wa maradhi ya moyo hasa watoto hapa Zanzibar nao hukutwa na kadhia hii. Baadhi ya watu kwenye jamii yetu huyatazama maradhi yenyewe  kama  laana au kuyafananisha na matokeo ya dhambi kutoka kwa wazazi wao au nguvu za kishirikisha. Ni unyanyapaa.  

Kwa muda mrefu jamii hii ya Kizanzibari imekosa uelewa juu ya kuyatazama maradhi ya moyo kama yalivyo maradhi mengine mengi yasiyoambukiza.

Tunaweza kusema maradhi haya ni mapya kwa jamii zetu hivyo upya wake ukawa ni sehemu ya huu unyanyapaa ambao baadhi ya wagonjwa wenyewe wameiambia Zanzibar Daima kuwa umekuwa ukiwaumiza na kufifisha juhudi za afya zao. 

“Nilizaliwa mwaka 1988 katika mtaa wa Chasasa, Mjini Wete, kisiwani Pemba. Wazazi wangu hawakuwa wakitambua kuwa mimi ni mgonjwa wa moyo hadi nilipofika umri wa miaka miwili baada ya majibu ya daktari nilipofikishwa hospitalini. Nikiwa na umri wa miaka 12 nilifanyiwa upasuaji mkubwa nchini Israel. Ila baada ya kurudi nyumbani nikakumbana na majina mengi mabaya dhidi yangu likiwemo jina la mgonjwa maghfira. Iliniuma sana. Kibaya zaidi ni kuona yule aliyeniita jina la Mgonjwa Maghfira akiwa mwalimu wangu skuli”, anasema Arafa Kombo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 33. 

Mgonjwa Maghfira ni msamiati wa dharau utumikao hasa kisiwani Pemba kumaanisha mtu aliye dhaifu sana kwa ugonjwa na aliye karibu kupoteza maisha.

Arafa ni mmoja tu miongoni mwa wengi wenye kukumbwa na kadhia hii ya unyanyapaa. Ndani ya jamii hali inatisha. Sababu mojawapo ni ukosefu wa elimu ya kuufahamu ugonjwa wa moyo, iwe kwenye kubaini viashiria vyake au hata miiko ya kukabiliana nayo.

Zipo familia zinazofarikiana kwa sababu tu mama kazaa mtoto mwenye maradhi ya moyo. Katika mkasa mmoja, Zanzibar Daima ilishuhudia familia moja ikikataa kumruhusu kijana wao wa kiume kumuoa binti mwenye maradhi ya moyo! Madai yao ni kuwa kumruhusu kijana wao kufunga ndoa na binti huyo kungeliendeleza kizazi cha watoto wenye maradhi ya moyo katika familia yao! 

Hata hivyo, madai haya yanapingana na uhalisia wa mambo. Na hapa Arafa Kombo anasimama kama ushuhuda dhidi ya wale wenye kupenda kuwatunukia majina mabaya paka ili wapate kuwauwa.

“Walikuwa wakiniambia mimi na kuwaambia hata wazazi wangu kuwa mimi siponi. Hii ni baada ya kugundua sasa kuwa nimesharudi nchini Israel na kufanyiwa upasuaji mkubwa wa matatizo yangu mwaka 2000. Nakumbuka walikuwa wanasema ‘binaadamu hapasuliwi, lipasuliwalo ni fenesi!’ Nashukuru Mungu, leo (tarehe 17 Februari 2019), madaktari wangu wale wale wa nchini Israel ambao wapo Zanzibar kwa sasa, wamenifanyia tena uchunguzi na kubaini kuwa sasa nimepona. Hii kwangu ni ‘suprise’ (mshangao) na jibu kwa waliokuwa wakinisema kwa ubaya juu ya kuumwa kwangu!”

Zanzibar Daima ilikutana na mama huyu wa watoto watatu muda mfupi baada ya kutoka kwenye chumba cha uchunguzi wa maradhi ya moyo katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.

Kwa muda mrefu sasa, kila mwaka madaktari kutoka Israel huweka kambi ya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa watoto wakishirikiana na madaktari wa Kizanzibari kwenye hospitali hiyo kuu ya serikali. 

Tanbihi: Makala hii imeandikwa na Abdulwahab Mohamed

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.