Ni fahari kubwa kwangu kushirikishwa katika  maadhimisho haya ya kumkumbuka Karimi Nduthu, mmojawapo miongoni mwa mashujaa wetu wa Kenya waliojitolea maisha yao ili kuendeleza harakati za mapambano ya kuleta mabadiliko ya kweli kwa sehemu kubwa ya Wakenya – hasa wale walioko katika matabaka ya chini.  Shujaa ambaye bado naendelea kumheshimu.

Ninavyoamini ni kwamba tumejumuika hivi leo ili kuadhimisha na kusherehekea maisha ya mzalendo huyu; wala si kuadhimisha kifo chake. Kwa sababu Karimi hakufa. Dhati yake bado inaendelea kuishi. Kama dhati yake ingekuwa imekufa, tusingekuwa tunaendelea kumtaja na kumkumbuka. Na kwa kuwakumbuka mashujaa wetu kama yeye huwa ndiyo tunaipa uhai historia yetu ya mapambano dhidi ya dhuluma za kila aina; na pia tunaendeleza mbele ule moyo wa kizalendo wa kujitolea nafsi zetu kwa ajili ya nchi yetu.

Nashukuru kwamba nilikuwa ni miongoni mwa Wakenya waliopata bahati ya kufanya kazi na mzalendo Karimi Nduthu wakati wa kile kipindi kigumu cha historia ya Kenya, ambapo nchi yetu ilikuwa imetandwa na giza la ukandamizaji uliokuwa ukifanywa na serikali dhalimu iliyokuwa ikiongozwa na Daniel arap Moi na KANU.

Nakumbuka kukutana naye Karimi kwa mara ya kwanza mwaka 1994, mjini Nairobi.

Na Abdulatif Abdalla

Mwaka huo wa 1994 ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kurudi nchini Kenya baada ya kulazimika kuishi uhamishoni (mwanzo Tanzania na baadaye Uingereza) kwa miaka 22 – baada ya kufunguliwa gerezani mwaka 1972. Mwaka 1994 Karimi alishakuwa Mratibu wa Kitaifa wa MWAKENYA. Mwaka huo nilifika Nairobi kutoka London nilikokuwa nikiishi, na ambako nilikuwa nikishirikiana na Wakenya wenzangu katika harakati dhidi ya serikali ya Moi-KANU. Nilikuwa nimetumwa na chama chetu hicho  cha MWAKENYA kuja kukutana na kushauriana na Karimi pamoja na mzalendo mwenzake, Tirop arap Kitur, kuhusu mipango ya mikakati ya kuendeleza harakati zetu ndani ya nchi. (Ni matumaini yangu kwamba Tirop naye yuko hapo ukumbini kwenye maadhimisho haya).

Kutokana na hali mbaya ya ukandamizaji iliyokuwako nchini wakati huo, ilibidi sisi watatu tukutane kwenye msitu wa Ngong ili tuweze kuzungumza bila ya kuhofia kwamba tunasikilizwa na serikali. Siku chache baadaye Karimi akanialika kwake, Riruta Satellite, alikokuwa anaishi. Lakini hapo nyumbani kwake hatukuzungumza jambo lolote la kisiasa. Baada ya hapo, tulikutana tena nje ya Kenya, pamoja na wanaharakati wenzetu kutoka ndani na nje ya Kenya, ili kufanya shughuli za MWAKENYA.

Kwa hivyo, nilifanya kazi naye Karimi kwa jumla ya miaka miwili tu, kabla ya kuuliwa. Lakini katika muda huo mfupi niliobahatika kufanya kazi naye, niligundua kwamba Karimi alikuwa na vitu vine, au sifa nne, ambazo ni muhimu sana kwa kila mwanaharakati wa kisiasa kuwa nazo:

Sifa ya kwanza ni kwamba Karimi alikuwa akiipenda nchi yake bila ya kiasi! Lau kama mtu angekifunua kifua chake, angeuona moyo wake umetandwa na umbo la Kenya.

Sifa ya pili aliyokuwa nayo ni kujitolea kwake mhanga ili kuitumikia nchi yake kwa moyo wake wote – bila ya kuchoka wala kunung’unika. Hakuna kazi ambayo aliiona kuwa ni nzito au ni ngumu, au ni chini ya hadhi yake kuitekeleza.

Sifa ya tatu aliyokuwa nayo ilikuwa ni unyenyekevu na kutopenda makuu. Kwa wale waliowahi kufanya naye kazi, watakubaliana nami nisemapo kwamba licha ya nyadhifa na vyeo alivyokuwa navyo katika shughuli mbalimbali za harakati,  Karimi hakuwa ni mtu wa majivuno na mbwembwe.

Sifa ya nne – ambayo ndiyo muhimu zaidi na ndio msingi mkuu wa harakati – ni imani thabiti aliyokuwa nayo kuhusu aliyokuwa akiyatenda. Hata mara moja  hakuteteleka (hakutetereka) au kuyumbayumba. Alikuwa ni mwamba madhubuti usioweza kutingishika! Na hakukata tamaa!

Huyo ndiye Karimi Nduthu, mwanaharakati, mzalendo na shujaa, ambaye serikali ya Moi-KANU ilitishika naye. Huyo ndiye Karimi Nduthu ambaye usiku wa tarehe 23 Machi, mwaka 1996, serikali hiyo dhalimu ilifikiri kwamba kwa kumuua itaifuta kumbukumbu yake. Lakini kumbukumbu za mashujaa hazifutiki! Kwa sababu kumbukumbu hizo huwa zimegubikwa ndani kabisa ya nyoyo za wale wanaoendelea kuishi, na ambao wanaijua thamani ya wazalendo wao; wale ambao wanapokezana kumbukumbu hizo kwa kizazi hadi kizazi; wale ambao kamwe hawausahau – wala kamwe hawatausahau – mchango wa mashujaa kama Karimi Nduthu, Dedan Kimaathi, Pio Gama Pinto, Bildad Kaggia, JM Kariuki, na wengineo wengi, katika kuifanya Kenya kuwa ni nchi ya usawa na uadilifu kwa kila Mkenya.

Ni matumaini yangu kwamba wanaharakati watajifunza na kuyapatia faida maisha ya Karimi Nduthu; na kwamba yatawahamasisha na kuwaongoza katika utendaji kazi wao. Hiyo ni miongoni mwa heshima kubwa tunayoweza kumpa Karimi Nduthu.

Nilitangulia kusema kwamba tumekusanyika hivi leo ili kuadhimisha na kusherehekea maisha ya mzalendo huyu; wala si kuadhimisha kifo chake. Kwa sababu dhati ya Karimi haikufa. Kwani shujaa aliyemo katika mapambano ya kupigania haki na kuleta mabadiliko katika jamii, ili jamii hiyo iweze kuishi maisha ya kibinadamu yaliyo huru na yenye heshima, huwa hafi!

Kama nilivyopata kusema mahali kwengine, kila pumzi moja ya shujaa inayomtoka wakati anapokuwa anakata roho, pumzi hiyo haipotei bure bali huingia katika nafsi za wale waliobakia, na kuwazidishia uhai na nguvu za kuiendeleza mbele kazi hiyo. Kila tone la damu linalomwagika kutoka katika mwili wa mwanaharakati kama huyo, damu hiyo huwa ni maji matukufu na yenye rutuba yanayouimarisha mti wa kupigania haki. Mti ambao una matawi mingi sana. Matawi ambayo hakuna mtu yoyote, au nguvu yoyote ya kilimwengu, inayoweza kuyakata na kuyamaliza. Wala mti huo haufi. Kama ungekuwa unakufa, ungekuwa umeshakufa kitambo sana katika nchi yetu hii baada ya wanaharakati na wapiganiaji haki wengi kuuliwa. Lakini mti huo bado unaendelea kuishi. Na utaendelea kukua.  Hautakufa!!

Katika  ukurasa wa 26 wa kitabu, Karimi Nduthu: A Life in the Struggle kumeandikwa kwamba Karimi alikuwa akipenda kusoma mashairi; na kwamba shairi mojawapo alilokuwa akilisoma mara kwa mara ni shairi langu liitwalo “Siwati”, lililomo katika kitabu changu cha mashairi niliyoyatunga nilipokuwa gerezani baina ya mwaka 1969 na 1972, kiitwacho Sauti ya Dhiki. Kwa hivyo, nataka niumalize ujumbe wangu huu kwa kumsomea Karimi shairi hilo, ikiwa ni njia ya kumhakikishia huko aliko kwamba vizazi na vizazi vya Wakenya havitaacha kuendelea na mapambano ya kujikomboa kutokana na mfumo dhalimu unaowakandamiza walio wengi:

Siwati nshishiyelo, siwati; kwani niwate
Siwati ni lilo hilo, ‘talishika kwa vyovyote
Siwati ni mimi nalo, hapano au popote
Hadi kaburini sote, mimi nalo tufukiwe

Siwati ngaadhibiwa, adhabu kila mifano
Siwati ningaambiwa, ‘tapawa kila kinono
Siwati lililo sawa, silibanduwi mkono
Hata ningaumwa meno, mkono siubanduwi!

Siwati si ushindani, mukasema nashindana
Siwati ifahamuni, sababuye waungwana
Siwati ndangu imani, niithaminiyo sana
Na kuiwata naona, itakuwa ni muhali

Siwati nimeradhiwa, kufikwa na kila mawi
Siwati ningaambiwa, niaminiyo hayawi
Siwati kisha nikawaa, kama nzi; hivyo siwi
Thamma nakariri siwi, na M’ngu nisaidiya

MAPAMBANO LAZIMA YAENDELEE!!

TANBIHI: Abdilatif Abdalla, mwanaharakati na mshairi wa Kenya anayeishi Hamburg, Ujerumani, aliandika kumbukumbu hii kwa ajili ya maadhimisho ya mwanaharakati mwenzake, shujaa Karimi Nduthu, yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Professional Centre jijini Nairobi, Kenya, tarehe 24 Machi 2018

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.