TONY Mwangi hakumchagua Raila Odinga anayewakilisha muungano wa National Super Alliance (NASA). Na wala hakumpendelea Uhuru Kenyatta wa Jubilee. Isitoshe hajachukia wala kujuta.

Mpigakura huyu katika uchaguzi mkuu wa Kenya, si kwamba amekosa tabasamu kwa uamuzi wa mahakama ya juu – Supreme Court of Kenya – kubatilisha uchaguzi wa rais wa taifa lenye uchumi mkubwa zaidi kwa kanda hii ya Afrika Mashariki.

Kwa hakika ni kinyume chake. Mwangi anaringa na kujivuna kwa hatua hiyo. Anafurahia kile anachokiita “tukio muhimu” la ustawishaji wa demokrasia na utawala wa sheria nchini kwake.

Hana wasiwasi kwa kuwa ana imani kubwa Kenya itampata rais katika muda uliopangwa ili aongoze jahazi la kusukuma mbele maendeleo yao.

Mahakama ya Juu ya Kenya imebatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 8 Agosti 2017 baada ya kuthibitisha malalamiko ya ukiukwaji mkubwa wa utaratibu yaliyowasilishwa na Odinga.

Odinga wa NASA aliyapinga matokeo tangu hatua ya kwanza yalipokuwa yakitangazwa hatua kwa hatua kupitia kituo cha kurushia matangazo ya matokeo kilichokuwa ukumbi wa Bomas, jijini Nairobi.

Taarifa yake ya awali ilisema kuwa matokeo yaliyokuwa yakitangazwa yalikuwa tofauti na yale yaliyokuwa yamerikodiwa kwenye fomu ya matokeo iliyosainiwa na watendaji wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC).

Upinzani wa matokeo aliouonesha Odinga uliendana na madai kuwa mfumo wa kuhakiki na kurusha matokeo uliingiliwa. Zikaja sauti kutoka kwa watu mbalimbali hasa makundi ya watazamaji wa uchaguzi kumtaka asubiri matokeo ya mwisho ndipo atangaze msimamo wake.

Matokeo yakatangazwa. Uhuru aliyegombea akitaka kuongoza kwa muhula wa pili mfululizo, baada ya kushinda awali mwaka 2013, akatangazwa ameshinda tena.

Tume, sasa ikiwa imekana madai ya upinzani kuwa mfumo wake wa kiteknolojia wa kuhifadhi matokeo uliingiliwa katikati, ilisema Uhuru alishinda urais kwa tofauti ya zaidi ya kura milioni mbili.

Ni hapo watazamaji wakainua sauti kwa msisitizo kumtaka Odinga na NASA yake kutochochea vurugu, badala yake, apeleke malalamiko yake mahakamani.

Shinikizo kwa Odinga lilikuwa na mantiki. Katiba ya Kenya na Sheria ya Uchaguzi vinaruhusu mgombea urais ambaye ametangazwa kushindwa kura, kufungua shauri mahakamani.

Kwa lugha nyingine, Katiba ya Kenya inatoa haki ya matokeo ya uchaguzi wa rais kuhojiwa. Hoja za kuyapinga matokeo zinawasilishwa kwenye mahakama ya juu inayoundwa na jopo la majaji saba.

Odinga kwa kuamini hajatendewa haki katika hatua ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza mpinzani wake, Uhuru Kenyatta, kuwa ndo mshindi, ametumia fursa ya kikatiba na haki yake kufungua shauri.

Katiba inatoa fursa na kupanga muda wa kuitumia fursa hiyo. Odinga akatimiza masharti ya kuhoji utaratibu wa kupatikana kwa mshindi.

Tume ikasikiliza kwa kupokea vielelezo vilivyoendana na malalamiko ya Odinga; na yenyewe ikiwa na muda maalum wa kisheria kufanya uamuzi wa malalamiko iliyoyapokea.

Ijumaa ya tarehe 1 Septemba 2017 ikawa siku ya Mahakama ya Juu chini ya rais wake David Maraga, kutoa uamuzi wa malalamiko ya Odinga.

Uamuzi ukathibitisha madai ya kukiukwa kwa utaratibu wa kisheria wa kuendesha uchaguzi. Majaji watano wakaridhika uchaguzi ulikuwa huru lakini haukuwa wa haki.

Vipi sasa kuhusu fidia ya ukiukwaji huo wa utaratibu wa kuendesha uchaguzi ulio huru, wa haki na kwa njia ya uwazi? Mahakama imeamua uchaguzi mpya ufanyike ndani ya siku 60 kutoka siku imetoka uamuzi wake.

Malalamiko yalitolewa ya kupinga matokeo. Walioona wameonewa wakatumia fursa ya kikatiba kudai haki itendeke. Upande wa Odinga umeridhika haki imetendeka.

Uhuru na kundi lake hawakuridhika na uamuzi wa Mahakama ya Juu na huku wakimuita Jaji Maraga na wenzake kuwa ni wakora au wezi, wameheshimu uamuzi japo hawauamini.

Mpigakura Mwangi anajivunia hatua hii. Inaendelea kuthibitisha kuwa nchi yake inazidi kuwa mfano wa baba wa demokrasia katika Bara la Afrika.

Mafanikio haya niliyaeleza bayana katika makala yangu wiki mbili zilizopita. Nikasema Kenya imepiga hatua nyingi mbele katika dhana ya demokrasia na utawala wa sheria. Nikasema na bado ninamaanisha, Tanzania na Zanzibar zinalo funzo kwa Kenya.

Ndipo ilipo tofauti ya hisia kati ya Mwangi wa Kenya na Mtanzania awe Mtanganyika au Mzanzibari. Mtanzania hana utulivu wala furaha kama alivyo Mwangi wa Kenya.

Tume ya Uchaguzi sio tu hazikuridhisha wagombea na wananchi kwa ujumla, bali kwa hakika zimeacha vinyongo ndani ya nyoyo za watu. Malalamiko yalikuwepo yalipuuzwa.

Mgombea urais upande wa Jamhuri ya Muungano kutoka upinzani uliounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa mpaka leo anaamini alishinda.

Kwa Zanzibar, hali ndio mbaya zaidi kwa sababu hivi ninavyojadili hapa, wananchi wanaamini mgombea wao kipenzi, Maalim Seif Shariff Hamad angetangazwa mshindi.

Watu wanasema wazi walisubiri Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) itangaze matokeo ya uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 kwa kuwa ndio kisheria uliostahili kuwapatia kiongozi wao.

Wanaamini Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na marekebisho yake makubwa ya 2010, haitambui kilichoitwa “uchaguzi wa marudio” ambao Tume iliutumia kumtangaza Dk. Ali Mohamed Shein kuwa rais.

Katiba hiyo haisemi popote kuwa tume au ofisa wake yeyote, kwa jina lolote lile, anaweza kufuta uchaguzi uliokwishafanyika. Hayapo mamlaka ya kumwezesha hata mwenyekiti wake kufanya hivyo.

Wazanzibari walipigakura kwa amani. Kura zikahisabiwa kwa amani. Matokeo ya viti vya uwakilishi na udiwani yalihisabiwa sambamba na yale ya urais. Washindi wa uwakilishi na udiwani walitangazwa na kukabidhiwa hati za ushindi.

Kura za urais zilihisabiwa kwa mfumo huohuo. Kazi ya kuzihakiki ilifanywa vizuri ndio maana matokeo yalianza kutangazwa kwenye kituo cha kurushia matokeo kilichowekwa ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani.

Ni nini kilichosababisha Mwenyekiti wa Tume, Jecha Salim Jecha kutangaza kuyafuta matokeo ya uchaguzi wote? Jecha katika tangazo lake la tarehe 28 Oktoba 2015 alifuta hata uchaguzi wa uwakilishi na udiwani ambao washindi walishakabidhiwa hati za ushindi.

Alifanya hivyo akijua fika hana mamlaka ya kisheria ya kufanya hivyo. Alijua na mpaka sasa anajua hana utetezi wowote wenye nguvu ya kisheria wa kumvua na kosa la kuhatarisha usalama wa nchi ikitokea ameshitakiwa mahakamani.

Ni kwa sababu alijua kwa kuwa watakaonufaika na hujuma yake ndio walioshika serikali, hataguswa na mkono wa sheria. Lakini ninaamini hajaukwepa mkono wa sheria. Unachelewa tu kumfikia.

Jecha alijua hakuna mahakama inayoweza kusikiliza malalamiko ya swahiba zake Chama Cha Mapinduzi (CCM) iwapo angewatangaza kuwa washindwa katika uchaguzi.

Kwa upande mwingine, alijua pia hakuna mahakama itakayofanya kazi ya kusikiliza malalamiko ya Chama cha Wananchi (CUF) katika kunyimwa haki yao ya ushindi katika uchaguzi huo.

Na hiyo ndiyo kasoro ya waziwazi na kikwazo cha kuisogeza Zanzibar kwenye demokrasia ya kweli, utawala wa sheria na utengamano wa kijamii kupitia uchaguzi mkuu ulio huru, wa haki na uliofanywa katika mifumo iliyo wazi.

Upinzani kupitia CUF na mwamvuli wa Ukawa upo tayari kama walivyo tayari wananchi wa Unguja na Pemba.

Shida kubwa iliyopo ni ukorofi wa viongozi wa CCM kwa kudhani wamehulukiwa haki ya kuiongoza serikali milele.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Jabir Idrissa na ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHALISI la tarehe 11 Septemba 2017.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.