Skip to content

Nguzo ya 8 ya mitaji ya mafanikio ni mahusiano mema

Pamoja na kufahamu mambo kadhaa ya kufanya peke yangu bila msaada, bado kilichoniwezesha kuandika na kutoa makala haya ni mahusiano mema. Tumezaliwa kutokana na mahusiano, tena mazuri sana, baina ya mama na baba. Tumelelewa katika mahusiano, tumesoma kupitia mahusiano na mawasiliano, na tunafanya kazi mbalimbali kutokana na mahusiano na watu wengine waliotuunganisha. Kila mmoja anaye mtu na/au watu waliomfanya awe mahali alipo na kazi anayofanya. Bila hao tusingekuwa hapo tulipo leo.

Hakuna awezaye kufanikiwa katika jambo lolote pasipo kuhusika au kuhusisha watu wengine. Hata biashara unayofanya inastawi kutokana na mahusiano yako mazuri na wafanyabiashara wengine pamoja na wateja wako. Na kwa kubaini hilo, hakuna mtu anapinga kuwa mahusiano mema ni mojawapo ya nguzo za mitaji ya kutufanikisha katika maisha yetu.

Umuhimu wa mahusiano mema kijamii

Mahusiano mema si kufanya kazi pamoja, kuishi pamoja, kuzaliwa pamoja, kusoma shule pamoja, kuwa na imani ya kidini moja, asili moja, kabila moja, rangi moja, kuoana au kuungana pamoja; la hasha. Mahusiano mema ni kumjali mwingine na kumpa nafasi sawa yenye kuleta faida na usawa kwa watu wawili au pande mbili zinazohusiana. Mnaweza mkaishi pamoja, mkasoma shule moja na kulala kitanda kimoja; lakini msiwe na mahusiano mema hata kama ni mapacha. Kila mtu akawa kivyake!

Aidha, mahusiano mema si lazima kuwa na urafiki. Mtu anaweza asiwe rafiki yako lakini pia asiwe adui yako kutokana na kuwepo uhusiano mzuri. Siku hizi tunasema tumeendelea sana na kustaarabika, na wengine kukiri kuwa dunia imekuwa kama kijiji kutokana na maendeleo ya kiteknolojia. Lakini kila mtu anazidi kuishi kibinafsi kivyake, mahusiano yanafifia au kutokweka kabisa. Na wengine wamekuwa wapweke katikati ya umati wa watu kwa kuwa tu hawana mahusiano mema na wengine.

Tumejenga maghorofa makubwa na marefu yakiwa na vyumba vingi vya kuishi pamoja kwa ukaribu, lakini kwa sehemu kubwa kila mtu yuko kivyake kwa kukosa mawasiliano na/au mahusiano na wengine. Hatuko karibu kama kijiji. Mara kadhaa imetokea mtu anakufa peke yake chumbani – mpweke! Watu wa vyumba jirani hawajuani wala hawasalimiani. Tukiri kuwa teknolojia bado haijaweza kutuleta pamoja.

Ukipanda basi, kila abiria yuko na simu yake. Ukirudi nyumbani kila mwanafamilia yuko simu yake. Ukienda mkutanoni kila mtu yuko na simu yake, anaparaza anayoyajua yeye. Wengine hudai simu zimetutenganisha na kutufarakanisha, hakuna mahusiano. Kama tungekuwa tunahusiana vema sisi kwa sisi kwa ukaribu kama tulivyo karibu na simu zetu, naamini magomvi, mitafaruku na hata vita visingekuwepo duniani.

Unyonyaji unaoendelea duniani, unatokana na uchumi kuwa mikononi mwa watu wachache wanaomiliki na kujirundikia utajiri wasiokuwa na haja nao, wakati wengine wanakufa kwa ufukara wa kutisha. Yote haya ni kutokana na kutokuwa na mahusiano mema ya kiuchumi. Tutambue kuwa bila rasilimali asilia za nchi zinazoitwa maskini, leo hii hatuwezi kuwa na nchi tajiri ambazo hutegemea sana rasilimali hizo. Lakini hakuna urari wowote na/au mahusiano mema.

Tukitambua umuhimu wa kila mtu au kila taifa kuhusiana vema pasipo unyonyaji, unyonywaji, ubaguzi, uonevu na ukandamizaji; hatutakuwa na matabaka ya watu au pengo kubwa kiuchumi baina ya watu wenye mali nyingi na wenye ufukara mwingi duniani. Kila mtu anamhitaji mtu mwingine ili aendelee na kustawi na kila taifa linalihitaji taifa lingine ili liendelee na kustawi.

Kila mtu ana thamani katika nafasi yake kwa kiwango chake cha kutumikia wengine na wengine kumtumikia yeye. Tungekuwa tunaelewa umuhimu na mchango wa kila mtu katika jamii na taifa, mahusiano yafuatayo kimaisha yangekuwa dhahiri:

  • Mwenye nyumba asingemwonea mfanyakazi wake wa ndani.
  • Mwenye gari asingemdharau mwenye mkokoteni au mbeba mizigo.
  • Mwenye kazi za ofisini asingemkebehi mkulima.
  • Mwenye elimu asingemdharau mjinga.
  • Mwenye shibe asingemhukumu mwenye njaa.
  • Mwenye afya njema asingemcheka mwenye udhaifu – mgonjwa.
  • Mwenye utajiri asingemdhihaki mwenye umaskini.
  • Mwenye uwezo wa kuajiri asingemnyanyasa mwajiriwa.
  • Mwenye umaarufu asingemdharau mtu wa kawaida (commoner).
  • Mtawala asingemkandamiza mtawaliwa.

Kiongozi angemjali sana anayemwongoza kwa kuwa kiongozi bora pia huongozwa na anaowaongoza. Vivyo hivyo, mataifa nayo endapo yangekuwa yanahusiana vizuri pasipo kunyonyana:

  • Tusingekuwa na nchi za kinyonyaji na za kinyonywaji.
  • Tusingekuwa na dunia ya kwanza, ya pili wala ya tatu.
  • Tusingekuwa na nchi tajiri wala maskini.
  • Tusingekuwa na nchi zinazokopesha na zinazokopeshwa.
  • Tusingekuwa na nchi kubwa wala ndogo kiuchumi.

Tusingekuwa na matabaka ya watu na ubaguzi wa rangi.

Tungejua vema nafasi na mchango wa kila nchi katika ustawi wa dunia yetu, basi tungekuwa na nchi zinazosifika kwa viwanda na nchi zinazothaminiwa na kuheshimika kwa kuzalisha malighafi za viwandani. Hata watumwa waliopelekwa Amerika, Asia na Ulaya kutoka Afrika hadi sasa wangekuwa wanaheshimika na kukumbukwa kwa jinsi walivyojenga miundombinu ya reli na majengo makubwa, na walivyolima mashamba makubwa ya miwa kwa ajili ya kuzalisha sukari. Waafrika na Afrika yetu tungekumbukwa tulivyotoa rasilimali watu na rasilimali vitu kuendeleza mataifa hayo.

Mtu mweusi toka Afrika kamwe asingedhalilishwa na kubaguliwa kwa rangi yake, bali angepewa heshima ya mchango wake na utu wake duniani. Na kwa kusema hivyo, lazima Afrika ijue kuwa bila sisi Waafrika, wazungu na wengineo hawawezi kuendelea pasipo sisi. Tukigoma kuruhusu rasilimali zetu kuvunwa, nchi nyingi za Asia, Ulaya na Marekani zitakwama! Sehemu kubwa ya maendeleo ya Ulaya, Marekani na Asia hutegemea utajiri wa Afrika na nguvukazi ya Waafrika.

Tungeelewa vema na kuthamini umuhimu na mchango wa kila nchi duniani tusingekuwa na nchi zinazojidai kwamba zinajitegemea na nchi zinadaiwa kuwa ni tegemezi. Bali tungekuwa na nchi zinazotambua kutegemeana. Hakuna nchi kubwa au inayojidai kuwa ni tajiri na iliyoendelea bila kutegemea au kushirikiana na nchi zingine zinazodaiwa kuwa ni ndogo na maskini. Tungetambua kuwa mahusiano mema ndio ukweli na uhalisia wa maisha yenye staha, basi tungeelewa kuwa kila nchi, ndogo au kubwa, tajiri au maskini, ina vitu vya kuisaidia nchi nyingine. Bila nchi maskini haiwezi kuwepo nchi tajiri na ndivyo ilivyo kinyume chake.

Na kwahiyo, hakuna nchi ndogo au kubwa kuzidi nyingine, wala hakuna nchi maskini au tajiri kuliko nchi nyingine, bali kila nchi inaihitaji nchi nyingine ili iweze kuendelea. Kama ni utajiri, kila nchi ina utajiri wake, kama ni umaskini kila nchi ina umaskini wake, yaani kile kitu ambacho nchi inakikosa hukipata kutoka nchi zingine. Tunategemeana kwasababu tunatofautiana katika kumiliki rasilimali vitu, rasilimali watu, mazingira, utamaduni, maarifa na teknolojia. Ufahamu huu ndio njia pekee ya kuundoa unyonyaji, ukandamizaji, uonevu na ubaguzi mkubwa ulioshamiri na unaozidi kushamiri duniani.

Migogoro mingi na vita vingi duniani kwa sehemu kubwa havitokani na tofauti zetu za imani za kidini bali hutokana na tofauti zetu kiuchumi, huku kila mmoja akishindana kumnyonya, kumpora na kumzidi mwingine. Kuna watu wachache au nchi chache sana duniani hufaidi rasilimali za dunia kwa mgongo wa watu wengine au nchi nyingine zinazotumika au kutumikishwa kuinua nchi hizo. Ushindani kiuchumi umegeuka kuwa uporaji na kuendeleza umaskini duniani.

Kwa kudhihirsha hoja zangu, mataifa mengi yanayodai yameungana, yamegundua kuwa yananyonyana na kutawalana tu. Mathalani, Uingereza ilijitoa umoja wa Ulaya ikidai haina uhuru wa kuamua mambo yake, eti inanyonywa na kupangiwa kila kitu na watu wa Umoja wa Ulaya walioko Brussels (Ubelgiji). Mwaka jana Waingereza walijitoa kwa kampeni kali iliyoitwa Brexit. Kumbe nchi za Ulaya nazo zimeungana lakini hazina mahusiano mema. Afrika tunao Umoja wetu (AU) lakini hatuko pamoja, hatuna mahusiano mema, kila nchi iko kivyake na utawala wake.

Tanganyika na Zanzibar ziliungana Aprili 26, 1964; lakini kiuhalisia waliungana na hadi sasa wameungana watawala. Muungano haukutokana na ridhaa ya wananchi. Watu wa pande hizi mbili kwa sehemu tunajiona hatuna mahusiano mema na yenye usawa. Wazanzibar wanalalamika miaka nenda rudi, na sasa miaka 53, kuwa wanapunjwa, wanakandamizwa, hawana fursa kitaifa na kimataifa kwasababu ya muungano uliopo.

Kuna watu hubaguliwa kama wabara na wengine wapemba. Mbaya zaidi hata ndani ya Zanzibar yenyewe, kuna watu wanaona mchotara si Wazanzibar, eti Zanzibar ni ya weusi. Bila soni huinua mabango mchana kweupe ya kuwatenga machotara. Ni kisiwa kimoja bila mahusiano mema. Vyama vya siasa navyo vinatufanya tubaguane na hata kuhasimiana vibaya.

Kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar kuwe kwa misingi ya mahusiano mema na udugu. Kuwa karibu au jirani si hoja. Leo tuna mahusiano mema na Kuba (Cuba) lakini iko magharibi ya mbali kabisa na Tanzania. Japani iko mashariki ya mbali sana na Tanzania lakini tuna mahusiano mema na ya karibu. Mnaweza mkawa majirani lakini mkawa mbali kabisa kimahusiano na kuwa na utengano badala ya utengamano. La sivyo tusingepigana na Idd Amini Dada maana Uganda ni jirani.

Naamini endapo kweli tunawapenda Wazanzibar hatuwezi kuwazuia kupata mamlaka, hadhi, haki na fursa yao kitaifa na kimataifa kwa kuwa ni ndugu zetu wa asili, wa damu, na zaidi sana ni Waafrika wenzetu. Napenda Zanzibar ipate hadhi ya kidola na kitaifa, na hakika itakuwa faida kwetu sote – Tanganyika na Zanzibar.

Korea ilikuwa nchi moja, watu wa asili moja, rangi moja na lugha moja, lakini waliingia katika mahusiano mabaya na kusababisha vita mbaya kabisa hadi kutengana Kaskazini na Kusini kwa misingi ya tofauti za itikadi za kisiasa. Hadi leo kuna uhasama mkubwa mno huku majeshi ya pande mbili yakiwa mpakani toka mwaka 1953 tayari kwa kushambuliana wakati wowote. Ndugu wa damu na familia moja walitenganishwa na hakuna kuonana hadi kwa ruhusa maalum ambayo haitokei kwa kipindi kirefu. Hata ikitokea wanaonana kwa muda mfupi na kuachanishwa.

Vivyo hivyo, Somalia sehemu kubwa wana imani moja ya kidini, kabila moja, lugha moja, asili na rangi ya aina moja. Lakini wanatwangana kila siku kwa misingi ya tofauti za kiukoo. Hata wangekuwa ukoo mmoja nchi nzima, pasipo mahusiano mema bado wangetwangana. Hakika mahusiano mabaya na yasiyo na urari ni kiini cha migogoro mingi duniani.

Hitimisho

Ili kuwa na mahusiano mema tunapaswa kuziishi sifa zifuatazo: kuwaza mema, kutolaumu sana, kutosengenya, kuwakubali wanaofanya mema na kutowahukumu sana wanapokosea, kuwa wasikivu kabla ya kusema lolote, na kupenda kusaidiana na kufaidiana kwa usawa. Maisha ni mazuri ikiwa hatuchoki kutenda wema, kuhurumiana, kuheshimiana na kujaliana. Ulimwengu huu utakuwa mahali pazuri pa kuishi endapo tutakazana kuwatendea wengine mema kama ambavyo nasi tungependa kutendewa mema. Na hakuna asiyependa kutendewa mema – hakuna, hata dhalimu!

Mahusiano mema hutufundisha kuhusu sisi wenyewe. Kama unamwangalia mtu na kuhisi au kugundua mambo ambayo hayafai kwake, unakuwa umejigundua wewe mwenyewe kwa kuwa tunafanana. Ni sawa na kujiangalia kwenye kioo, unayemwona ni wewe mwenyewe. Makosa tunayoyaona kwa wengine ndiyo tuliyonayo, na mazuri tunayoyaona kwa wengine ndio tupasayo kufanya. Tusimhukumu sana mtu akikosea bali iwe nafasi ya kujiona tulivyo. Na kwahiyo tutatangulia kwanza kujisahihisha wenyewe ndipo tuwasahihishe wengine kwa ustaarabu kwa kuwa ndivyo tulivyo sote.

Mtu anayepigana vita nzuri ni yule anayejishinda mwenyewe kwanza, si anayemshinda mwingine. Ni yule anayeshinda chuki ndani yake, wivu mbaya ndani yake, mawazo mabaya ndani yake, kiburi ndani yake na udhalimu ndani yake. Ndiposa tutaweza kuwasaidia wengine baada ya kujisaidia sisi wenyewe kwanza.

Nihitimishe kusema kuwa kwa usalama wako, waheshimu watu wote ili uwe na mahusiano mema nao, lakini waamini wachache (respect all, trust few).

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Gwandumi Gwappo A. Mwakatobe, mchambuzi  huru wa masuala ya kitaifa na kimataifa, anayeishi Mwakaleli, Busokelo, Rungwe, Mbeya. Anapatikana kwa anuani ya baruapepe: gwandumi@hotmail.com au gwappomwakatobe@gmail.com

Leave a Reply