UCHAGUZI  mkuu uliomalizika nchini Kenya umetuachia mengi ya kuyaangalia na kujifunza. Nitajaribu kufananisha machache ambayo yanatuachia mengi ya kujiuliza kwa nini sisi Tanzania yatushinde?
 
Mara baada ya Rais Kenyatta kutangazwa kuwa ndiye mshindi wa kiti cha urais alisema bila masimango ya aina yoyote kwamba iliyoshinda ni Kenya wala siyo yeye. Wakati Tanzania ilisemwa kwamba iliyeshinda ni Magufuli  na siyo mtu mwingine yeyote.
 
Vile vile Rais Kenyetta alisema kwamba wapinzani, hasa Mheshimiwa Raila Odinga, anawahitaji sana kufanya nao kazi ya kuijenga nchi yao kwa vile hata kama wao ndio wangeshinda bado kazi ilikuwa ni ileile ya kuijenga Kenya.
 
Lakini hapa kwetu, mara baada ya ushindi wa Magufuli,  wapinzani walichukuliwa kama watu wa kuja ambao rais aliyeshinda alisema hawahitaji katika shughuli zake!
 
Wakati kule Kenya rais mteule akiweka wazi kwamba shughuli za kisiasa, hata kama ni maandamano ya amani ya kumpinga yeye, ni ruksa na askari wanapaswa wayalinde kwa vile yapo kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, hapa kwetu vitu hivyo ni haramu kabisa pamoja na ukweli kwamba vinahalalishwa na Katiba ya nchi yetu!
 
Lakini kwa leo ninachotaka kukiangalia zaidi ni upendeleo kwa kina mama. Kufuatia jinsi tulivyoona kina mama wa kule Kenya wakijitokeza kupambana katika kuwania nafasi mbalimbali,  udiwani, ubunge, useneta na hata ugavana, bila kutegemea nafasi za upendeleo, nimeona kuna haja ya kuliangalia zaidi jambo hilo.
 
Nimesukumwa zaidi kuliangalia hilo na ujumbe wa maandishi niliotumiwa na James Kiemi wa Isamilo, Mwanza. Ujumbe huo unasomeka hivi:
 
“Huenda nitawaudhi baadhi ya wananchi, hasa kina mama, lakini naomba niwahakikishie kuwa nawaheshimu na kuwapenda sawia. Napendekeza nafasi za viti maalumu  ziwe maalumu kwa maana halisi ya neno maalumu. Hiyo ni kwa walemavu, wajane lakini wenye sifa ya kuelewa mambo”.
 
“Waliogombea wakashindwa lakini wakiwa na sifa za kipekee kitaifa nakadhalika. Na muda wa viti hivyo maalumu usizidi vipindi viwili kwa vile waliopata nafasi hizo kwa muda huo watakuwa wamepata uzoefu wa kutosha wa kugombea ili wakawapishe wengine nao wakanufaike”.
 
Kiemi anaongeza kwamba “Kwa mtazamo wangu tuepukane na utamaduni wa kuwaona wanawake ni vyombo, badala yake tuwaone ni watu wenye uwezo ili wakajijenge katika kujiamini wenyewe kuliko kutegemea tu fadhila, ili  waanze kuthamini zaidi vichwa vyao”.
 
Nianze kujadili hoja hiyo kwa kukumbusha kwamba kidunia ulitengenezwa mkakati shawishi wa uwakilishi wa kinamama kufikia walau asilimia 30. Lakini mkakati huo ulisuasua nchini Kenya na baadaye kugota kwenye asilimia 8.1.
 
Ila kwa sasa Bunge la Kenya linatoa asilimia 12 za viti maalumu vya kinamama na asilimia 20 kwenye seneti. Ila kule kinachotiliwa maanani ni nafasi maalumu kwa maana halisi, vijana, walemavu, wafanyakazi na makundi mengine maalumu.
 
Katika makundi hayo ni lazima jinsia izingatiwe kusudi nafasi hizo maalumu zisiende kwa jinsia moja.
 
Kwahiyo tutaona kwamba Kenya, pamoja na kulishughulikia suala la nafasi maalumu, walau wanao utaratibu muafaka unaozifanya nafasi hizo zionekane kwa nini ziitwe maalumu. Kwa upande wangu nakataa suala la umaalumu kuwaendea wanawake kana kwamba umama unamaanisha ulemavu.
 
Jambo hilo kulichukulia namna hiyo sio haki hata kidogo kwa jinsia ya kike. Na kwa mantiki hiyo naona kama nafasi hizo zitakuwa zinawadhalilisha wanawake.
 
Hata hoja ya Kiemi ya kwamba wanawake wajane wanafaa wapewe nafasi maalumu sikubaliani nayo. Sababu ujane sioni unapunguza nini katika uwezo wa mwanamke kutafakari na kuamua mambo.
 
Nitoe mfano, Profesa Anna Tibaijuka ni mjane, lakini ni wanaume wangapi wanaoweza kusema wanaufikia uwezo alionao mjane huyo kiakili? Je, naye anasitahili kupewa nafasi maalumu? Mbona kapambana na wanaume na kuwabwaga, kidunia, kimataifa, kitaifa na hata kijimbo na sasa ni mbunge wa kuchaguliwa Muleba Kusini?
 
Kwa nini Tibaijuka asiwe mfano tosha kwa wanawake wengine? Kwa nini tusimtumie mtu kama huyo kuwaamsha wanawake ili waweze kufanya mambo kwa kujiamini bila kusubiri fadhila ambazo ni kama zinaididimiza jinsia yao?
 
Wapo watu waliochangia hoja hiyo kwa njia za ujumbe mfupi wa maandishi wakisema kwamba wanawake wanaotegemea nafasi za viti maalumu kuingia Bungeni, hasa kwa upande wa chama tawala, kazi yao ni kuuponda tu upinzani huku wakipitisha kila jambo linaloletwa na serikali Bungeni kwa kusema….ndiyoo….ipiteee…bila ufafanuzi wa hoja zenye mantiki.
 
Eti wanafanya hivyo kama mtaji kusudi ukija uchaguzi mwingine warudishwe kwenye nafasi hizo hata kama watakuwa hawana faida yoyote kwa nchi na wananchi. Uwepo wao Bungeni unakuwa mzigo tu kwa walipakodi.
 
Kusema ukweli sioni kama fikra za aina hiyo zinaitendea haki jinsia ya kike. Jambo la kuondoa fikra za aina hiyo dhidi ya jinsia ya kike ni kuondoa kabisa kinachoitwa nafasi maalumu kwa wanawake, ni bora tukaiacha jinsia hiyo ijitegemee kwa kujiamini ili ikajijengee heshima isiyoyumbishwa na yeyote.
 
Nafasi maalumu, kama nilivyoonesha hapo juu, zingeachwa zibaki kwa watu walio na mahitaji maalumu, sanasana walemavu. Kumweka mwanamke kundi moja na mlemavu sio kumtendea haki hata kidogo, uko ni kuidhalilisha jinsia ya kike.
 
Mikakati ya kinamama, ambayo pia na mimi naiunga mkono, ni ya kutaka usawa wa kijinsia. Sasa inawezekanaje katika usawa ukawepo upendeleo? Neno upendeleo au nafasi maalumu, vinatakiwa vipigwe vita na jinsia zote mbili katika kuuweka usawa mahala pake.
TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Prudence Karugendo, anapatikana kwa anwani ya barua-pepe prudencekarugendo@yahoo.com na simu nambari +255 784 989 512

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.