“Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa…” (Hosea 4:6), ndivyo Mungu anavyosikitika na kutoa sababu ya watu wetu kuangamizwa kuwa ni ukosefu wa maarifa. Tunalalamika kuwa tu maskini, lakini hapohapo tena tunajidai kuwa tuna utajiri wa rasilimali asilia nyingi na za kututosha. Umaskini unatoka wapi kama tuna utajiri huo wa rasilimali asilia lukuki?

Rasilimali asilia zikibaki zilivyo katika uasili wake, pasipo kuchakatwa, kuchenjuliwa, kusindikwa na kuboreshwa; haziwezi kutuletea mapato, faida na/au mafanikio. Lazima tupate maarifa na elimu (si wawekezaji uchwara) ya kuchakata, kuchenjua na kusindika rasilimali zetu ili kuziongezea thamani na kuziuza kwa faida katika masoko ya  kitaifa na kimatiafa.

Zanzibar ina utajiri mkubwa wa mwani, na ni mojawapo ya maeneo machache yanayozalisha mwani kwa wingi duniani. Lakini Wazanzibari wengi bado maskini. Tatizo liko wap? Tatizo ni kukosa maarifa, elimu na vifaa (teknolojia) stahiki ya kuuchakata, kuusindika, kuuboresha na kuuongezea thamani mwani kwa kuzalisha bidhaa zake mbalimbali kama wafanyavo wenzetu Singapore na Ufilipino. Tunahitaji maarifa ili tusizidi kuangamizwa na ufukara katikati ya utajiri wa mwani na rasilimali zingine.

Umuhimu wa Maarifa na Elimu kwa Maendeleo ya Watu

Maarifa ni ujuzi, umahiri, ufundi, ustadi au uhodari katika fani au nyanja fulani, ambayo kwa sehemu kubwa hutokana na kipaji alichonacho mtu na kukiboresha kwa elimu au utaalamu wa ziada katika fani husika. Maarifa na elimu ni msasa wa vipaji, na ni muhimu zaidi kuliko hata rasilimali asilia nilizozijadili makala ya nyuma. Kosa kila kitu, lakini si maarifa na elimu!

Leo hii nchi nyingi duniani hazina madini, misitu, wanyama, mafuta wala ardhi nzuri kwa kilimo; ila zina maarifa na elimu inayoziletea utajiri mkubwa. Mathalani Ulaya, nchi za Japan, Singapore, Korea Kusini, nk.; hazina neema ya rasilimali asilia kama tulizojaaliwa Afrika, hususan kusini mwa jangwa la Sahara, lakini matajiri. Watu wake wanafaidi rasilimali zetu kuliko sisi wenye nazo. Wanatuzidi nini sasa? Maarifa na elimu!

Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike, maana yeye ni uzima wako. Ndivyo tunavyoisoma hekima ya Mungu katika misahafu (Mithali 4:13). Kinara wa ukombozi wa utu wa mtu, hususan kwa Waafrika, Nelson Mandela, aliwahi kusema, ninanukuu: “Elimu ni silaha yenye nguvu sana ambayo unaweza kuitumia kuleta mabadiliko ulimwenguni.”

Neno elimu tumelitafsiri kutokana na neno la Kiingereza la “Education.” Education hutokana na neno la Kilatini la “Educare.” Educare means to draw out or to impart and fill. Yaani kwa tafsiri rahisi, “Educare” ni kuwa mpana zaidi/kutanuka au kuweka na kujaza. Tunapoelimishwa tunapewa uelewa mpana au kuwekewa na kujaziwa maarifa yanayotupa ufahamu, ustadi na ujuzi katika vichwa vyetu. Elimu si tu kujua kusoma na kuandika, la hasha; bali ni kuwa na maarifa, ujuzi, umahiri ua uhodari katika kukabiliana na changamoto za mazingira yetu na maisha yetu.

Elimu ni maarifa anayopata au anayokuwa nayo mtu ili aweze kuishi kwa kupambana au kuyamudu mazingira yaliyopo kupitia kipaji au utaalamu wake. Aidha, elimu huchonga, hupalilia, huchochea, huimarisha na huboresha kipaji cha mtu – inamfanya mtu awe na ufanisi. Bila elimu mtu huonekana hafai hata kama ana kipaji kizuri. Mtu asiye na elimu au mwenye kiwango duni cha elimu hujiona mnyonge na hukosa fursa nyingi za kujiendeleza kimaisha – anaangamizwa na ukosefu wa maarifa.

Tokea enzi na enzi elimu iliyorasmi na isiyorasmi hutafutwa popote pale na kugharimiwa ili kumtoa mtu katika ujinga na ufukara wa fikra. Kabla ya kuwa na shule na vyuo, watoto na vijana wetu walifundishwa na wazazi wao au jamii yao namna ya kuwinda, kurina asali, kuwasha moto kwa vipande vya miti na kuvipekecha kwa fimbo, kuvua samaki, kufuma nguo, kulima, kufua chuma, nk. Maarifa na elimu vilitolewa kwa njia isiyorasmi lakini iliyo thabiti, na tunaendelea kujifunza vitu vingi kwa njia zisizorasmi na rasmi. Vitabu, na sasa simu na kompyuta, ni hazina kubwa ya maarifa na elimu.

Elimu ipo katika nyanja mbalimbali na imekuwa ikiboreshwa kuendana na wakati kadri ugunduzi wa teknolojia na maarifa unavyozidi kuongezeka. Miongoni mwa walimu na wakufunzi wa elimu ni wazazi na/au walezi katika familia wakitufundisha masuala mbalimbali yahusuyo maisha yetu na mazingira yetu. Heshima na shukrani ziende kwa wazazi na walimu wote.

Elimu ina faida nyingi na muhimu sana katika maisha ya binaduamu. Mtu mwenye maarifa na elimu ana mtaji kwa ajili yake mwenyewe na pia naye ni mtaji kwa jamii na taifa kwa ujumla. Ndio maana serikali, taasisi na watu binafsi huajiri watu kulingana na viwango vyao vya maarifa, ujuzi na elimu.

Ulimwenguni kote rasilimali watu ni kwa watu wenye elimu na huchukuliwa kwa umuhimu wa pekee. Ingawa kila mtu ni muhimu katika jamii, na ana mchango wake – hata kama ni kubeba mizigo sokoni, lakini kwa dunia ya sasa thamani ya mtu imewekwa zaidi kwenye maarifa na elimu yake. Mtu mwenye maarifa na elimu bora hutafuta njia bora na vifaa au teknolojia stahiki ili kufanya kazi zenye tija, ufanisi na maendeleo.

Kadri tunavyoelimika ndivyo hata vipato vya maisha yetu huongezeka. Elimu pia hutuwezesha kuwasaidia wengine wasiokuwa na uelewa. Kwa muhtasari, baadhi ya manufaa na faida za elimu ni hizi zifuatazo:

  • Inatufanya tujitegemee na kuwa huru katika kufanya maamuzi sahihi na kwa weledi ili kujipatia kipato cha kuendeshea maisha yetu binafsi pasipo kumtumainia moja kwa moja mtu mwingine
  • Inatusaidia sana katika kuleta heshima ya kiwango fulani, sifa stahiki na usawa miongoni mwa wanajamii
  • Inatufanya tujiamini katika kujieleza na kutoa maoni, na watu hutuamini kutokana na kuthamini viwango vyetu vya elimu
  • Inatusaidia sana kupunguza kwa kiasi kikubwa umaskini uliokithiri miongoni mwa wanajamii na kutusaidia kuajiriwa na/au kujiajiri
  • Inatusaidia kuongeza tija katika uzalishaji mali na bidhaa mbalimbali kwa viwango vya juu
  • Inatusiaidia kustaarabika na kuishi maisha ya utengamano, uelewano na maridhiano miongoni mwa wanajamii na mataifa
  • Ni silaha kubwa ya kutokomeza ujinga na magonjwa, na aghalabu jamii huwa na mwamko mkubwa wa kutatua matatizo ya kiafya
  • Inatupa mwanga unaotuonesha jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha kwa ustadi na urahisi zaidi
  • Inatupa mbinu na njia mbalimbali za kuzibadili rasilimali asilia kuwa na tija na zenye faida katika maisha yetu
  • Taifa lenye watu walioelimika linakuwa na ukuaji wa kiuchumi (economic growth) na maendeleo ya kiuchumi (economic development).

Hitimisho

Urithi mkubwa na unaojitosheleza kwa watoto wetu si kuwapatia fedha, nyumba, ardhi, magari au vitu vyovyote vile tunavyomiliki. Bali ni kuwapatia maarifa na elimu. Ukimwezesha mtoto kusoma na kupata elimu, tayari umemrithisha na kumpa kila kitu. Unakuwa umemlipia mahari au umemwoza, umemjengea nyumba, umempa gari, umempa ajira na umempa mtaji wa kumsaidia yeye na familia yake. Unakuwa umempa utajiri, huna haja ya kuhangaika kumtafutia ajira au kuanza kumgawia mali yako kama urithi – urithi wake kutoka kwako unakuwa elimu na maarifa aliyopata.

Tukishapata maarifa na elimu, hatuwezi kuuza magogo ya miti au mbao zake, na kisha kununua kwa bei kubwa samani za thamani za miti na mbao hizohizo. Tukiwa na maarifa na kuelimika, hatuwezi kuuza ngozi za ng’ombe Kenya na kuja kununua viatu vya bei kubwa kuliko ngozi zetu tulizowauzia. Tukiwa na maarifa hatuwezi kuomba misaada kwa nchi zilizoendelea, bali tutachota maarifa na elimu ya nchi hizo ili ije itusaidie nyumbani.

Naam, tukiwa na maarifa hatuwezi kuuza makinikia huku tukiachiwa mahandaki na uharibifu mkubwa wa mazingira yetu. Bali tutahakikisha tunachenjua makinikia yenyewe sisi wenyewe na kuuza madini safi. Nchi za Japan, Malaysia, Singapore, Korea Kusini, Uswisi, nk.; zimeendelea baada ya kuchota maarifa na elimu ya kutosha na kuitumia nyumbani kwao.

Haziombi misaada au wataalamu wawaletee maendeleo. Hapana! Zinasaka maarifa na elimu ya kujiletea maendeleo yao. Tuyatafute maarifa na elimu popote duniani ili tusiendelee kuangamizwa na ujinga wetu. Maarifa na elimu ni nguzo ya mitaji ya kutuletea mafanikio katika maisha yetu. Tukibaki na ujinga wetu tunakuwa katika hatari ya kunyonywa na kutumika au kutumiwa na wengine kwa faida yao.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Gwandumi Gwappo A. Mwakatobe, mchambuzi huru wa masuala ya kitaifa na kimataifa, anayeishi Mwakaleli mkoani Mbeya. Anapatikana kwa anwani ya baruapepe: gwandumi@hotmail.com au gwappomwakatobe@gmail.com

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.