MOJA ya kauli nzito ambazo Rais Dk. John Magufuli amekuwa akizitoa wakati huu anapoendelea kuzunguka nchi kwa ziara rasmi ya kiserikali anayoiita ni ya kushukuru wananchi kwa kumchagua kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kushughulikia au kufuta dhambi.

Rais Magufuli anasema anafuatilia dhambi dhidi ya Taifa na Watanzania. Ni dhambi zilizopita. Ni dhambi zilizotokana na awamu zilizopita za uongozi wa nchi. Awamu za uongozi zenyewe zote zimekuwa chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Chama hicho kilichukua uongozi kama mrithi wa vyama vya Tanu na Afro-Shirazi (ASP), vilivyopigania uhuru wa Tanganyika na Zanzibar, nchi zilizozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuunganishwa tarehe 26 Aprili 1964. CCM ilizaliwa tarehe 5 Februari 1977 kufuatia kuunganishwa Tanu na ASP.

Rais Magufuli, kama walivyo marais waliomtangulia, ameingia uongozini kupitia chama hicho CCM; leo anaomba wananchi ambao anajivuna kuwa ndio waliompa ridhaa ya kuongoza, wamuunge mkono kwa namna mbalimbali katika kushughulikia dhambi.

Anasema anatenda kwa kuwa anawapenda wananchi na anasema anausema ukweli huo kwa kuwa msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Kama hiyo haitoshi, anasisitiza kwamba yeye ni rais wa wananchi wote na kwa hivyo anavyoenenda, anafanyakazi hiyo katika kuwatumikia Watanzania wote. Wao wananchi basi, wanao wajibu wa kuonesha moyo na kumuombea kwa Mwenyeezi Mungu.

Rais anasema anashughulikia mambo hayo ambayo yalifanywa kifisadi na kwa ajili ya maslahi binafsi ya wahusika hao na familia zao, matokeo yake yakawa ni kuwaumiza wananchi kwa kuwa yamesababisha serikali kunyimwa uwezo wa kuwahudumia kwa ufanisi.

Maelezo yake yana maana kuwa kwa kutendwa mambo ndivyo sivyo yanayohusu uendeshaji wa serikali ukitumia raslimali zake, watendaji wa serikalini na washirika wao waliofadhili mipango ya kutafuna au kufisidi uchumi wa taifa, walisababisha serikali ikose mapato stahili lakini pia waliifedhehesha serikali na kwa upana wake, jamhuri.

Katika lugha ya picha, mara nyingi ukiitafsiri unapata nguvu ya kuamini kuwa ni kweli huyu rais wa awamu ya tano, anakusudia kusema kazi hiyo anayoifanya ni jambo jema na katika kutimiza dhamira aliyoahidi wakati wa kampeni ya uchaguzi, ya kuwatumikia Watanzania wa vyama vyote vya siasa na hata wasiokuwa na vyama, hatofanya ubaguzi wa aina yoyote.

Wananchi wa Tanzania au Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamekuwa wakishuhudia utendaji serikalini ukileta matokeo yanayoathiri maisha yao ya kila siku. Matendo yanayofanywa na watumishi waliopewa dhamana na serikali ya wananchi yamekuwa mabaya na yakisababisha dhulma kubwa dhidi yao kwa muda mrefu.

Tayari katika utekelezaji wa dhamira yake rais, kuna idadi si haba ya kesi zimefunguliwa kwenye mahakama zetu na nyingi zingali katika hatua ya upelelezi.

Kwangu binafsi leo, nataka kuweka kumbukumbu vizuri kwamba nimekuwa napata uzito kumuelewa rais. Kwamba ni kweli amekusudia kufuta dhambi walizotendewa wananchi? Ni kweli anafuta dhambi kwa yote mabaya yaliyofanywa au anachagua baadhi yao huku mengine akiwa anayapita?

Je, utekelezaji wake wa kufuta dhambi unayaangalia hayo mabaya kwa kigezo cha uzito au anachukua hili na jingine kuliwacha? Isitoshe, anapofuta dhambi kwa yale maovu yaliyofanywa huko nyuma, analenga kuinua taswira ya nchi na watu wake kama nchi inayojali haki za watu au anakipalilia tu chama kilichompa ridhaa ya kuwania uongozi wa juu nchini? Niliseme moja. Suala la Zanzibar.

Kwamba Rais Dk. Magufuli ameridhika na msimamo wake ambao ndio msimamo khasa wa CCM kuwa Zanzibar isubiri uchaguzi mkuu wa mwaka 2020? Kwamba huo bado ni msimamo anaouamini kuwa unastahili?

Inawezekana Rais amesahau ahadi yake alipohutubia Bunge jipya la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, siku ambayo alikuwa analizindua tarehe 20 Novemba 2015.

Pale aliposema kuwa Zanzibar kuna tatizo kidogo katika uchaguzi wao na akaahidi kuwa atalitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na makamu wake, Mama Samia Suluhu Hassan, pamoja na Dk. Ali Mohamed Shein, alilenga kitu gani hasa?

Nataka kuamini kuwa alilijua kwa upana wake tatizo alolitolea ahadi kulitafutia ufumbuzi. Niamini alijua hivyo, kwa sababu zinajulikana njia kadha wa kadha za kuelezwa kilichotokea kuuhusu uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika siku ileile ya tarehe 25 Oktoba 2015, ya uchaguzi mkuu kwa upande wa nafasi ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge na madiwani wa Bara.

Kama Rais Dk. Magufuli alijua tatizo lililopo ndipo akathubutu kujitwika jukumu la kulimaliza ili Jamhuri yote iwe na amani na salama, miaka miwili sasa ikikaribia tangu pale, ndo tuseme ameridhika kabisa kuwa ameitimiza ahadi yake?

Ule msimamo mpya na mkali alioutoa wakati alipofanya ziara ya mikutano miwili Zanzibar – wa kwanza ukiwa uliofanyika kwenye Uwanja wa Gombani ya Kale, mjini Chake Chake, Pemba, na wa pili uliofanyikia Uwanja wa Demokrasia Kibandamaiti mjini Unguja – kwamba Dk. Shein ndiye rais aliyechaguliwa na wananchi wa Zanzibar, anaushikilia hata leo?

Siamini. Rais alitoa msimamo wa haki akiwa mbele ya Bunge siku ile Novemba 2015. Aliaminika kuwa amemaanisha au kama Waswahili wapendavyo kusema, “atatembea kwa maneno yake.” Ila kwa msimamo mpya kwenye majukwaa ya CCM ameondoka alipoahidi, na kuamua kupuuza au kuikanyaga ahadi yake.

Hivi Zanzibar ilivyo sasa imegawanyika huku zaidi ya nusu ya watu wakiwa wanyonge kwa sababu ya kuamini hawajatendewa haki kwenye uchaguzi ule, rais haoni kuwa anaongoza Jamhuri inayosononeka? Haoni kuwa ule umoja wa kitaifa na mshikamano wa kiuananchi uliokuwepo kabla na wakati uchaguzi unafanyika, umetikiswa na kutikisika vilivyo?

Ninamsihi atambue ukweli kuwa Zanzibar ambayo ni sehemu ya jamhuri anayoongoza tena akiwa ndiye amiri jeshi mkuu wa majeshi yote ya ulinzi na usalama; imegawanyika. Ni mgawanyiko uliotengenezwa kukidhi maslahi ya kisiasa zaidi kuliko kuona sehemu hiyo inapiga hatua ya maendeleo. Ni dhambi tupu ambayo mimi ninaamini asipoona hivyo leo, itakuja siku ataona, maana maji hayageuki maziwa hata yakipakwa rangi vipi.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MwanaHalisi la tarehe 7 Agosti 2017.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.