Binafsi sioni ushindi kwa yeyote kati ya Profesa Ibrahim Lipumba na Maalim Seif Sharif Hamad katika mgogoro unaoendelea sasa kwenye Chama cha Wananchi (CUF), bali ushindi pekee ni kwa wawili hao kupatana, kusameheana na kukiunganisha chama na wanachama.

Najua ni ngumu na yataka moyo, lakini wakati wote ukifaulu kufanya mambo magumu kwa kuthubutu na kujituma, mwishowe ushindi wake ni mtamu na hudumu.

Lipumba na Seif wametoka mbali na kufanya pamoja mambo mazuri mengi yanayowaunganisha zaidi kuliko mabaya machache yanayowatenganisha, huku wakiongoza chama ambacho kina historia ya mafanikio makubwa kwenye kuimaliza migogoro ya mazungumzo.

CUF waliwahi kuitwa na CHADEMA CCM B, lakini sasa vyama hivyo viwili ni marafiki wa chanda na pete kwenye muungano wao wanaouita UKAWA, Umoja wa Katiba ya Wananchi.

Dunia pia imejaa mifano tele ya aina hii. Nelson Mandela, mathalani, aliwahi kuteswa na makaburu lakini alipopata urais alifanya kazi nao pamoja na kuunda tume ya ukweli, maridhiano na kusameheana. Mandela alimpa mpinzani wake Chifu Mangisuthu Buthelezi wizara nyeti.

Raila Odinga nchini Kenya alihasimiana sana kisiasa na Mwai Kibaki na ukatokea umwagaji damu mkubwa. Baadaye walipatana wakawa pamoja, Raila Odinga akiwa Waziri Mkuu na Mwai Kibaki akabakia Rais.

Je, nani alitegemea uhasama na shutuma alizopata Lowassa, hasa kutoka CHADEMA kwa takribani miaka 8, leo hii angekuwa kada tegemeo kwa CHADEMA?

Mwaka 2000 Maalim Seif alipokosa urais dhidi ya Amani Abeid Karume yaliibuka machafuko makubwa yaliyomwaga damu nyingi Januari 2001 na kuzalisha wakimbizi. Lakini baadaye alipatana na Karume mpaka ikarekebishwa katiba iliyozaa serikali ya umoja wa kitaifa mwaka 2010.

Kumbe kwa upande mwingine, Maalim Seif ni mvumilivu, msikivu na mpenda majadiliano na upatanishi. Kama Maalim Seif alipatana na kufanya kazi pamoja na wana CCM kwa miaka mitano akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais, sioni kama atashindwa kupatana na Lipumba aliyefanya kazi naye kwa muda mrefu akiwa Mwenyekiti wake.

Ndani ya CUF, si mara ya kwanza kwa Maalim Seif kukosana na viongozi wenzake, wakiwemo James Mapalala na Hamad Rashid Mohammed. Bahati mbaya hakuwahi kusuluhishana na kupatana nao.

Sasa ni fursa adimu na adhimu kwake kukutana, kusalimiana na kusuluhishana na Lipumba. Chonde chonde Profesa Lipumba na Maalim Seif nawaomba tulieni, tafakari na kaa pamoja. Kumbukeni mema mengi mliyofanya pamoja na muyaenzi kwa kufuta mabaya machache yaliyojitokeza ili mpate ushindi pekee na utakaowaletea heshima kwa Watanzania na kukiunganisha chama na wanachama wenu.

Maelewano, mapatano na maridhiano ni mbegu njema kwa watoto na watoto wa watoto wetu kama alivyofanya Mandela.

Napendekeza jamii ya wapenda amani, demokrasia na upatanishi, tuwawezeshe Profesa Ibrahim Lipumba na Maalim Seif kukutana ana kwa ana, na kila mmoja apewe nafasi ya kusikilizwa vya kutosha kwa kile kinachomuumiza na kumsumbua dhidi ya mwenzake.

Kisha pale inapowezekana, kila mmoja aeleze yale ambayo anaona mwenzake amewahi kufanya vizuri au kila mmoja ataje mema ambayo anaona mwenzake anayo. Mimi binafsi, ikiwapendeza wahusika, najitolea kuwapatanisha viongozi hawa. Najua sina cheo au wadhifa wowote mkubwa katika jamii, lakini najisikia uchungu na maumivu yaleyale wanayoyapata hawa wawili, wanachama wa CUF na wote wanaopenda amani.

Kwa yeyote mwenye mawasilino na hawa wawili aniunganishe nao. Vyama vya upinzani hususan vya muungano wa UKAWA, kama wataitambua busara hii, watoe tamko la kuunga mkono upatanishi huu.

Tuwaponye wanachama na kuwaonesha ukomavu wetu wa kutatua migogoro. Ndio njia pekee na bora kabisa ya kumwaibisha adui anayeutumia mgogoro huu kudhoofisha vyama vya siasa na demokrasia nchini.

Profesa Lipumba na Maalim Seif wakubali kustaafu na kubakia wazee wastaafu wa chama wenye busara. Sambamba na hilo, katiba ya chama irekebishwe ili kuweka kipengele maalum cha baraza la busara na ushauri la wazee wastaafu. Na kisha uchaguzi maalum ufanyike ili kujaza nafasi ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu Taifa.

Mwishowe, iandaliwe hafla fupi na chakula maalum cha kuwakutanisha, kuwapongeza, kuwaenzi na kuwaaga rasmi wastaafu Profesa Ibrahim Lipumba na Maalim Seif. Kwenye hafla hiyo waalikwe viongozi wa vyama vyote vya siasa, viongozi wa kijamii na watu maarufu wenye hekima kutoka ndani na nje ya nchi. Washuhudie na kutoa nasaha zao za jinsi Waafrika tunavyotatua migogoro yetu kwa ustaarabu na uungwana wa Kiafrika.

Nihitimishe kuwa kabla ya kufariki Januari 30 1948, Mohandis Karamchand Ghandi, almaarufu Mahatma Ghandi, alituasa kwa kusema, nanukuu: “Kazi yangu katika maisha kwa miaka 33 iliyopita, imekuwa kuorodhesha urafiki na watu wote, kwa kuwafanya wawe marafiki bila kujali asili ya mtu, rangi au imani.”

Naam, Lipumba na Maalim Seif rejesheni urafiki wenu, na mnayo nafasi na ushawishi mkubwa wa kukinusuru chama.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Gwappo Mwakatobe, mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii anayeishi Mwakaleli, Mbeya, kama sehemu yake ya kuchangia suluhu ndani ya CUF. Mwandishi anapatikana kwa anwani za barua-pepe gwandumi@hotmail.com na au gwappomwakatobe@gmail.com

One thought on “Maalim Seif, Profesa Lipumba ndio pekee wa kuinusuru CUF”

  1. Mwakatobe umetoa ushauri muhjmu , lakini historia au chanzo cha mgogoro huu na nia ya kuletwa huu mgogoro na huyo alie uleta inatia mashaka kukubali kuondoka kwasababu tu ya maslahi ya chama. Agenda ya mleta mgogoro ni kubwa na hajatimiza aliyotumwa. Atawaeleza nini wafadhili wake.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.