Licha ya Zanzibar kutajwa kuwa nchi ya tatu duniani kwa kuzalisha mwani kwa wingi na wenye kiwango kizuri, bado wakulima wanalalamika kutofaidika vya kutosha kwa kilimo hicho.

Wakulima wa mwani ambao ni zaidi ya 20,000 visiwani Zanzibar – wengi wao wakiwa wanawake wa vijijini – wamekuwa wakipanza sauti zao kutokana na bei ndogo, kodi iliyokithiri, ukosefu wa vifaa na kufanyakazi katika mazingira magumu.

Kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015, wanasiasa wa pande zote mbili kuu waliyatumia sana majukwaa ya kampeni kwa kuwaahidi wakulima wa zao hilo  kwamba wangeliwabadilishia maisha yao kwa kuimarisha kilimo hicho.

Dk. Ali Mohamed Shein wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliahidi ugawaji wa vihori (vifaa maalumu vya kubebea mwani baada ya kuvunwa baharini) na pia kujenga viwanda vya usindikaji zao hilo hapa hapa Zanzibar.

Lakini hadi leo, wakulima na wauzaji wa mwani wana kilio kile kile cha awali – kodi iko juu, bei ni ndogo, gharama za kilimo haziendani na mapato.

Katika maonesho ya Siku ya Mwani Zanzibar mwaka huu, mkulima Mariam Pandu Kweleza kutoka kijiji cha Bwejuu alimuambia mkuu wa shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Idd, kuwa kazi wanayofanya ni ngumu  na huku pato wanalolipata si robo ya maumivu ukulima wa kilimo hicho.

Baadhi ya bidhaa zitokanazo na mwani wa Zanzibar.

“Mheshimiwa, kilo twauza kwa shilingi 300. Kweli zitaweza kufuta jasho letu? Kazi hii ni ngumu mno na sasa hivi tunaambiwa ni zao la tatu kwa kuingiza fedha za kigeni lakini wakulima bado twaumia!”

Alieleza kuwa bei ya zao hilo inapangwa na makampuni bila kuangalia kazi ngumu zinazofanywa na wakulima hao, ambao wengi wao ni wanawake tena wajane.

Amina Khamis, muuzaji wa bidhaa zinazotokana na zao la mwani, anasema kuwa makato wanayokatwa ni makubwa kupitia taasisi mbili tofauti zza kodi – Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB), ambapo muuzaji mwani nje ya Tanzania hukatwa asimilia mbili ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) utoka TRA na baada ya mauzo hayo hukatwa tena asimilia kutoka ZRB.

Kilio cha wakulima na wafanyabiashara ya mwani kinafanana na sekta nyengine zote za biashara zinazofanyika Zanzibar. Mapungufu ni yale yale, madai ni yale yale, ahadi ni zile zile, lakini kisha hali inasalia kuwa vile vile.

Je, kuna jitihada zozote za kubadilisha mambo? Ndiyo, katika kutafuta njia ya kuwanyanyua na  kuwaendeeleza wakulima hao ambao hufanya kazi zao baharini, Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation imekuja na mpango maalumu kwa kushirikiana na Taasisi ya Zanzibar Seaweed Cluster Initiative ( ZaSCI) kuongeza usarifu na matumizi ya mwani na kupandisha juu mahitaji na matokeo yake, kwa hivyo, kupandisha bei ya zao hilo.

Bi Khadija Shariff, Mkurugenzi Mtendaji wa taasis ya Milele Zanzibar Foundation, anasema ili kufikia hatua hiyo panahitajika kwanza kuwa “viwanda vya kusarifia mwani ndani ya nchi ambapo ndani yake utaweza kutengeneza sabuni za mwani, shampoo, dawa za meno, poda, mafuta ya kung’arisha mwili, keki, jam…”

“Ikiwa ushirikiano nzuri baina ya wazalishaji na taasisi utaendelea, basi hakuna litakaloshindikana”, anaongeza Bi Khadija.

Mwani wa Zanzibar unaweza kuwa njia kuu ya uchumi wa visiwa hivi vidogo lau nchi itajpanga kikamilifu.

Milele Zanzibar Foundation inajihusisha, pamoja na mengine, na kutafuta fursa zilizopo visiwani Zanzibar hasa zile zinazoweza kuwainua kiuchumi wananchi wa visiwa hivi. Ndipo ilipogundua kuwa zao la mwani linaweza kuwa ni miongoni mwa fursa kuu zinazopatikana na zinazoweza kuwakwamua kiuchumi wakaazi wa visiwa hivi vya Bahari ya Hindi.

Baada kutambua na kuvutiwa na kazi nzuri za Kongamano Bunifu la Mwani Zanzibar mwaka 2015, taasisi hiyo sasa imeungana mkono na kongamano hilo ili kuwajengea uwezo wakulima na wasarifu wa mwani katika kupata taaluma na kuwawezesha katika kujenga mashirikiano mazuri na wadau wengine wa sekta ya mwani.

“Hadi sasa tumeweza kufanikisha uzinduzi wa Siku ya Mwani Zanzibar kwa lengo la kuutangaza na kueneza uelewa wa matumizi na faida za mwani,” anaeleza Khadija.

“Tunaishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuamua kuwa siku hii itakuwa inaadhimishwa kitaifa kila mwaka.”

Alieleza kuwa wamefanikiwa kuwapatia wakulima na wasarifu wa mwani elimu ya ujasiriamali na kuwafumbua macho namna ambavyo wanaweza kujikomboa kimaisha kupitia zao hili.

“Pia tumefanikiwa kuwakutanisha wakulima, wasarifu, wauzaji, wasafirishaji na wadau wote wa mwani  kwa kufanya mikutano kila baada ya miezi mitatu kwa lengo la kujadili changamoto zinazoukabili mwani na namna ambavyo wanaweza kujinasua katika changamoto hizo,” anafafanua Khadija.

Mwani huuzwa na kutumiwa sana katika mataifa ya  Japan, China, Korea Kusini, Denmark, Ufaransa, Singapore na Marekani kama chakula na bidhaa nyengine.

Kwa Zanzibar, biashara ya zao hili ilikuwepo tangu miaka ya 1950 kwa kuokotwa mwani wa asili baharini, lakini kuanzia mwaka 1989 ukaanza kulimwa rasmi kwa mbegu za kutoka Ufilipino. Mbegu hizo aina ya Spinosum na Cottonii ndizo zinazolimwa hadi hivi leo.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Talib Ussi

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.