KIBURI ni uovu uliokatazwa na maandiko matakatifu. Mwenye nacho amedharau utu. Ni kwa maana hiyo hata wahenga walifikia hitimisho la kuwa na methali ya Kiswahili inayosema ‘kiburi si maungwana.’

Methali hii ina maana kuwa mtu mwenye heshima na busara hatakiwi kuwa na kiburi. Ni methali inayotumika kusisitiza kuwa mtu muungwana sharti awathamini wenzake na kuwatendea haki na sawa.

Katika maisha ya binadamu, wapo watu wanaoaminika kuwa viongozi kwa kuchaguliwa na wananchi, siyo wa kujitwalia madaraka kwa nguvu za mtutu wa bunduki, aghalabu hujifunza uungwana.

Hujiepusha na kiburi, kwa kuwa kiburi kinajenga umimi, jeuri, ubabe na kupuuza wengine. Kiburi kinajenga na kuushibisha moyo wa binadamu ganzi ya kukosa utu, huruma. Kiburi ni mama na baba ya uharibifu wote kwa mwanadamu.

Katika historia ya viongozi wa Tanzania waliopata kukaa Ikulu kwa ridhaa ya wananchi, wapo watano. Kwa sasa yupo Rais John Magufuli. Kabla yake, alikuwapo Jakaya Kikwete (2005-2015), ambaye aliachiwa kiti na Benjamin Mkapa (1995-2005).

Mkapa akiwa rais wa tatu alipata madaraka baada ya Ali Hassan Mwinyi (1985-1995) aliyempokea kijiti Muasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere (1961-1985).

Katika orodha hii, ukiweka pembeni aliyepo madarakani na kwa maana hiyo si haki kumjadili hapa kwa sababu hajamaliza ng’we yake, waliobaki wanne, hakuna wa kufananishwa na Mkapa kwa kiburi.

Mkapa ni kiongozi pekee mstaafu wa ngazi ya urais mwenye ujasiri wa kutukana wananchi. Kuwatusi wale anaoamini wana mawazo tofauti na yake. Kwake, anayetofautiana naye ni ‘mpumbavu na lofa.’

Akiwa wilayani Chato wiki iliyopita, Mkapa alirejea maneno aliyoyatamka mwaka 2015 viwanya vya Jangwani, kwenye mkutano kuzindua kampeni za kusaka urais za mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Magufuli.

Alisema wanaosema habari ya ukombozi wa nchi ni ‘wapumbavu na malofa.”

Pamoja na kuwako na shutuma nyingi dhidi yake kutokana na kauli ya ‘upumbavu na ulofa’ takribani miaka miwili baadaye, bado kiburi hakimuachii kutambua kuwa anatumia lugha ya kuudhi na kudharau wananchi.

Dhidi ya walipakodi wanaomwezesha kuishi maisha ya raha na amani. Anaamini kila anayesema ambayo hataki kusikia ni mpumbavu na lofa.

Kamusi ya Kiswahili Sanifu inaelezea lofa kama mtu anayezururazurura, asiye na kitu wala kazi. Mpumbavu anatajwa kuwa mtu anayeshindwa kuelewa jambo hata akielezwa. Kwa meneno mengi anaitwa juha, zuzu, nyange, banghami, bahau, fala, hambe, jahili, mbumbumbu na mengine mengi.

Ungeliweza kuelewa na kuvumilia kwamba mwaka 2015, huenda Mkapa alihemuka kama wahemukavyo wanasiasa wengine wanapoona umati kama uliokuwa umejitokeza kushiriki fungua kampeni ya mgombea urais wa CCM.

Lakini miaka miwili baadaye anasema maneno yaleyale, tena safari hii mbele ya yule aliyekuwa anamnadi Jangwani. Kitu pekee kinachotoa ujasiri huo kwa kiongozi mstaafu wa aina yake ni kiburi. Kiburi tu.

Wapo watu wamejiuliza maswali mengi juu ya kiburi cha Mkapa. Kwamba kinatokana na nini? Wapo wanaonasibisha kiburi hicho na tabia, makuzi na hulka yake. Wengine wanasema ni matokeo ya shibe na kinga ya kutenda bila kujali nini kitampata kwa sababu ya kuzama kwenye kichaka cha sheria na mifumo ya kulindana uliowekwa na CCM.

Mifumo yenyewe inawasukuma washika madaraka kuamini hata wakitoka, watakuwa tu salama hata kama walikosea walipokuwa wanatenda.

Hivi, kama kiongozi aliyekaa ikulu kwa miaka 10 na akiwa ameshikilia nafasi za uwaziri, ubalozi na hata utumishi wa ngazi nyingine serikalini kwa zaidi ya miongo minne, si tu alitarajiwa kujifunza kuwa mnyenyekevu, bali mwalimu kwa wengine. Uongozi ni utumishi.

Kwa nini anaona Watanzania hawana kitu -malofa? Mkapa anaposema “watu wenye mawazo tofauti na watawala ni malofa” anakusudia kuwadhalilisha kwa sababu wanahoji ambayo yeye Rais Mstaafu amekuwa sehemu ya uwajibikaji wake.

Malofa hawa wamefikishwa walipo. Ni kweli hawana kitu. Ni vipi mwananchi hohehahe atakuwa sawa na rais mstaafu anayeishi na kugharamiwa kila kitu kwa kodi za wananchi?

Ni vipi mwenyekiti wa chama cha siasa kisicho hata ruzuku ya serikali, apate maisha mazuri sawa na rais mstaafu? Ni vipi mwananchi wa aina hiyo atakuwa na walinzi kadhaa wa kumlinda kila aendako; ni vipi atakuwa na nyumba inayogharimiwa na serikali kila kitu.

Huyu rais mstaafu analipwa mshahara wa asilimia 80 ya mshahara wa rais aliyeko madarakani; nyumbani ana wapishi watatu; mtunza bustani; anabadilishiwa gari kila baada ya miaka mitatu na anagharamiwa angalau safari mbili nje ya nchi kila mwaka na anatibiwa kwa kodi za wananchi.

Kwa mfumo wa maisha na stahili za rais mstaafu hawezi kuwa lofa. Lakini kitu kimoja cha msingi malofa ambao Mkapa anawakejeli yumkini wapo wanaoendesha maisha kwa kujikimu kwa kilimo, wanalipa ushuru na kodi nyingine ambazo serikali huchukua na sehemu yake ndizo zinatumika kumpa yeye maisha ya ukwasi.

Lakini kitu kingine anachosahau ni kwamba hao malofa anaowakejeli hawakupata fursa na hawakuwa sehemu ya mpango wa miaka 10 wa serikali yake wa kuuza na kukwapua mali za umma- mashirika, nyumba na rasilimali nyingine nyingi. Kwa hiyo wanufaikaji wa sera za kupora mali ya umma chini ya kivuli cha ubinafsishaji, ndio wenye jeuri ya kuwaita wengine malofa.

Hakuna lofa aliyepewa nyumba ya serikali kwa bei ya bure kwa kisingizio cha kuwa mtumishi wa umma katika sakata la karne la watumishi wa umma kuamua kilaghai chini ya Mkapa kuuziana nyumba za serikali kwa bei ya kutupa. Kwa kuwa hawana nyumba za kupeana bure, ndio waitwe malofa?

Kikubwa zaidi ni malofa kwa sababu hawakushiriki kuandaa mikataba ya kilaghai iliyowapa wawekezaji umiliki wa raslimali ya madini, gesi, vitalu vya uwindaji na mapande ya ardhi yasiyoendelezwa.

Kwa hiyo, Mkapa kama mtu mzima wa umri na uelewa, kinachomsumbua ni kiburi cha ukwasi unaotokana na rasilimali za taifa. Ni kiburi kinachochangiwa na ulinzi wa sheria na mifumo walioiasisi kwamba wana haki ya kutenda makosa pasina kuadhibiwa – utamaduni wa kulindana (culture of impunity).

Kwa matusi yake ya rejareja anazidi kuthibitisha kuwa ameshindwa kuwa kiongozi wa taifa (statesman), badala yake anajiona kuwa salama yake ni kutetea mifumo ya ovyo ya kupora rasilimali za taifa; kupiga vita uwazi, uwajibikaji na demokrasia.

Ameshindwa kujielewa kuwa kwa nafasi alizowahi kushika ingempasa sasa kuamini – maana anatambua – kuwa kiburi si uungwana na ni vibaya mtu aliyeshiba kulala mlalo wa kumwonyesha Mungu tumbo lililofura. Ajue, shujaa muungwana huacha asili.

TANBIHI: Makala hii iliyoandikwa na Chris Alan ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la MwanaHalisi la tarehe 17 Julai 2017.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.