Tarehe 2 Julai 2017, kwa nia wizara ya kazi, uwezeshaji, wazee, vijana, wanawake na watoto ilitangaza kima kipya cha mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi Zanzibar kupitia Waraka wa Sheria Nambari 69 (Legal Notice no. 68), ambacho kiliamuriwa kuanza kutumika kuanzia tarehe 1 Julai 2017.

Mabadiliko hayo yanawafanya wafanyakazi wenye hadhi ya kuwa na mikataba ya maandishi, mishahara yao kuongezeka kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 145,000/- hadi kufikia 300,000/-, ambapo ongezeko hilo ni zaidi ya asilimia mia moja. Mabadiliko hayo yamefanyika chini ya Kifungu cha 97 (1) cha Sheria ya Ajira nambari 11 ya mwaka 2005. Mbali na hayo, kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi wa mikataba ya maandishi kwa taasisi ndogo zitakazoainishwa katika kanuni, kimeongezeka kutoka kiwango cha sasa cha shilaingi 145,000/- hadi kufikia 180,000/- kwa mwezi.

Wizara inasema kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi vibarua wa kutwa wenye ujuzi kimeongezwa kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 10,000/- hadi 30,000/- kwa siku. Aidha kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi vibarua wa kutwa wasio na ujuzi, kimeongezwa kutoka shilingi 7,000/- wanazolipwa hivi sasa hadi kufikia 25,000/- kwa kutwa.

Kwa maamuzi hayo ya kisheria kabisa yaliyochukuliwa na wizara hiyo, hakika yangestahiki kupongezwa sana na Wazanzibari, lakini kwa mtazamo wangu kidogo napata ukakasi kuyapongeza maamuzi haya.

Na Ali Mohammed

Tarehe 5 Mei 2015 niliandika makala Sera ya Ajira ya Zanzibar Ndiye Adui wa Vijana, ambayo ina lengo la kutetea maslahi ya Wazanzibari katika sekta za ajira, hususan, katika sekta binafsi, nikionyesha jinsi sera hiyo iliyotungwa mwaka 2009 inavyokosa utekelezaji wake kutokana na kwamba inapingwa na sheria zetu za ajira zilizopo, ambazo hadi leo hazijabadilika wala kurekebishwa katika sehemu muhimu ili ziwabebe Wazanzibari katika masuala ya ajira kupitia sekta binafsi.

Kwa muktadha huo huo, hata waraka huu nambari 68 (The Legal Notice No. 68) bado haujamnufaisha Mzanzibari hata kwa asilimia 50, nikiwa mdau wa ajira Zanzibar bado sheria zetu hazijaruhusu Wazanzibari waliowengi wapate fursa za ajira katika sekta binafsi hususan katika sekta ya utalii hasa hasa sekta ya mahotelini.

Sitaki nionekane kama labda kuna upande fulani naubagua, la hasha, lengo ni kuisaidia serikali na taasisi husika ili ziweke mazingira ya kisheria ambayo yatamuwezesha mzawa kupata fursa kwanza na baadae mgeni afuatie, na nafanya hivi kwa sababu usipompa nafasi ya ajira mzawa unadhani atakwenda wapi aajiriwe?

Kuna sababu tofauti ambazo zinamfanya Mzanzibari asinufaike katika kupata ajira katika sekta binafsi ambapo zinamzuia kutofaidika na kima hichi kipya cha mshahara kwa sekta binafsi, ambapo ni jambo la historia katika nchi yetu:

  1. Kutokuwepo watendaji wa juu wa Kizanzibari katika makampuni binafsi. Hii ni sababu moja wapo kuu na ya msingi sana, naweza kusema asilimia zaidi ya 90 katika mgawanyo wa madaraka kwa nafasi za juu za usimamizi katika sekta binafsi, basi wawekezaji wengi wamewapa watu kutoka nje ya Zanzibar, ambapo nafasi za juu aidha hupewa raia wan chi za Ulaya, Asia, Kenya na Uganda, nafasi za katikati hupewa watu kutoka Kenya na Tanzania Bara, panapokuwa na mahitaji ya ajira mara nyingi watu wa nafasi za kati hufanya ushawishi kwa viongozi wao ili walete marafiki na ndugu zao ambapo huwa si Wazanzibari.
  2. Ruhusa ya sheria zetu. Kuna haja ya kuzipitia na kuzifanyia marekebisho sheria zetu zinazosimamia ajira, kwani sera ya kila nchi duniani ni kuhakikisha inawapatia ajira wananchi wake, ili kupunguza umasikini, lakini sheria zetu zinazosimamia ajira zinatoa mwanya wa kuzidisha umasikini kwa raia wazawa kwa sababu wazawa wengi hawapati fursa ya ajira katika sekta binafsi, jambo ambalo linawafanya Wazanzibari wengi kurundikana ofisi za Tume ya Utumishi wa Umma kusubiria ajira za serikali, takribani sheria zetu zote zinazosimamia ajira visiwani Zanzibar hazitoi fursa ya kisheria inyohakikisha Mzanzibari kuwa ni mtu wa mwanzo kupewa ajira. Katika sheria nambari 11 ya mwaka 2005 kifungu nambari 36 (1) kinasema: “Hakuna Muajiri atakayeruhusiwa kuajiri mgeni isipokuwa: (a) endapo hakuna Mzanzibari mwenye sifa zinazotakiwa katika nafasi hiyo.”

Wakati kifungu hichi kinatungwa na kuwekwa katika sheria hii, nakubali kwamba zama zile kweli hakukuwa na Mzanzibari aliyekuwa na uwezo wa kuajiriwa katika nafasi nyingi hasa katika sekta ya hoteli na utalii, lakini kwa sasa kifungu hichi kimepitwa na wakati, wahitimu wapo isipokuwa kizuizi kipo katika sababu nambari moja ambayo nimeieleza hapo juu na kizuizi chengine ni ruhusa ya kisheria ambayo muajiri amepewa ruhusa na sheria yetu ya Vitega Uchumi ya mwaka 2004 ambapo muajiri pia amepewa ruhusa kuajiri mtu aneyemtaka kwa sababu za kiufanisi na imani ya kibiashara.

Endapo tuna nia ya dhati kumnufaisha Mzanzibari katika masuala mbali mbali yakiwemo haya ya ajira binafsi na mishahara na tuna imani na kuitakidi kwamba ndiye raia muhimu wa Zanzibar na mwenye haki namba moja, basi kuna haja kuzifumua sheria zetu zote zinazosimamia ajira na kusifuma upya, kwa kuweka vipengele katika sheria hizo vitakavyolazimisha kila muekezaji kwa uchache awe ameajiri mzanzibari kwa asilimia 60 tu, na asilimia 40 zilizobakia iwe kwa watu kutoka nje ya Zanzibar.

Pia kuwe kuna utaratibu wa hawa viongozi wa juu wawe wanaajiriwa katika sekta binafsi kwa muda mchache na sio muda mrefu kama ilivyo sasa, ili kuwapa fursa na Wazanzibari kufanya kazi za kiungozi katika makampuni binafsi, kwani naamini kwa Zanzibar ya sasa kila fani Wazanzibari wapo, kinyume na hivyo serikali ya Wazanzibari itaendelea kuwaboreshea maslahi wasio Wazanzibari ndani ya Zanzibar yao.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.