MAMLAKA  na madaraka ni vitu hatari. Vinahitaji umakini mkubwa kuvimudu. Ni kwa sababu vitu hivyo wakati mwingine vinalevya na kumfanya aliye juu yavyo kujisahau na kujiona ni kitu kingine tofauti na binadamu wenzake alio nao.

Mamlaka na madaraka vinaweza kumfanya mtu aamue atakavyo bila kujali maamuzi yake yataleta madhara gani ndani ya jamii aliyomo. Matokeo yake mamlaka na madaraka vinajenga chuki, vinatengeneza vinyongo, uhasama wa kudumu na hatimaye kujenga uadui ndai ya jamii husika.

Mamlaka na madaraka vina tabia ya kuwapofusha wale waliovishikilia wasiweze kuangaza na kupaona mbele ya pale walipo, ambapo baadaye vinawageuka na kuwaponza hasa pale vinapokuwa vimewatoka. Ndiyo maana nikasema kwamba vinahitaji umakini mkubwa kuvimudu.

Kwa hiyo, tunapotaka kujenga jamii isiyo na uhasama wala chuki iwezayo kusababisha uadui, jamii isiyo na vinyongo viwezavyo kusababisha kulipiza visasi, tunatakiwa kuvichukulia kiuadilifu vitu hivi viwili, mamlaka na madaraka.

Kuna hadithi ya mtawala mmoja mbabe katika himaya ya Kirumi aliyeitwa Julius Kaizari, yeye alileweshwa na vitu hivyo, mamlaka na madaraka, akawa haoni wala hasikii. Hakukiogopa kitu chochote akidai kwamba waoga hufa mara nyingi kabla ya vifo vyao, wakiona kitu wanashtuka, oh mama nakufa, yeye akisema jasiri hafi ila mara moja!

Lakini siku moja alishtukia mamlaka na madaraka vinampotezea ujasiri wake pale alipoanza kushambuliwa na watu wake mwenyewe huku aliyekuwa kipenzi chake, Marcus Junius Brutus, akiwa ndiye anayeongoza mashambulizi hayo wakati Kaizari akishangaa kwamba “na wewe Brutus!”.

Kaizari aliangamizwa kwa kutoyachukulia mamlaka na madaraka kwa uangalifu. Alileweshwa na vitu hivyo, akajisahau na kuona angeweza kufanya kila alichokitaka kwa vile ndiye aliyekuwa bwanamkubwa.

Watawala wengi, hususan wa Afrika,  wanashindwa kupata mafundisho kutoka kwenye hadithi hiyo na baadaye kujikuta yanawapata yaliyompata Julius Kaizari au zaidi yake. Mtu mmojawapo ninayeweza kusema kwamba aliweza kupata fundisho akiwa madarakani ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alikuwa mpenzi mkubwa wa hadithi za William  Shakespeare.

Idd Amin Dada wa Uganda alileweshwa na mamlaka na mdaraka akaishia kutimuliwa kama mbwa koko toka nchini mwake na kufia ughaibuni. Wapo wengi wa aina hiyo, Ngbendu Mobutu Sese Seko wa Zaire, Jean Bedel Bokassa wa Afrika ya Kati, Francisco Nguema nakadhalika.

Wengine ni kama Frederick Chiluba wa Zambia, kipindi kaingia madarakani akaanza kumsumbua sana Baba wa Taifa wa Zambia, Mzee Keneth Kaunda. Inakumbukwa alipomuweka ndani bila sababu za maana Kaunda akagoma kula chakula mpaka swahiba wake, Mwalimu Nyerere, alipokwenda Zambia na kumfuata gerezani akimtaka ale chakula.

Lakini baadaye, pamoja na Chiluba kumweka mrithi aliyeamini atamlinda, Mwanawasa, hakuwa na jeuri ya kuikwepa “lupango” aliyodhani imetengenezwa kwa ajili ya Kaunda tu! Aliingizwa ndani na hatimaye kupoteza maisha kutokana na misukosuko aliyojitafutia mwenyewe kwa ulevi wa mamlaka na madaraka!

Mtu pekee, tena aliye wa aina yake,  ni Madiba, Nelson Mandela wa Afrika Kusini. Baada ya kutoka ndani alikowekwa kwa miaka 27 kwa uonevu wa makaburu, akawa na kauli ya kwamba yaliyopita tuachane nayo tuangalie tu yaliyo mbele yetu. Mzee huyo alidhamiria kuijenga jamii isiyokuwa ya vinyongo wala visasi.

Kilichonisukuma kuyasema hayo ni mambo ninayoyaona hapa nchini kwetu katika utawala huu wa serikali ya awamu ya tano. Tunaona kwamba mamlaka na madaraka vimeshika kasi katika kukilazimisha kila kitu kifanyike kadri ya walio na mamlaka na madaraka wanavyotaka kiwe. Haijalishi kama kitu hicho kipo kwa mujibu wa taratibu na sheria!

Jambo lingine ni lile la kuwabana na kuwakomoa wanaoonekana ni wapinzani wa serikali iliyo madarakani, japo upinzani upo kwa mujibu wa sheria, lakini bado unaonekana kama ujambazi unaopaswa kufutwa kwa nguvu zote!

Tumeshuhudia viongozi wakuu wa kambi ya upinzani wakifanyiwa mambo yasiyositahiki hata kidogo bila kujali kwamba uwepo wao unafuata Katiba ya nchi kama walivyo viongozi wa serikali. Mfano kiongozi mkuu wa kambi ya upinzani, Freeman Mbowe, ambaye pia ni mbunge amefanyiwa mambo mengi machafu dhidi ya mali zake binafsi!

Kavunjiwa ofisi binafsi na sehemu za biashara zake, kaharibiwa mali zake nyingi pale zilipokuwa ofisi hizo na sehemu ya biashara, kikaingiliwa kilimo chake cha kisasa kule Kilimanjaro na kuharibiwa kikatili. Hiyo yote ikiwa ni kumkomoa kwa vile ni kiongozi mkuu wa upinzani!

Kwa mtindo huo kinachojengeka kwenye jamii yetu ni kitu gani kama sio vinyongo, chuki na mawazo ya kulipiza visasi? Hata kama sio kwa leo, hiyo inajengwa ndani ya roho za hata vizazi vijavyo.

Mfano ukiwauliza Wapalestina na Waisraeli wanapigania nini kwa sasa, yawezekana husipate jibu. Maana kule kila mtoto anayezaliwa na kuanza kupata akili maramoja anaambiwa fulani ni adui, hata kama hajui uadui huo ukoje!

Mimi nadhani mamlaka na madaraka tusingeviachia vikatusambaratisha kiasi hicho. Ungekuwepo umakini wa kuvimudu tukielewa kwamba ipo siku walio madarakani kwa sasa  watakuwa nje ya madaraka wakati ujao. Kwahiyo ili kuyaepuka yaliyowakuta niliowataja, huu ndio uliokuwa wakati bora wa kujitofautisha nao.

Sababu fikiria Mbowe au mwanae  anaingia madarakani wakati kiongozi wa sasa au mwanaye akiwa nje ya madaraka hali itakuwaje? Maana sio binadamu wote wana roho kama ya Mandela, wapo wenye vinyongo na visasi. Kwa mtindo huo si inaweza kutokea Palestina na Israeli ndani ya jamii yetu?

Kama tunataka kujenga jamii yenye amani na utulivu ulio endelevu tunapaswa kuanza sasa, tusijali tu kwa vile sisi tumevifaidi vitu hivyo, tuviangalie hata vizazi vyetu huko mbele. Tusiachie mamlaka na madaraka vikaisambaratisha jamii yetu.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Prudence Karugendo. Anapatikana kwa barua pepe: prudencekarugendo@yahoo.com, au kwa simu nambari +255 784989512

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.