Mahali popote penye vivutio vya utalii panapaswa kujihusisha na siasa za utalii ili kujadiliana, kujipanga na kuainisha sera na mikakati ya kuendeleza na kutangaza vivutio vya utalii vinavyoweza kuinua na kuboresha uchumi wa mahali husika na taifa kwa ujumla. Nyanda za Juu Kusini Magharibi zina vivutio kedekede katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa na sehemu ya kaskazini magharibi ya mkoa wa Ruvuma yenye wilaya za Nyasa na Mbinga.

Hali ya hewa na maeneo ya asili ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi ni mithili ya bustani ya edeni ya zama hizi. Milima ya kupendeza iliyojipanga kimiujiza na kuinuka juu sana mawinguni pamoja na kupambwa na misitu minene inalifanya eneo la ukanda huu kuwa kivutio kikubwa cha mandhari ya kiasili na kivutio kikubwa cha utalii. Ukianzia mwinuko wa mlima Rungwe uliokaa kama uyoga na kuendelea usawa wa safu ya milima ya Ukinga (Livingstone Mountains) kuelekea Mbinga, utastaajabu na kushuhudia ustadi na usanifu mkubwa wa milima hii. Dr David Livingstone, akiwa upande wa Malawi alistaajabu sana mpangilio na mwinuko huu na historia imelienzi jina lake kwa kupewa milima hii, japo hakuweza kufika.

Ukiwa upande wa bonde la Mwakaleli, milima ya Livingstone inaonekana kama vile inaning’inia mawinguni. Inapendeza sana! Wakati mwingine huogofya kama vile inakaribia kuporomoka. Vivyo hivyo, ndivyo ilivyo kwa milima ya Udzungwa kuanzia Mufindi kusini, kuelekea Malinyi, Kilombero, Mikumi, kusini mwa Mpwapwa, maeneo ya Mtera, mbuga ya Ruaha hadi mashariki mwa Mbarali. Katikati ya nyufa za milima hii kuna vijito na mito yenye maji meupe yakitiririka saa 24 kila siku kuelekea mabondeni. Aidha, misitu katika milima hii huleta hewa safi, mvua za kutosha, ardhi yenye rutuba, kijani kibichi na chemchemi zenye maji safi, salama na matamu, na kumfanya kila anayefika ukanda huu atamani kuhamia. Kuna Mjerumani mmoja kwa jina Otto Schüler aliyejiita kwa Kinyakyusa Mwakapalila aliapa kuzikwa Mwakaleli na mkewe Alma Schüler a.k.a Mwabulenge.

Wakati katikati ya jiji la Mbeya pakipambwa kwa milima kusini na kaskazini, unapoingia mji wa Sumbawanga kutokea Tunduma mpakani mwa Tanzania na Zambia, kumepanbwa kwa vilima vya kuvutia njia nzima kila upande. Manisapaa ya Iringa iko juu milimani na imepambwa kwa majabali ya mawe yanayoning’inia juu pasipo kuporomoka. Miji ya Njombe, Mafinga, Makambako na mingineyo katika uwanda wa juu, iko kwenye tambarare baridi kama Ulaya. Mwishoni miaka ya 1990 nilimtembeza mzungu aitwaye Alexander Hipkiss, akashangaa mno na kujiona yuko kwao Uingereza.

Wilaya za Kyela, Ludewa, Nyasa na Mbinga, pamoja na kupambwa na milima ya Livingstone, pia huzunguka ziwa Nyasa lenye samaki aina ya mbasa wenye nyama laini, tamu na kitoweo mujarabu kwa wali au ndizi. Ziwa Rukwa hupakana na mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa, na lina kambale watamu kuliko wote. Kingo zake huzalisha mpunga mzuri kuliko wa Kyela. Sisahau kuwa mkoa wa Rukwa pia hupakana na ziwa Tanganyika.

Maporomoko ya Kalambo mkoani Rukwa hulingnishwa na Victoria Falls nchini Zimbabwe au Niagara Falls nchini Canada. Niipongeze serikali kwa kuweka ngazi za kushuka na kupanda kuyastaajabu maporomoko haya. Mbali na kuwa na maziwa makubwa, mkoani Mbeya kuna maziwa madogo ya volkano (crater lakes) yanayovutia sana kama vile Ngozi katika milima na misitu ya Uporoto, Kyungululu, Ilamba, Itamba, Ikapu, Kisiba na Kingili wilayani Rungwe. Ziwa Ngozi ni la pili kwa ukubwa barani Afrika na maziwa haya hayatoi wala kuingiza maji popote. Ni maajabu na kivutio kikubwa!

Mbuga ya Ruaha ina wanyamapori na ndege wa kila aina. Mbuga ya Kitulo ina uwanda mkubwa wa maua yanayong’ara na kuvutia mno. Maua haya hulinganishwa na nyumbu wa Serengeti na kwahiyo Kitulo huitwa Serengeti ya Maua (Serengeti of flowers). Kimondo kilichoko wilayani Mbozi ni kivutio cha dunia nzima, lakini hakitangazwi ipasavyo. Kuna vivutio vingi mno kiasi ambacho maandishi na simulizi hizi nzuri za mandhari ya Nyanda za Kusini Magharibi hazitoshelezi hadi mtu ajionee mwenyewe. Ulinwengu mzima karibuni Nyanda za Juu Kusini Magharibu – uwanda wa Edeni ya sasa!

Nihitimishe kwa kushauri kamati za utalii za mikoa zijenge hoteli za kisasa na kambi za kupumzikia (campsites) juu ya vilima na milima na ufukweni mwa maziwa yote. Iwepo mitumbwi maalum kwa ajili ya watalii kuvinjari maziwa na mito. Mikoa yote iwe na vituo vya hifadhi ya wanyamapori na utamaduni (Wildlife and Cultural Zoos). Aidha, kila mkoa uwe na tovuti zenye picha mnyato na mgando na maelezo ya vivutio vyetu. Sambamba na hilo, halmashauri zote zijenge miundombinu ya kuvifikia vivutio vyote.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Gwappo Mwakatobe, mchambuzi wa masuala ya kitaifa na kimataifa anayeishi Mwakaleli, Mbeya. Anapatikana kwa anwani za barua pepe: gwandumi@hotmail.com na au gwappomwakatobe@gmail.com

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.