Madiwani 19 wa Chama cha Wananchi (CUF) katika jiji la Dar es Salaam wameungana na Katibu Mkuu wa chama chao, Maalim Seif Sharif Hamad, wakimtuhumu mwenyekiti wa zamani, Ibrahim Lipumba, kwa ‘kutumiliwa’ na ‘kuisaliti’ CUF.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Hoteli ya Peacock mapema leo, madiwani hao walisema CUF ilishiriki uchaguzi wa mwaka 2015, ambao kwawo walipatikana wao kushikilia nafasi walizonazo sasa “bila ya kuwa na mwenyekiti wa chama taifa kutokana na kujiuzulu kwa… Profesa Lipumba kwa utashi wake mwenyewe mbali na kumnasihi sana kusitisha mpango wake huo.”

Madiwani walisema sio tu kwamba walifanya kampeni wakiwa hawana mwenyekiti wa taifa, bali hata makamu mwenyekiti wao, Juma Duni Haji, ambaye alihamia CHADEMA ili kukidhi masharti ya kuwa mgombea mwenza kwa tiketi ya chama hicho kupitia muungano wa UKAWA.

“Tumeshiriki uchaguzi tukiwa kama Mayatima na Wakiwa. Tumeweza kushinda nafasi tulizozipata za kuwakilisha wananchi katika kata zetu katika mazingira magumu bila ya uwepo na ushiriki wa Profesa Lipumba ambaye mbali na kudai kuwa atabaki kuwa mwanachama wa kawaida na kuahidi kushiriki kampeni za majimbo, hakuweza kufanya hivyo hata katika jimbo au kata moja na si pekee kwa Dar es Salaam bali hakushiriki kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015 katika maeneo yote nchini.”

Itakumbukwa kuwa kupitia uchaguzi mkuu huo ambao Profesa Lipumba na baadhi ya washirika wake wa sasa waliukacha, CUF ilifanikiwa kwa mara ya kwanza kupata madiwani kadhaa katika jiji la Dar es Salaam na hivyo kuchukuwa nafasi za unaibu meya katika manispaa za Ubungo, Ilala na hata kwenye jiji hilo kubwa kabisa kiuchumi na kibiashara nchini Tanzania.

“Tangu wakati huo Madiwani wa Manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Wastahiki Manaibu Meya Mheshimiwa Musa Kafana (Mstahiki Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam), Mheshimiwa Ramadhani Kwangaya (Mstahiki Naibu Meya wa Manispaa ya Ubungo) na Mheshimiwa Omary Kumbilamoto (Mstahiki Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala) tukiwa ni viongozi wa Chama kiserikali, tumekuwa kitu kimoja na msimamo wa kuyaangalia maslahi mapana ya ustawi wa Taasisi yetu ya CUF dhidi ya maadui wa ndani na nje ya Chama chetu,” linasema tamko la madiwani hao, ambao waliongozwa na Naibu Meya wa Dar es Salaam, Mussa Kafana.

Madiwani hao walionesha kuutilia mwenendo wa sasa wa Profesa Lipumba ambaye wanasema amebadilika kutoka kiongozi waliyekuwa wakimpenda na kumuheshimu sana hadi kuwa mtu ambaye mikono yake si salama kwa “uhuru kamili wa kupambana na kusimamia mabadiliko makubwa ya kidemokrasia, kisiasa na kiuchumi nchini.”

Kwa mujibu wa tamko lao la pamoja, madiwani wote 19 wa CUF wanaungana na uongozi wa chama chao kwenye kuipinga Wakala wa Usajili (RITA) na maamuzi yake mbele ya Mahakama Kuu kwa kufungua kesi dhidi yake kwa mujibu wa kifungu cha 26 “kwa kukiuka taratibu za Sheria ya Wadhamini (The Trustees’ Incorporation Act Cap. 318) kwa kutojiridhisha juu ya uhalali wa majina ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya CUF yaliyofikishwa kwake na iwapo yamefanywa na kikao halali cha Chama chenye mamlaka hayo kwa mujibu wa Katiba ya Chama,” linasomeka tamko hilo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.