“Kwa hiyo, yale mambo yote mazuri yaliyotajwa kwenye dibaji ya Muswada wa Sheria hii, ikiwa hayatatekelezwa na Serikali au ikiwa Serikali itakwenda kinyume nayo, au ikiwa mtu ataathirika kwa namna moja au nyingine wakati wa utekelezaji wa masuala hayo; basi hakuna shauri lolote linaloweza kufunguliwa kwa minajili ya kufanya madai, na wala hakuna mahakama yoyote itakayoweza kushughulikia jambo hilo. Kwa maneno mengine zile ahadi nzuri zinazotelewa na ule utangulizi ni “cosmetic”, kwa kuwa hakuna haki inayoweza kutolewa ikiwa kuna ukiukwaji wa haki umetokea katika sehemu hiyo.”


HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA, KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MAPITIO NA MAJADILIANO KUHUSU MASHARTI HASI KATIKA MIKATABA INAYOHUSU MALIASILI ZA NCHI WA MWAKA 2017 (THE NATURAL RESOURCES CONTRACTS (REVIEW AND RE-NEGOTIATION OF UNCONSCIOUNABLE TERMS) ACT, 2017

Inatolewa Chini ya Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Bunge, toleo la 2016

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, katika Wizara ya Katiba na Sheria, Mheshimiwa Tundu Lissu (Mb), naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano, kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017.
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena, Serikali imeleta Muswada wa Sheria Bungeni kwa hati ya dharura; ili bunge litunge sheria kwa dharura kurekebisha makosa yaliyoisababishia nchi hasara kubwa kutokana na udhaifu wa sheria za madini, petroli na tasnia ya uzinduaji (TEITI) ambazo zilipitishwa kwa dharura kutokana na kuwasilishwa kwa hati ya dharura.

Mheshimiwa Spika, wahenga wetu walishasema kuwa, sikio la kufa halisikii dawa. Nasema hivi kwa sababu kwa miaka yote ya uhai wa bunge la tisa, bunge la kumi na sasa bunge la kumi na moja, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikemea vikali suala la kuleta miswada ya sheria Bungeni kwa hati ya dharura, hususan miswada ya sheria zenye athari katika maslahi ya kiuchumi kwa taifa; lakini Serikali hii ya CCM imekuwa ikweka pamba masikioni; na matokeo yake Taifa limepata hasara kubwa kutokana na ukaidi huo wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, kitendo kinachofanywa sasa na serikali hii cha kujidai kwamba ina uchungu na rasilimali za nchi hii; na kujidai kuleta harakaharaka miswada hii ili kufanya mapitio ya mikataba yenye masharti hasi inayohusu maliasili za nchi yetu, ni sawa na kula matapishi yake; kwa kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilishatoa rai kwa Serikali kufanya hivyo kwa takriban miaka 15 iliyopita; lakini Serikali ikawa inangangania kwamba mikataba hiyo iko sawa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa miaka yote hiyo niliyotaja, ilikuwa ikiitaka Serikali kuleta mikataba yote inayohusu rasilimali za nchi yetu ambayo Serikali inaingia na wawekezaji ili ijadiliwe na kuridhiwa na Bunge, lakini mara zote Serikali ilikataa kufanya hivyo. 

Mheshimiwa Spika, Serikali haipaswi kujisifu wala kujinasibu kwamba ni ya kizalendo zaidi kwa kuleta muswada huu wa kupitia mikataba yenye masharti hasi sasa; kwa kuwa si jambo jipya. Inatekeleza ushauri uliotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani uliotolewa takriban miaka 15 iliyopita. Hata hivyo Serikali imeanza vibaya kutekeleza ushauri huo.

Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Serikali imeshagutuka kwamba; Taifa lilikuwa linanyonywa kutokana na mikataba mibovu iliyotokana na sheria dhaifu zilizopitishwa kishabiki na kwa harakaharaka; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitegemea kwamba; safari hii Serikali ingetulia na kuandaa muswada wa sheria kwa umakini na kuwashirikisha wadau wote na kwa muda unaotosha; ili kuziba mianya yote ya kinyonyaji iliyokuwepo kutokana na uharakaharaka katika utungaji wa sheria husika. 

Mheshimiwa Spika, kinyume na matarajio hayo; Serikali inarudia makosa yaleyale ambayo yaliisababishia nchi hasara; tunataka tuyarekebishe leo kwa kutumia njia zile zile na akili zilezile. Hatuwezi kupata matokeo tofauti kwa kufanya hivyo!!!!!!. We cant solve problems by using the same kind of thinking we used when we created them (Albert Einstein). Kwa maneno ya mwanafalsafa huyu, ni kwamba kuna haja ya Serikali kubadili mbinu na mfumo mzima wa kushughulikia jambo hili.

Mheshimiwa Spika, itoshe tu kusema kwamba; Serikali inabidi ikiri kwamba ilikosea kuliingiza taifa katika mikataba ya kinyonyaji iliyotokana na sheria dhaifu na hivyo kulisababishia hasara; na kwamba sasa inatakiwa kufanya retreat ili kubaini ilipokosea na kujirekebisha. Na ili Serikali ifanikiwe katika retreat hiyo, haitakiwi kuwa na pupa wala papara.

MAONI YA JUMLA KUHUSU MUSWADA 

Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, sasa naomba nitoe maoni ya jumla kuhusu Muswada ulioko mezani.

Dibaji (Preamble) ya Muswada

Mheshimiwa Spika, tofauti na utaratibu wa kawaida uliozoeleka wa uandishi wa Miswada ya Sheria, Muswada huu una Dibaji, ambayo mwandishi amejitahidi sana kuupamba kwa maneno yanayoashiria utaifa, uzalendo na nguvu ya wananchi katika kumiliki na kulinda rasilimali za nchi; lakini ikumbukwe kwamba ni Serikali hii hii ya CCM iliyoingia mikataba ya kinyonyaji na wawekezaji, wananchi wakafukuzwa katika maeneo yao tena bila fidia na wengine wakauwawa kwa kupigwa risasi hususan katika maeneo yaliyo karibu na migodi ya madini. 

Mheshimiwa Spika, maudhui ya dibaji hii, na vitendo halisi wanavyofanyiwa wananchi walio karibu na mali asili za nchi yetu vinafanana kabisa na ile methali inayosema utamu wa nanasi, ndani kipande cha mtihani. 

Kama kweli Serikali hii ina mapenzi na wananchi kwa kiasi hicho, mbona imewanyima haki na uhuru wao wa kikatiba wa kupata habari kwa kuzuia kurushwa moja kwa moja kwa mijadala ya Bunge lao; na kuwawekea sheria ngumu na kandamizi ya makosa ya kimtandao inayowanyima uhuru wa habari?

Kama kweli Serikali hii ina mapenzi na wananchi kwa kiasi hicho; mbona imewanyima haki yao ya kikatiba ya kukusanyika, na kujiunga na vikundi au vyama vya siasa kwa kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa?

Kama kweli Seriali hii ina mapenzi na wananchi kwa kiasi hicho; mbona inawazuia wananchi wasiuze mazao yao ya kilimo nje ya nchi ili wapate faida?

Kama kweli Serikali hii ina mapenzi na wananchi kwa kiasi hicho, mbona wananchi wanaoishi katika maeneo ya machimbo ya madini wanaendelea kuwa masikini, kunyanyaswa na kuuwawa mpaka leo?

Mheshimiwa Spika, yapo mambo mengi mabaya wanayofanyiwa wananchi, na Serikali hii inaona na wala haichukui hatua. Hivyo kuja kuwahadaa wananchi kwamba wao ndio wenye mamlaka kwa kutumia maneno matamu ya utangulizi na wakati kinachofanyika ni kinyume na maneno hayo, haikubaliki.

Matumizi ya Sheria Inayopendekezwa

Mheshimiwa Spika, ibara ya pili ya Muswada wa Sheria inayopendekezwa inasema kwamba; sheria hiyo itatumika Tanzania Bara, bila kuathiri mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar juu ya umiliki na udhibiti wa rasilimali zake za taifa.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba iliyopo sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; masuala ya mafuta na gesi ni miongoni mwa mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa katika nyongeza ya kwanza ya Katiba. Pamoja na takwa hili la kikatiba; Serikali hii ya CCM ikishirikiana wabunge wake; ilitunga sheria ya Gesi na Petroli ya mwaka 2015 inayoipa Zanzibar mamlaka juu ya mafuta na gesi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haipingi Zanzibar kuwa na mamlaka juu ya rasilimali zake; isipokuwa mihilimili ya Bunge na Serikali iwe makini vya kutosha ili kuepuka kutunga sheria zinazokinzana na Katiba. 

Mahakama Kufungwa Mikono katika Kuamua Mashauri Yanayotokana na Sheria Inayopendekezwa

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mapungufu makubwa ya Muswada wa Sheria inayopendekezwa ni kwamba inalenga kuifunga mahakama mikono isiweze kushughulikia shauri la mtu atakayeonewa au kutendewa visivyo na sheria hii. Dibaji ya Sheria hii imefanya rejea ya ibara za 8 na 9 zilizoainishwa katika Sehemu ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ambazo kwa mujibu wa Katiba hiyo, haviwezi kutiliwa nguvu na mahakama yoyote nchini.

Mheshimiwa Spika, ibara ya 7(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kwamba: Masharti ya sehemu hii (yaani sehemu ya pili ya Katiba) hayatatiliwa nguvu ya kisheria na mahakama yoyote. Mahakama yoyote nchini haitakuwa na uwezo wa kuamua juu ya usuala kama kutenda au kukosa kutenda jambo kwa mtu au mahakama yoyote, au kama sheria au hukumu yoyote inaambatana na masharti ya Sehemu ya Sura hii. 

Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika, yale mambo yote mazuri yaliyotajwa kwenye dibaji ya Muswada wa Sheria hii, ikiwa hayatatekelezwa na Serikali au ikiwa Serikali itakwenda kinyume nayo, au ikiwa mtu ataathirika kwa namna moja au nyingine wakati wa utekelezaji wa masuala hayo; basi hakuna shauri lolote linaloweza kufunguliwa kwa minajili ya kufanya madai, na wala hakuna mahakama yoyote itakayoweza kushughulikia jambo hilo. Kwa maneno mengine zile ahadi nzuri zinazotelewa na ule utangulizi ni “cosmetic”, kwa kuwa hakuna haki inayoweza kutolewa ikiwa kuna ukiukwaji wa haki umetokea katika sehemu hiyo.

Marekebisho ya Sheria Mbalimbali kwa Kuzingatia Maudhui ya Muswada wa Sheria Inayopendekezwa

Mheshimiwa Spika, Dhana ya Utajiri na Rasilimali za Asili ni pana sana, na kwa vyovyote vile haiwezi kuhusishwa na madini au mafuta na gesi peke yake. Kwa mujibu wa tafsiri iliyotolewa na muswada huu, Rasilimali za Asili ni vitu vyote vinavyotokea kiasili, kuanzia ardhini, majini na hata angani vyenye thamani ya kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na upana wa dhana hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani ilitegemea kwamba Serikali ingeleta Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ili sheria zote zinazohusu maliasili na utajiri wa asili zifanyiwe marekebisho ili ziendane na maudhui ya Sheria hii inayopendekezwa. Lakini cha ajabu ni kwamba Serikali imeleta Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba 4 ukiwa na marekebisho ya sheria mbili tu zinazohusu utajiri na maliasili za nchi – yaani Sheria ya Madini na Petroli, pamoja na sheria zingine za mapato na kodi. Lakini sheria nyingine zinazohusika katika maeneo ya utajiri na rasilimali za asili kama vile wanyamapori, utalii, ardhi, uvuvi, uhifadhi wa mazingira nk. hazijaletwa kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba ili sheria hii inayopendekezwa iwe na tija, ni lazima sheria nyingine zinazohusika na masuala hayo zifanyiwe marekebisho

Mamlaka ya Bunge katika Kupitia Mikataba

Mheshimiwa Spika, Katika Mikataba ya Rasilimali za Nchi, ukitazama kwa kwa juu juu, inaonekana kama ina nia nzuri; lakini haiweki mfumo madhubuti wa kujadiliana mikataba hiyo. Aidha, Bunge linapewa madaraka pale tu mikataba hiyo inapokuwa imejadiliwa na kuanza kutelezwa bila kuzungumzia mikataba mipya inayojadiliwa. 

Aidha, sheria haiagizi kuwa mikataba yote iwasilishwe Bungeni kwa ajili ya kuridhiwa kama itakiwavyo na Ibara 63(3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania inayoagiza kuwa mikataba yote isainiwayo na serikali lazima iwasilishwe na kuridhiwa na Bunge. 

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 4 cha Muswada huu kinasema kwamba; Bunge linaweza kupitia upya mikataba ya rasilimali za nchi kuhusu Masharti hasi katika Mikataba inayohusu rasilimali hizo. Hata hivyo, ukisoma kwa makini ni kuwa, bado serikali itakuwa na mamlaka ya kuingia mikataba ya uvunaji wa rasilimali isipokuwa Bunge linaweza kuipitia upya mikataba hiyo baada ya kuingiwa na serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba, Serikali isiingie mkataba wowote unaohusu rasilimali asili za nchi mpaka mikataba hiyo itakapojadiliwa na kuridhiwa na Bunge.

Haki ya Wananchi Kushirikishwa katika Uamuzi juu ya Rasilimali za Nchi
Mheshimiwa Spika, Muswada huu hauna kifungu cha kinachotoa haki kwa wananchi ya kushirikishwa, kuhusishwa na kutaarifiwa kuhusu maamuzi yote yanayohusu utafutaji au uvunaji wa rasilimali za umma. 

Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kwamba licha ya Bunge kuwa na nafasi ya kujadili mikataba hiyo; lakini pia wananchi wa eneo lenye rasiliali hizo washirikishwe kupitia serikali zao za mitaa, vijiji na vitongoji. 

Aidha, Kamati ya Bunge itakayokuwa inashughulikia masuala hayo, ikusanye maoni kutoka kwa wananchi hao, ili maoni hayo yalisaidie Bunge katika kufanya mapitio ya Mikataba hiyo.

Ukosefu wa Vyombo au Taasisi za Kufanya Majadiliano ya Mitakaba Hasi

Mheshimiwa Spika, Muswada hauzungumzii au hauundi chombo au taasisi yoyote ile ya serikali ambayo itahusika na mazungumzo ya mikataba hasi. Huu ni usahaulifu wa ajabu na kwa kweli ni kutokana na kuandikwa kwa miswada hii kwa haraka. Ili kuweza kuwa na majadiliano mazuri ni lazima kuwepo kwa Timu Bobezi ya Kitaalamu kuweza kujadiliana na Kampuni za uwekezaji katika maliasili za nchi yetu. 

Hivyo Muswada huu lazima uwe na kifungu kinachounda Timu Bobezi ambayo inajumuisha watu wa kada mbalimbali wakiwemo wanauchumi, wanasheria, watoza kodi, wahasibu, wanajiolojia, wanamazingira, wahandisi, wanasayansi (ikiwemo wanahisabati, wafizikia na wakemia), watakwimu na wataalamu wa TEHAMA. 

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kwamba; wataalamu watakaoiunda Timu hii wawe watu ambao ni wabobezi na ambao mapenzi yao kwa nchi yetu hayatiliwi mashaka. Watoke ndani na nje ya serikali na pale ambapo mtaalamu wa kada fulani hayupo nchini basi atafutwe kutoka nje. Mfumo huu umetumiwa kwa mafanikio makubwa na Kamati ya Madini ya Botswana.

Kutokuwepo kwa Vifungu vya Adhabu

Mheshimiwa Spika, Muswada huu unalipa Bunge madaraka ya kutoa maazimio juu ya mikataba yenye mashariti hasi; lakini hausemi ni adhabu ipi Bunge litatoa kwa Kiongozi au Ofisa wa Serikali anayekiuka azimio la Bunge. Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa sheria itamke kwa uwazi kabisa kuwa Waziri au Mtendaji yeyote yule wa serikali anayeshindwa kutekeleza azimio la Bunge anatenda kosa la jinai na adhabu yake ni kushitakiwa mahakamani kwa kosa hilo licha ya adhabu ya kinidhamu. 

Mheshimiwa Spika, Licha ya Sheria kutoa fursa ya majadiliano ya upitiaji wa masharti hasi sheria inaonekana kuwa kandamizi kwani inalazimisha matokeo ya majadiliano. Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa pale kunapotokea kutokuelewana basi suala hili lipelekwe Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara. Aidha, sheria isifunge orodha ya vifungu vya mashariti hasi na itoe nafasi kuwa jambo lolote lile ambalo kutokana na mabadiliko ya sheria au mazingira ya utendaji basi sharti hasi linapojitokeza nalo liweze kuchagiza majadiliano mapya. 

HITIMISHO 

Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia hotuba yangu kwa kusisitiza kwamba nchi yetu inaangamia kutokana na mifumo mibovu ya kiutawala. Mifumo yetu ingekuwa thabiti kusingekuwa na tabia hii ya kuleta miswada ya sheria kwa hati ya dharura hata kwa mambo yasiyo ya dharura. 

Hati za dharura hutolewa iwapo kweli kuna jambo la dharura kwa mfano nchi iko vitani; au kuna hali ya hatari katika nchi au kuna mlipuko wa gonjwa hatari, n.k.

Mheshimiwa Spika, ungekuja Muswada wa Sheria ya kudhibiti mambo yanayoendelea huko Rufiji na Kibiti kwa hati ya dharura tusingeshangaa na tungeunga mkono; lakini kuleta miswada ya sheria ya mambo makubwa yanayohusu utajiri na rasilimali za nchi hati za dharura ni matumizi mabaya ya hati hizo; na Mheshimiwa Spika, Kambi Rasi ya Upinzani Bungeni inakutegemea upige marufuku tabia hiyo.

Mheshimiwa Spika, Nimesisitiza kwamba; ili taifa hili liondoke katika shimo la uharibifu, ni lazima kuanzia sasa tuamini katika mifumo ya kitaasisi kuliko kuamini katika mtu au watu. Ukiangalia miswada ya sheria iliyoletwa mbele ya Bunge lako utagundua kwamba kinachotafutwa ni utukufu wa mtu (Glorification of a person) na sio utukufu wa taasisi. Hii ni hatari kubwa sana kwa kuwa, mtu huyo anayetafutiwa utukufu katika sheria hizi ikiwa hayupo, na akitokea mwingine ambaye hapendi utukufu huo; maana yake ni kwamba; sheria hizi zitakuwa redundant na nchi itaparaganyika kwa kuwa, kutakuwa hakuna mifumo ya kitaasisi iliyojengwa kusimamia nchi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.

John Wegesa Heche (Mb)

KNY: MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, KATIKA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

3 Julai, 2017

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.