“UMEKUJA kufanya nini huku?” aliniuliza kwa hasira Mpalestina wa makamo aliyekuwa dereva wa shirika moja la Umoja wa Mataifa mjini Jerusalem ya Mashariki.
“Watu kama nyiye mkija huku ni tatizo,” aliongeza.

Sikuwa na hila.  Azma yangu ilikuwa kulizuru eneo la Gaza mara baada ya eneo hilo kushambuliwa na majeshi ya Israel kuanzia Desemba 27, 2008 hadi Januari 18, 2009 .  Nilikuwa Mkuu wa Chumba cha Habari na Mhariri Mkuu wa Mashariki ya Kati na Asia wa Shirika la Habari la IRIN, ambalo wakati huo lilikuwa chini ya Umoja wa Mataifa.

Nikiwa na ofisi yangu Dubai, nilikuwa na dhamana ya ripoti kutoka nchi kadhaa za Mashariki ya Kati (Misri, Iraq, Iran, Israel, Palestina, Syria, Lebanon, Jordan na Yemen), na mbili za Asia (Afghanistan na Pakistan).  Zote hizo zilikuwa “nchi zangu”, milki yangu kama tulivyokuwa tukisema ofisini. 

Katika kila moja ya nchi hizo nilikuwa na mwandishi au waandishi waliokuwa wakituletea ripoti kila siku. Mara kwa mara ilinilazimu kuwatembelea ili kuwapa moyo pamoja na miongozo ya uandishi na kuwaelekeza kuhusu aina ya ripoti tulizotarajia kutoka kwao.

Ziara hizo zilinipa fursa ya kuziona hali halisi zilivyokuwa katika nchi hizo. Niliweza pia kuyatambua mazingira magumu ya kufanyia kazi ya waandishi wetu. Kadhalika, ilikuwa muhimu waandishi wetu wafahamu kwamba hatuwajasahau.

Niliamua kwenda Gaza mara tu baada ya kupatikana mapatano ya Israel ya kusita kulishambulia eneo hilo. Mashambulizi hayo yasiyodumu hata mwezi yaliwaua Wapalestina wasiopungua 1,400, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Pia mashambulizi hayo yaliligeuza eneo la Gaza liwe vifusi, magofu na ardhi iliyojaa majeraha ya aina kwa aina.  Makovu ya majeraha hayo  yakionekana wazi kwenye kuta za hospitali kuu ya Gaza, Al Shifaa, kwenye jengo la makao makuu ya polisi

Kulikuwa njia mbili za kunifikisha Gaza; ama kutokea upande wa Misri au kutokea Israel. Mpaka wa Misri na Gaza ulikuwa umefungwa na kwa hivyo  kama nilivyogusia sikuwa na hila ila kupitia mpaka wa Israel wa Erez.  Njia hiyo ilinilazimu niwe Israel na ilinipa fursa mbili nyingine. Kwanza, ya kukutana pia na mwandishi wetu wa Israel aliyekuwa akituandikia akiwa Tel Aviv na pili, ya kuuzuru mji wa Jerusalem na kuswali katika Msikiti wa Bait al Muqaddas, msikiti wa tatu kwa umuhimu. 

Jerusalem ni mji wa kale kabisa duniani na tangu 1967 umekuwa wenye utata mkubwa kimataifa.  Leo Jerusalem ni moja ya miiba inayochoma vikali sana katika mzozo baina ya Wapalestina na Israel.  Waisraeli walipopigana na Waarabu 1948 waliiteka sehemu ya Magharibi ya mji huo. Jordan, kwa upande wake, iliiteka Jerusalem ya Mashariki, ikiwa pamoja na Mji wa Kale.

Mji mmoja uligawika pande mbili, upande mmoja ukiwa chini ya Israel na mwingine chini ya Jordan.  Hali iliendelea kuwa hivyo hadi Juni 1967 pale Israel ilipoiteka Jerusalem ya Mashariki baada ya kuzivamia nchi za Misri, Syria na Jordan.

Yule dereva wa Kipalestina alikuwa na sababu za kunikasirikia tulipokutana Jerusalem ya Mashariki.  Aliniona kama mtu aliyekwenda kwao bila ya kujali uonevu wanaofanyiwa Wapalestina katika ardhi zao na Israel.

Ni uonevu huo uliowashawishi viongozi wa Kiafrika, wakiwa pamoja na Kwame Nkrumah wa Ghana na Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania waiangalie Israel kwa jicho lilelile kama walivyokuwa wakiwaangalia wakoloni waliokuwa wamezikalia kwa nguvu ardhi ya Waafrika na kuwatesa Waafrika.  Viongozi hao walizisemesha nafsi zao na wakaona kwamba watakuwa wanafiki wakiendelea kuwa na mahusiano na Israel.

Nchi za Kiafrika, moja baada ya moja, zikaanza kuvunja mahusiano yao ya kiserikali na Israel tangu baada ya 1967.  Msimamo huo siku hizi umepata pigo kubwa kwa kuwa mataifa ya Kiafrika, moja baada ya moja, yameanza kuyarudisha mahusiano yao na Israel.  Mengine yameyakuza zaidi.

Hii ni hadithi ambayo hatuwezi kuisimulia katika makala moja.  Itatubidi tuirejelee tena, mara kwa mara, kuonesha mkakati wa Israel ulivyo na jinsi viongozi wetu wa Kiafrika wanavyoturejesha nyuma na kutufanya tusahau maadili, tuusahau utu na tuiisahau misimamo yetu iliyokuwa imeipa heshima bara la Afrika katika medani ya siasa za kimataifa.

Hii si hadithi ya nchi moja ya Kiafrika.  Ni hadithi inayolihusu bara zima la Afrika.  Ni hadithi iliyokaa kama mchuzi wenye viungo vingi.  Miongoni mwa viungo hivyo ni hongo wanazopewa viongozi wetu, njama za kuupora utajiri wa Afrika, madini adimu, visingizio vya mambo ya usalama na vita dhidi ya ugaidi wa kimataifa. 

Pamoja na yote hayo katikati ya mchuzi huo kuna viongozi wetu walio tayari kutumiliwa. Na la kusikitisha zaidi ni kwamba wanatumiliwa na walewale ambao kwa miaka na miaka wamekuwa wakilidhalilisha bara la Afrika na watu wake.

Wenye kuiendesha dola la Israel wanahamaki unaposema kwamba nchi hiyo imekuwa kama ilivyokuwa Afrika Kusini siku za utawala wa kibaguzi wa makaburu.  Lakini huo ndio ukweli kwani hivyo ndivyo Israel ya leo ilivyo.

Mwaka huu wa 2017 ni mwaka wenye umuhimu mkubwa katika historia ya Palestina. Novemba itatimu miaka mia tangu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza wa siku hizo,  Arthur James Balfour, alipokaa kitako akamwandikia barua Lord Rothschild, mmoja wa viongozi wa Shirikisho la Wayahudi la Uingereza na Ireland. 

Barua hiyo ina ibara isemayo kwamba serikali ya Uingereza inapendelea Wayahudi wawe na nchi yao katika ardhi ya Palestina na itajitahidi iwezavyo kufanikisha lengo hilo.  Ibara hiyo inajulikana kama  “Tangazo la Balfour” na ndio mzizi wa fitina na mzozo baina ya Wapalestina na Israel tangu siku hizo hadi leo.

Novemba mwaka huu itatimu pia miaka 70 tangu Umoja wa Mataifa ulipotangaza Mpango wa Kuigawa Palestina na kuwagaia sehemu Wayahudi ili wawe na nchi yao, Israel, kama alivyoahidi Balfour. Waarabu walilalama na kupinga lakini wakubwa wa dunia walitaka na taifa jipya la Israel likaundwa Mei 14, 1948.

Mwaka huu imetimu miaka 50 tangu Israel iyatwae na kuyakalia kinyume na sheria za kimataifa maeneo ya Wapalestina ya Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, Ukanda wa Gaza na Jerusalem ya Mashariki.  Kadhalika, mwaka huu inatimu miaka kumi tangu Waisraeli walizingire eneo la Gaza.

 Hiyo ndiyo mizizi ya Israel ya leo.  Ukiifuata itakufikisha kwenye mzizi mkubwa wa 1948 pale vijiji vya Wapalestina visivyopungua 400 vilipovamiwa na majeshi ya Israel, majeshi ambayo yalianza kwa kuwa vikundi vya magaidi.  Magaidi wa siku hizo ndio baadaye walioliunda taifa la Israel na juu ya misingi ya unyang’anyi, mateso, uporwaji wa haki za Wapalestina. 

Magaidi hao ndio waliopigana na Waingereza na waliowashambulia Wapalestina na kuwatoa kutoka nyumba zao, mashamba yao, vijiji vyao na miji yao.  Ndio waliowafanya Wapalestina waliokuwa na chao waondokee patupu na wawe wakimbizi waliotawanyika kila pembe ya dunia. 

Tuunganishe historia kidogo kwa kukumbusha kwamba hali kama hiyo imewafika maelfu kwa maelfu ya Wazanzibari waliolazimika kuhama nchi yao, ama kwa lazima au kwa hiyari yao, baada ya Mapinduzi ya 1964.  Kuna wale ambao serikali iliwatia melini na ikawafukuza rasmi nchini; kuna waliolazimika kuikimbia nchi kwa sababu kulikuwa ku moto hakukaliki tena; kuna waliokuwa wakisoma nje wakaamua wasirudi kwani habari kutoka kwao ziliwasukuma wasirudi.

Matokeo ya yote hayo ni kwamba hii leo kuna Wazanzibari walio raia wa nchi mbalimbali.  Wapalestina nao ni hivyohivyo.  Wametawanyika sehemu mbalimbali za dunia.

Wapalestina wanalizwa na mwaka wa 1948; Wazanzibari wanalizwa na 1964.  Aprili 1948, zaidi ya wanavijiji mia wa Kipalestina waliuliwa na wanamgambo wa Kizayuni katika kijiji cha Deir Yassin. Wapalestina wanauita mwaka huo wa 1948 kuwa ni mwaka wa “Nakba”, au maafa.

Kwa Wazanzibari “nakba” yao ilikuwa 1964, mwaka wa Mapinduzi ya Januari 12, yaliyoipindua serikali iliyokuwa imekabidhiwa uhuru na Waingereza Desemba 10, 1963.  Na kuanzia Aprili 26, mwaka huohuo ndipo Zanzibar ilipoupoteza uhuru wake ilipoungana na Tanganyika na kuunda Tanzania.

Huu si wakati wa kuyafanya yawe mema mahusiano baina ya Israel na nchi za Kiafrika.  Wakati wake haukufika bado. Israel itahitaji kwanza iwe na uadilifu, sifa ambayo kwa sasa haina.  Israel inaikosa sifa hiyo kwa sababu ya madhila na mateso inayowafanyia Wapalestina kila uchao.  

Waafrika wanaokimbilia Israel nao pia wanajikuta wanakabiliwa na ubaguzi, mateso na madhila ya kila aina. Israel pia ni mzizi wa fitina kubwa iliyopo sasa Mashariki ya Kati, inayozigongesha vichwa nchi mbalimbali za eneo hilo na inayopalilia chuki za kimadhehebu baina ya Masunni na Mashi‘a.  Sumu ya chuki hiyo inautishia uzima wa umma wa Kiislamu katika bara la Afrika pia.

Kuna safari ya kufanywa kabla ya kuyarekebisha mahusiano baina ya Israel na Afrika.  Ni safari ndefu ya kuweka msingi wa ushirikiano baina ya mataifa ya Kiafrika na Israel.  Ushirikiano huo haustahiki uanze sasa.  Huu si wakati wake.  Wakati wake ni pale tu Israel itapoacha kuzikalia ardhi za Wapalestina na pale Palestine itapokuwa imejikomboa na kuupata uhuru wake.  Ukombozi wa Palestine ndio uwe ufunguo wa kuyafungua mahusiano mapya baina ya nchi za Kiafrika na Israel. 

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ahmed Rajab na kuchapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Raia Mwema la tarehe 28 Juni 2017. 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.