Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa, amemtaka Rais John Magufuli kuwaachia huru masheikh wa Uamsho wanaoshikiliwa kwa zaidi ya miaka minne sasa.

Akizungumza katika futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga, Mhita Waitara, Lowassa amemuomba Rais Magufuli kuwaachia masheikh hao, huku akisema ni jambo la aibu kwa nchi kama Tanzania kuwashikilia viongozi wa dini bila kuwafikisha mahakamani.

“Nilipokuwa katika kampeni kote nilikozunguka niliahidi kuwa nikiingia tu madarakani nitawaachia masheikh hawa na pia niliahidi kuunda tume ya kuchunguza suala la makini. Sasa juzi Bwana Mkubwa alipotangaza kuunda Tume, nikasema naam, umetekeleza mambo ya UKAWA. Ningeomba vile vile atekeleze na hilo masheikh hawa watoke.”

“Nchi gani ina uhuru wa miaka zaidi ya 50. Watu wao, tena waumini wa dini, wanawekwa ndani tena bila kesi..bila kesi kwa sababu ya tofauti za kiitikadi? Tuwaombe masheikh wale watoke..ni aibu kwa nchi yetu..ni aibu kwetu ni aibu kwa serikali yetu.”

Aidha Lowassa amewataka Waislam kuwa ngangari katika kudai haki kwa masheikh hao akisema wamekuwa baridi sana na akamkumbuka aliyekuwa sheikh wa msikiti wa Mtoro jijini Dar es Salaam, Marehemu Sheikh Kassim Bin Juma.

“Kuna nini? Mbona Waislam niliokuwa nawajua wakati wa awamu ya Mzee Mkapa na Mzee Mwinyi..mbona si wao!!? Kulikuwa kuna msikiti pale Dar es Salaam alaam kila wakienda kusali Ijumaa serikali inaweka masikio leo inaskiliza kutoka nini..alikuwa Kassim bin Jumaa nadhani..alikuwa akisema kila mtu anasikia Dar es Salaam yote inasikia leo msikiti ule umetoa maneno. Nikasema mbona siku hizi mmelegea! Msiwe baridi sana katika kuwaombea masheikh hawa watoke. Zungumzeni mfanye nini. Ni aibu masheikh hawa kuendelea kuwa kizuizini”, alisema Lowassa kwa hisia kali.

Aidha Lowassa amewataka Watanzania waendelee kudumisha amani na utulivu wa nchi yao. “Ramadhan ni kipindi ambacho mja hutulia na kumcha mola wake..nimefikiri na mimi kwa undani nikasema hivi isingekuwa busara ikawepo siku moja ndani ya nchi kila Mtanzania akatafakari juu ya amani na utulivu wa nchi yetu..tujiulize hii ndiyo amani aliyotuachia baba wa taifa? Huu ndiyo utulivu aliyoutaka au kuna nini? Nasema haya kwa sababu hivi sasa kuna chuki imeanza kuingia katika jamii na hii inaletwa na vyama vya siasa. Hii ni mbaya sana,” ameonya Lowassa.

Wakati huo huo, katika salamu zake za sikukuu ya Eid-ul-Fitr kwa Watanzania, Lowassa amewataka Watanzania kuwakataa viongozi wanaoeneza chuki na ubaguzi miongoni wa Watanzania.

Amesema kwa hali inayoendela nchini hivi sasa, viongozi wa kisiasa ni muhimu kuchunga ndimi na matendo yao kwani wanaelekea kulitumbukiza taifa katika mtifuano mkubwa.

“Tuwakatae kwa nguvu zote viongozi hawa wenye kutumia vibaya madaraka yao na kukandamiza haki za kidemokrasia za wenzao,” amesema.

Imeandikwa na Richard Tambwe Hiza katika ukurasa wake wa Facebook.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.