Chama cha upinzani nchini Tanzania, ACT-Wazalendo, kimekuwa cha kwanza katika taifa hilo kubwa kabisa Afrika Mashariki kutoa msimamo wake juu ya vikwazo vya mataifa sita ya Kiarabu dhidi ya Qatar, kikitaka viondoshwe mara moja tena bila masharti yoyote.

Msimamo huo umo kwenye tamko la Kamati ya Kimataifa ya chama hicho chini ya Venance Msebo, ambapo inavitaja vikwazo hivyo kuwa ni “vikali na visivyo vya kiutu.”

“Licha ya kwamba tunayalaani vikali makundi ya kigaidi duniani na waungaji mkono wao wote, tunatiwa wasiwasi pia na vikwazo vya kikatili na visivyo vya kiutu ilivyowekewa Qatar bila kujuulishwa au kuzungumza nayo kabla,” inasema taarifa hiyo ya ACT.

Mataifa sita ya Kiarabu yakiongozwa na Saudi Arabia yanaendeleza kile yanachokiita vikwazo vya ardhini, baharini na angani dhidi ya taifa hilo dogo la Ghuba takribani kwa mwezi mzima sasa. Awali walitoa madai yasiyofanana kwenye vikwazo vyao hivyo, lakini baada ya shinikizo la Marekani hapo jana wakachapisha masharti 13 ya kutekelezwa na Qatar ndani ya siku 10, likiwemo la kukifunga kituo cha televisheni cha al-Jazeera na kukata mahusiano yote na Iran.

“Tukiwa tunatambua umuhimu wa kuishi pamoja kwa amani na dhima ya Dola la Qatar katika vita dhidi ya ugaidi, ACT Wazalendo tunatoa wito kwa pande zote husika kuanzisha majadiliano yasiyo masharti yoyote kwa nia ya kupata suluhisho muafaka,” inasema taarifa hiyo.

Pamoja na hayo, chama hicho kimeitaka pia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kuwa vikwazo hivyo “haramu na vya upande mmoja” vinakomeshwa haraka.”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.