Kamisheni ya Kuondosha Ufisadi nchini Indonesia (KPK) imetangaza kwamba ripoti zinazohusiana na zawadi za Eid zilizokubaliwa na maafisa wa serikali na vyombo vya dola zimeongezeka. 

Mkurugenzi wa KPK, Giri Suprapdiono, amesema kuwa ongezeko hilo limeanza kutokea kwa miaka miwili sasa. 
Kwa mujibu wa Giri, ripoti 35 zinazohusika na zawadi za siku ya Eid, ambazo zaidi huwa vyakula, vinywaji, vyombo vya jikoni, vito vya thamani na samani zenye thamani ya Rupia milioni 35.8 zilirikodiwa kwa mwaka 2015. 

Lakini mwaka jana 2016, idadi hiyo ilipanda zaidi ya mara kumi kwa ripoti 371 za takrima ambayo ni kinyume na maadili. Thamani ya vitu vilivyotolewa zawadi ilifikia Rupia bilioni 1.1.

“Mara nyingi hivi ni vitu ambavyo watu wameviripoti, kunaweza kuwako wengi ambao bado hawajatambua umuhimu wa kuripoti zawadi wanazopokea,” amesema Giri hivi leo (Ijumaa, 23 Juni). 

Indonesia ina sheria maalum ya kuwazuia maafisa wa serikali na vyombo vya dola kupokea zawadi isipokuwa katika mazingira maalum. Kifungu 12B (1) cha Sheria Nambari 31 iliyopitishwa mwaka 1999 kinaeleza kwamba zawadi yoyote inayotolewa kwa maafisa hao inatambuliwa kuwa ni rushwa ikiwa inahusiana na nafasi yake na inakinzana na wajibu na majukumu yake. 

“Zawadi yoyote lazima ama ikataliwe au iripotiwe,” anasema Mwenyekiti wa KPK, Agus Rahardjo, akiongeza kuwa zawadi inayopokelewa na afisa wa serikali huchukuliwa kuwa ni rushwa endapo haitaripotiwa ndani ya siku 30 tangu kutolewa kwake. 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.