WIKI iliyopita, Serikali ilitangaza kulifungia gazeti la MAWIO kwa muda wa miaka miwili kwa maelezo ya kukiuka agizo la kutowahusisha marais wastaafu wa Tanzania na sakata la usafirishaji wa makinikia nje ya nchi.

Jambo la kwanza ambalo napenda kulisema ni kwamba mimi si muumini wa dhana ya serikali kufungia magazeti au chombo chochote cha habari. Mimi ni miongoni mwa wanaoamini kwamba uhuru wa kujieleza na kutoa taarifa ni mkuu  kuliko mamlaka ya kufungia uhuru huo.

Katika nyakati tunazopita sasa, uhafidhina ni mojawapo ya changamoto kubwa za kizazi hiki. Ndiyo sababu tumeshuhudia watu kama Donald Trump kuchaguliwa Rais nchini Marekani na Waingereza kukubaliana na Brexit.

Katikati ya uhafidhina ni mgawanyiko wa nini hasa maana ya SISI na WAO. Tabia moja kubwa zaidi ya uhafidhina ni kugawa jamii au taifa katika makundi makubwa mawili ya walio pamoja na wasio pamoja nao. Na hata kama hawa akina SISI ni wachache, wanaweza kufanya ikaonekana wako wengi kuliko hata WAO.

Katika kilele cha uhafidhina, kunakuwa na maneno kama vile wasiokubaliana na hili si wazalendo na wanaokubaliana na hili ndiyo wazalendo. Kwamba kuwa mzalendo au mzalendo kunategemea na nini ambacho wahafidhina wanataka katika wakati husika. Ukiwa pamoja nao, wewe ni mzalendo, mkitofautiana, wewe si mzalendo. Lakini hii haijawahi kusaidia nchi yoyote, popote.

Jambo la kwanza ambalo wenye nchi wanapaswa kulishughulikia ni kwenye kujenga utaifa kwa watu wake. Njia ya haraka ya kufikia hili ni kwa kutumia vyombo vya habari na taasisi zake.

Kwa mfano, mimi sielewi kwanini serikali hadi sasa haijafikiria mpango wa kuwapa wahariri wa vyombo vyake vikubwa vya habari na mawasiliano hapa nchini mafunzo maalumu kuhusu masuala ya ulinzi na usalama kupitia Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kilichopo Kunduchi jijini Dar es Salaam.

Kwa kufanya hivi, wahariri watafahamu mengi kuhusu masuala ya ulinzi na usalama kidunia na pia kwa taifa lao. Sehemu ya mafunzo inaweza kuwa kuhusu masuala ya maslahi ya taifa; kwamba ni yapi na ni namna gani vyombo vya habari vinaweza kuhakikisha yanalindwa.

Haiwezekani katika nchi kama yetu, kuachiwe wachache wa kuamua yapi ni maslahi ya taifa letu kwenye siasa, uchumi, utamaduni na kijamii kwa ujumla. Kama hayako kwenye Katiba ya Nchi, ni muhimu yakatafutiwa mitala kwenye shule au vyuo ili watu wayasome na kuyaelewa.

Kama kundi moja katika jamii yetu, watawala, ndiyo watapewa fursa ya kuamua yapi ni maslahi ya taifa na ni namna gani yatalindwa, hayo yatakuwa ni makosa. La muhimu ambalo wahusika wanatakiwa kulifahamu ni kwamba kwenye utawala kuna mabadilishano  – kwamba aliye madarakani leo, kesho anaweza kujikuta uraiani.

Sababu zilezile alizozitumia kuwashughulikia wapinzani wake, ndiyo sababu hizohizo zitatumika kumshughulikia yeye wakati mwingine atakapokuwa kwenye nafasi ileile. Wengine huwa watesi wa wenzao kwa vile labda wanajua wanaumwa na maradhi yao yamewahakikishia kuwa hawataishi muda mrefu duniani au tu wamezeeka na wanaweza kuondoka duniani wakati wowote na hivyo hawajali.

Wanasahau kwamba watakapoondoka hapa duniani, watawaacha watoto na wajukuu na kama wao wenyewe ni wagumba, bado watakuwa na dada na kaka, baba na mama au ndugu, jamaa na marafiki watakaoendelea kubaki hapa.

Nao, kwa sababu moja au nyingine, watashughulikiwa kwa vigezo vilevile ambavyo mpendwa wao alivitumia kuumiza wengine.

Njia bora zaidi ya kujenga taifa moja ni kuhakikisha wale wenye wajibu wa kulijenga wanafahamu kuanzia msingi. Chukua kwanza wahariri wa vyombo vyote vya habari vya kimkakati kwenye mafunzo maalumu. Na halafu chukua wakuu wa mashirika ya umma na taasisi za serikali ili wawe kitu kimoja.

Hawa watahakikisha maslahi ya taifa yanalindwa katika sehemu za kazi. Wengine watapromoti maslahi hayo kupitia vyombo vya habari walivyonavyo na wengine wataanza kufundishwa kwenye mitaala yao shuleni katika ngazi za chini kabisa.

Kwa bahati nzuri, tayari serikali yetu ina NDC na hivyo kinachohitajika kwa sasa ni dhamira tu ya kuhakikisha hilo linafanikiwa. Kama sote hatuko katika mstari mmoja, kufungiana huku hakutakwisha na mbaya zaidi, tutatengeneza mazingira ya kufungiana na kushughulikiana kwa muda mrefu zaidi kutoka sasa.

Uzalendo wa kihafidhina siku zote ni mbaya kwa sababu nguzo yake kuu ni ulaghai na ubaguzi. Hakuna taifa litakalobaki salama wakati msingi wa ujenzi wake ni vita ya SISI dhidi ya WAO.

Kama tunajenga taifa moja, nafasi iliyopo ni kwa ajili ya SISI moja tu na hakuna WAO. Uzalendo wa kihafidhina haujawahi kuwaacha salama wale wote wanaoutukuza wakati unapowafaa.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ezekiel Kamwaga na kuchapishwa kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 21 Juni 2017. Chanzo: http://www.raiamwema.co.tz/uzalendo-wa-kufungiana-suluhisho-la-kunduchi/

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.