TANGU kutokea kwa songombingo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kutokana na utendaji wa shaka wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, bado hali ya siasa Zanzibar haijapata kivuli cha kutulizana.

Songombingo ilitokea kwa sababu Jecha alifuta matokeo ya uchaguzi huo wa tarehe 25 Oktoba 2015, uchaguzi ambao waangalizi wa ndani na nje walikubali ulikuwa huru na haki. Walisema uchaguzi uliendeshwa vizuri. 

Sababu kubwa ya kufuta matokeo hayo, ukiangalia kwa jicho la kawaida, ni kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilikuwa tayari kimeshindwa. Kwa njia hiyo ya kufuta uchaguzi na matokeo yake, waliopanga waliona itakuwa suluhisho.

Hadithi ni ndefu na imeeleweka kwa wengi. Uchaguzi wa marudio ambao chama kikuu cha upinzani Chama cha Wananchi (CUF) na vingine kadhaa viliususia, ambao hauna nafasi kwenye Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ndio uliotumika kuibakisha CCM madarakani.

Na kwa namna CCM, kupitia mgombea wake Dk. Ali Mohamed Shein ambaye alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa marudio kwa asilimia 92 ya kura, ilivyounda serikali, imeweka kando muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa; tukio la kudharau maamuru ya katiba yaliyoidhinishwa na wananchi Julai 2010.

Maswali ni mengi yasiyo na majibu imara, kutoka wakati ule hadi tulipo; nini kinafuata? Ile haki ambayo CUF wanaamini waliporwa wataipata? Je, hali itakuwaje utakapofika uchaguzi mkuu wa 2020?

Miezi kadhaa baada ya uchaguzi wa marudio kufanyika, nilikuwa Zanzibar kwa ajili ya likizo ya kimasomo. Hakukuwa na zaidi ya mazungumzo ya kisiasa kila upembe upitao.

Ukweli nilishuhudia nyuso za aina tatu: zile zenye matumaini kupita tarehe ya matumaini yao, ubaya ni kuwa tarehe ile ikifika ukimfuata hukupa terehe mpya, ikiisha na hiyo, atakupa tarehe nyengine, ni nyengine-nyengine-nyengine hadi hii leo.

Haya yao, yanafaa kuitwa matumaini yaliyokosa kutimia hadi sasa.

Matumaini haya yaliyokwama, huwa hayaachi kutaja Umoja wa Mataifa, Jumuiya za Kimataifa kuwa ndio zitaleta ile haki ambayo Jecha aliikanyaga kwa maslahi ya chama tawala ambacho anasema kinastahiki kuongoza.

Kuna waliokuwa watulivu mno, adimu hata kupata maoni yao, yaliyo mioyoni mwao ni ngumu kuyatabiri, hawaeleweki ikiwa wamekata tamaa au ni kimya cha kuchoka na kusawijika au kuna walifichalo.

Hili kundi la mwisho ndio wamekata tamaa kabisa, aina ya mazungumzo yao ni ya kuvunja moyo kupita kiasi, hawana chembe ya matumaini juu ya kile wanachoamini kuwa ni uporaji wa haki kurudi kwa mwenye haki.

Matumaini yao ni kama kumtazama paka mweusi kizani, labda naye akutazame ndio umuone. Kwa maneno mengine, ni matumaini yaliyokufa na kukauka.

Huenda wameathiriwa na historia ya siasa za Zanzibar, kuwa za kilaghai, wizi, ubabe, mabavu, kutishana na mbinu chafu. Hukata matumaini kwa sababu wanajua haki ikienda kombo kwenye mikono ya CCM, ndio hairudi. Ndivyo walivyozoea na ilivyozoeleka.

Miezi inaendelea kukatika wala nami sioni mabadaliko makubwa katika siasa zile, Dk. Shein na serikali aliyounda anaendelea kuongoza nchi bila ya kujali wapo maelfu kwa mamia wangali na matumaini kuwa Maalim Seif Shariff Hamad atapewa nchi hata kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Ukiwabishia unakuwa adui.

Katika hali kama hiyo, tegemea tu jambo moja kati ya haya mawili yaliyopo. Moja; kutokuwepo kwa mabadiliko yoyote ya kisiasa hadi mwaka 2020 utakapowadia uchaguzi mwingine.

Pili; ima tegemea mabadiliko ambayo yatatokana na nguvu zilizo nje ya Zanzibar, kwa sababu Dk. Shein na Maalim Seif wamekaa vikao vingi bila ya mafanikio. Mabadiliko hayo, binafsi siyapi nafasi kubwa kutokea.

Ikiwa kutakuwa na mabadiliko yoyote yatakayoondoa mkwamo uliopo sasa, ndivyo wengi tunavyoomba, lakini yasipokuwa, bado kutakuwa na tahadhari kubwa ya namna siasa zitakavyokuwa kuelekea huo mwaka wa uchaguzi mwingine.

Ukweli ni kuwa kundi kubwa la Wazanzibari wanaamini haki yao imeporwa, huku waporaji wakiwa hawana hata wasiwasi au hofu juu ya kundi kubwa la kama hili.

Ni hatari katika nchi kuwa na watu wanaoamini hawatendewi haki kila linapokuja suala la kumchagua kiongozi wa nchi. Kanuni na sheria ziko wazi lakini wanaona kila muhula kanuni na sheria hizo hupindishwa na wao kukoseshwa walichokichagua.

Fujo na vurugu zitokeazo katika baadhi ya mataifa ya dunia hii, zinatokana na hadithi kama hii ya Zanzibar – watalawa kudhulumu haki za wengine tena walio wengi. Huku ni kuitia nchi kwenye mtihani kwa sababu ya ubinafsi tu.

Ninachokiamini siku zote dhulma haina inachokizalisha zaidi ya balaa. Na hilo ndilo niliogopalo. Hapo ndio napata hofu kuwa muhula gani utazalisha balaa!

Ikiwa huko tulikotoka tumepenya kwenye salama ya hatihati, nahofia twendako kama hata hiyo salama ya hatihati inaweza kukosekana na mbadala wake ukawa mbaya. Siombi tuingie kwenye balaa. Naogopa kwa kweli.

Jaalia hakuna mabadilko yoyote ya kisiasa Zanzibar, na Wazanzibari wanatulizana hadi uchaguzi mkuu mwengine unafika, huku CCM wakiwa na akili ileile ya kufanya figisufigisu zao ili washinde kwa lazima.

Ndio maana naiangalia 2020 kwa jicho la hofu zaidi kuliko mabadilko yoyote yanayoweza kutokea sasa. Sitaki kuja kuona demokrasia iliyowekwa kusudi ili raia wachague viongozi wao huku wakiambia kuwa ni haki yao kuchagua wakitakacho, ibadilike na kuwa moshi wa mauti.

Siasa hizi za majitaka kwa upande wa CCM wa Zanzibar, wamekuwa nazo kwa muda mrefu sasa, huko nyuma zimetoa athari lakini mazungumzo yakafanyika na watu wakaendelea na maisha.

Je, ikiwa viongozi wa CCM wataendelea na siasa chafu za aina hii hadi huko twendako, hali itakuwaje? Kuna hakikisho gani kuwa demokrasia ya kuchagua itafanyika kwa salama na amani?

Mbinu gani nyengine chafu itatumika kumuweka madarakani mrithi wa Dk. Shein? Naangalia mbele lakini zaidi ni kiza kinene cha siasa za majitaka, ambazo hazitoipeleka nchi sehemu salama hata kidogo.

Bado yaliyopita wanayahesabu kama si ndwele, huenda wanatafuta ndwele nyengine iliyo kubwa na mbaya zaidi. Mwenyeezi Mungu anawaona.

Tanbihi: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la MWANAHALISI na mwandishi wake Rashid Abdallah anapatikana kwa simu namba +255657414889.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.