NI nani anayestahili kuitwa mkorofi kati ya mwakilishi anayeiambia ukweli serikali ili ijirekebishe au kujisafisha penye madoa, na yule anayetishia hatima ya kisiasa huyo anayeamini anachokisema ni sahihi?

Nadir Abdulatif Jussa, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, anayewakilisha wananchi wa jimbo la uchaguzi la Chaani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, amejitoa kwa ujasiri kuamua kusema anachokiamini.

Mwakilishi huyu kijana aliyeingia katika Baraza kwa mara ya kwanza, anakosoa mwenendo wa ufisadi kwenye miradi ya miundombinu ya barabara. Anasema barabara zinazotajwa kujengwa kwa zaidi ya Sh. 150 bilioni zinaharibika baada ya kipindi kifupi.

Analalamika kuwa ni kutokana na ujenzi wa miradi hiyo kutekelezwa kwa kiwango cha chini. Kampuni iliyojenga ambayo hata hivyo, hakuitaja kwa jina, imechukuliwa tu pasina serikali kujiridhisha kuwa inao uwezo wa kitaalamu na zana za kufanyia kazi.

Hakuthubutu kusema kwamba anajua kilichofanyika kwa maana ya viongozi waliohusika kuiwezesha kampuni hiyo kutunukiwa kandarasi ya barabara zilizoharibika kiasi cha kuwa mbovu kwa muda mfupi wa kutumika kwake.

Isipokuwa Nadir ambaye ni mwakilishi aliyepitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), anasema anasikitika kwamba ujenzi unafanyika kwa kiwango duni huku viongozi wakubwa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakishuhudia lakini wakishindwa kuchukua hatua kukomesha ubadhirifu wa fedha za serikali.

Katika kuonesha kutoridhishwa na uzembe unaofanywa katika jukumu la kusimamia miradi ya miundombinu, Nadir akaliambia Baraza la Wawakilishi kuwa yeye haikubali bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano.

Lakini kwa kujua ukorofi wa uongozi wa serikali kwa wanaoikosoa, Nadir akatoa indhari kuwa yeye haogopi mtu yeyote; amesema anachokiamini na haongezi kitu kwa sababu anajua “watatokea wakubwa waseme hivi na vile… hawataki kusikia mawazo tofauti.”

Nadir anazungumzia uzoefu aliokwishaupata. Amekuwa akionekana kama anafanya kazi ya upinzani. Ameshutumiwa mara kadhaa hadharani pamoja na wawakilishi wengine ambao kama yeye, wamejenga ujasiri wa kuthubutu kueleza makosa ya serikali.

Na Jabir Idrissa 

Yaliwahi kuwakuta Jaku Hashim Ayub (Paje), Simai Mohamed Said (Tunguu), Hamza Hassan Juma (Shaurimoyo) na Hassan Khamis Hafidh (Welezo). Kutokana na kujitoa kusema ukweli wao, wamesimangwa.

Machano, kada makini wa CCM, aliyekuwa mjumbe wa Barala la Mapinduzi (BLM) katika serikali ya umoja wa kitaifa aliyoongoza Dk. Shein 2010/2015, safari hii ameibana serikali kujisafisha na uchafu wa kujiingiza kwenye biashara ya mchanga iliyokuwa ikifanywa na wananchi wenyewe kwenye maeneo yao ya mashamba.

Machano anaishangaa serikali kuwa iliamua kuachana na biashara ya bidhaa za chakula kikuu kwa Zanzibar – mchele, unga wa ngano na sukari – kwa kuwa haitakiwi kufanya biashara. “Leo inarudi kule ilikoacha, ni jambo la ajabu.”

Alimtafadhalisha waziri anayehusika na maliasili na mazingira, Hamad Rashid Mohamed, aliyeteuliwa waziri kutokea chama cha Alliance for Democratic Party (ADC), baada ya kupata kura 9,734), sawa na asilimia 3 ya kura, kwamba ameingia katika mradi usiofaa wakati ni kiongozi mzoefu katika siasa.

Ametaka pale serikali inapotangaza kuwa imeongeza mapato ya mchanga unaochimbwa kwa kupata Sh. 500 milioni, kwa msimamo wake hizo ni fedha haki ya wananchi wanaomiliki mashamba ambamo mchanga unachimbwa. Alisema ni kuwadhulumu wananchi ambao walikuwa wakifuata taratibu zote za kiserikali kupata kibali cha kuchimba mchanga kwa ajili ya shughuli za ujenzi.

Machano amesema hatua ya serikali kujiingiza katika biashara ya mchanga, imesababisha bei ya maliasili hiyo kupanda kwa kasi ya zaidi ya asilimia 100.

Nikamsikia Soud Said Soud, Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi (BLM) aliyeteuliwa kutoka Chama cha AFP, akisema ana neno dhidi ya watendaji wasiofuata utawala wa sheria, utawala bora na wanaojihusisha na vitendo vya ufisadi serikalini.

Soud amesema anataka ofisi ya Balozi Seif Ali Iddi ichukue hatua dhidi ya viongozi hao si hivyo atawashitaki kwa kuwataja atakapokutana na Dk. Shein. “Nachukia viongozi wanaodharau utawala wa sheria na utawala bora, hawaitakii nchi mema. Serikali iwadhibiti kabla ya kuwashitaki kwa kiongozi mkuu,” alisema.

Kama ni kutoa alama, basi wajumbe hao wanastahili alama zaidi ya 8 kwa kumi, kwani wamegusa maeneo ambayo ni kero kubwa inayokabili wananchi wa Zanzibar. Fedha za serikali zinatafunwa kama vile ndani ya serikali kuna mchwa binadamu. Hakuna hatua makini zinazochukuliwa wanaoshukiwa.

Mara mbili serikali kupitia Wizara ya Fedha na Uchumi inayoongozwa na Dk. Khalid Salim, imetoa taarifa ya matendo ya ufisadi serikalini yaliyowagusa watendaji wakubwa katika mawizara, lakini kufikia sasa hakuna aliyeshitakiwa licha ya kuwepo Sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Kituko ni pale ambapo serikali inalaumiwa kwa kulinda watendao ufisadi huku kiongozi wa serikali ndani ya Baraza la Wawakilishi akisikika kuwatishia baadhi ya wawakilishi wenye ujasiri wa kuthubutu kuyaeleza mabaya ya serikalini kama huo ufisadi.

Balozi Iddi amesikika akisema barazani kuwa wawakilishi wajue wao ni viongozi wanaopaswa kutumia busara katika kuikosoa serikali. Haistahili kwao kutoa kashfa dhidi ya serikali, tena kwa kutumia maneno makali.

Alitoa maelezo yaliyoashiria hasa kumlenga mwakilishi Nadir wa Chaani. Balozi Iddi alisema mwakilishi anapoikosoa serikali huku akisema hamuogopi mtu yeyote, anaweza kuchukuliwa kuwa ameamua kukivua nguo chama kilichompa tiketi ya kugombwa uwakilishi.

Sasa kama yeye mwakilishi anajinasibu kuwa hamuogopi mtu yeyote, na sisi tutasema kuwa analazimia kuangaliwa kama ana uadilifu kweli au ameamua kukichafua chama kilichomleta humu ndani ya baraza, alisema.

Balozi Iddi amejibu ukosoaji wa Nadir ambaye kiuongozi anao wajibu wa kuyasema yasiyofaa kwa kuwa moja ya majukumu makuu ya mwakilishi ni kuieleza serikali ilipokosea na kuishauri kuhusu utendaji mzuri unaoleta tija kwa nchi na watu wake.

Nadir na wawakilishi wenzake wanaothubutu kuikosoa serikali, hawajatenda kosa lolote si kisheria wala kimaadili, lakini inaeleweka anapotokea kiongozi mkubwa wa serikali akawakemea. Panakuja swali muhimu la kwamba huyo anayewakemea ndio anaonesha namna uongozi wa juu wa serikali ulivyokosa dhamira ya dhati ya kukomesha ufisadi?

Tanbihi: Makala hii iliyoandikwa na Jabir Idrissa ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la MWANAHALISI la tarehe 12 Juni 2017.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.