Tanzania ni mojawapo ya nchi chache sana duniani zenye neema tele ya maji. Hatujawahi kukosa maji hata siku moja! Ila tunashindwa tu kuyasambaza ili yaje kwenye makazi, mashamba na viwanda kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Kwenye uso wa ardhi, tuna maji ya bahari, maji ya maziwa makubwa kuliko yote barani Afrika, maji ya mito mikubwa na mirefu inayotiririka masaa 24 kila siku kwa miaka yote.

Tuna maji ya ardhini ambayo kwa utafiti wa kitaalamu ni zaidi ya maji yaliyoko kwenye uso wa ardhi. Kwa upande wa Tanganyika tuna mabonde 9 yenye vyanzo vikubwa vya maji nchini. Hatuhitaji kutafuta maji, tunayo kwa wingi. Tunatakiwa kuyasambaza tu, basi!

Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka 2017/28 kama ilivyowasilishwa na Waziri Gerson H. Lwenge, na kama ilivyowekwa kwenye tovuti ya wizara, ukurasa wa 122, inasomeka: “… nchi yetu imebahatika kuwa na rasilimali za maji za kutosha juu na chini ya ardhi ambazo ni pamoja na mito, maziwa, maji ya chini ya ardhi na maeneo oevu.”

Tunataka Mungu atujaalie vipi kuwa na neema hii ya maji? Waziri alijichanganya katika hotuba yake sura ya 15, ukurasa wa 7 aliposema: “mwenendo usioridhisha wa upatikanaji wa mvua kwenye baadhi ya maeneo nchini umeathiri shughuli za maendeleo zikiwemo kilimo, ufugaji na uzalishaji umeme.”

Uongo mtupu! Kama tumebahatika kuwa na maji ya kututosha kiasi hicho, chini na juu ya ardhi, kwa nini waziri ategemee mwenendo wa mvua? Mbona kasema vyanzo vingine ni vya kutosha? Na mwaka huu mvua za kutosha zilinyesha na tukaleta mafuriko baada ya serikali kushindwa kuyavuna maji ya mvua hususan katika maeneo ya pwani na visiwani Zanzibar. Tukivuna maji ya mvua vizuri na kuyahifadhi, hata migogoro baina ya wakulima na wafugaji itatoweka kabisa.

Kulingana na utafiti wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, nchi yetu ina eneo la hekta milioni 29.4 zinazofaa kilimo cha umwagiliaji. Lakini eneo linalotumika kwa kilimo hicho ni hekta laki 4.5 tu! Eneo hilo huchangia takribani 24% ya mahitaji ya chakula chote nchini. Ina maana tukimwagilia hekta millioni 1 kati ya milioni 29.4, zitachangia nusu ya mahitaji yote ya chakula nchini.

Na endapo tutamwagilia hekta milioni 2 tu kati ya milioni 29.4, badala ya kutegemea mvua, tutakidhi 100% ya mahitaji yote ya chakula na ziada kubaki. Hatutategemea tena mvua zisizotabirika, na pengine tutapata akili ya kuzivuna vizuri zikija kwa wingi kwa ajili ya akiba ya kunyweshea mifugo, matumizi ya nyumbani na kuzalishia umeme.

Pamoja na kwamba tunapaswa kutumia kilimo cha umwagiliaji hekta milioni 2 tu kukidhi mahitaji ya chakula chote nchini, Wizara inapanga kumwagilia hekta milioni 1 tu ifikapo mwaka 2020. Kwa hapo niseme wazi kuwa tunatania na tunajitakia kuwa na upungufu au ukosefu wa chakula, na maeneo mengine kukumbwa na njaa kali.

Jambo lingine, kuna watu husema wana kero ya maji. Kamwe maji si kero ila sisi ni kero kubwa. Ukosefu wa maji ni kero, lakini si maji yenyewe! Watu tunaleta kero wenyewe kwa kukosa mipango na utekelezaji. Aidha, hakuna maji machafu ila tunayachafua kwa vinyesi vyetu, ukurutu wetu, vumbi tunalotimua na taka tunazotupa ovyo. Hata kipindupindu hakiletwi na maji machafu, bali husababishwa na uchafu wetu. Msomaji, asikuambie mtu, kipindupindu ni uchafu wetu!

Kibaya zaidi, tunakosea sana tunaposema maji yamekosa mwelekeo. Maji hufuata mkondo wake lakini hayana macho ya kukwepa makazi ya watu au mashamba. Sijawahi kuona maji yakitiririka yenyewe kupanda milimani! Ukitaka yatiririke kuelekea huko basi utatakiwa kutumia nguvu ya ziada ya kuyasukuma kupanda milimani.

Wanaokosa mwelekeo na mipango ya kuyaelekeza maji ya mvua yanakopaswa kupita ni sisi. Kupita wapi? Kwenye mikondo, mifereji, mitaro na kutuama kwenye mabonde, malambo, mabwawa, matenki na visima, na kuyahifadhi yatufae wakati wa ukame. Mvua isigeuke mafuriko yenye maafa bali iwe neema yenye faida kwetu. Hiyo ndiyo miundumbinu na miundomsingi ya maji ya kutusaidia sisi wenyewe.

Cha kwanza kwa umuhimu katika uhai wetu ni hewa na kisha maji. Ukiwa na hewa na maji utabaki hai kwa siku kadhaa hata kama utakosa chakula. Matabibu bingwa hukiri kuwa dawa ya kwanza kumtibu mtu mahututi si vidonge wala sindano, bali ni maji.

Ni ukweli usiopingika maji ni uhai, uzima na afya yetu. Itoshe kusema tuna baraka na bahati ya maji tele. Ni kiasi tu cha kuwa na mwelekeo na mipango ya kuyahifadhi, kuyasambaza na kuyapa mwelekeo stahiki.

Tusiyaache maji yapite na kutuama kwenye barabara zetu, makazi yetu na mitaa yetu. Kuna baadhi ya nchi huhifadhi maji ya mvua ya kutosheleza miaka mitatu bila mvua. Lakini sisi ukija ukame tunalia, ikija mvua tunalalama na wengine kulaani!

Badala ya kuyavuna maji tunavunwa sisi na maji kwa kuzamishwa na kufariki kizembe kabisa. Laana gani hii? Eeh Mungu, naomba tupe macho na akili ya kuiona vema neema ya maji uliyotuumbia kwa ajili ya uhai wetu, mimea, wanyama, wadudu na kitu chochote chenye chembechembe ya uhai.

Tanbihi: Makala hii iliyochapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Mwelekeo la tarehe 13 Juni 2017, imeandikwa na Gwandumi Gwappo A. Mwakatobe, mchambuzi wa masuala ya kitaifa na kimataifa anayeishi Mwakaleli, Busokelo, Rungwe, Mbeya. Anapatikana kwa anuani ya baruapepe: gwandumi@hotmail.com au gwappomwakatobe@gmail.com

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.