Vidio inasambaa mitandaoni. Vijana wanaonekana kumzonga kwa maneno na kumchapa bakora mtu anayetajwa kuwa mlevi katika mchana wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Hakika, ni kitendo kisicho cha Kiislamu hata chembe kwa mwenye hasa kuujuwa Uislamu na qaida zake na taratibu zake za kuyashughulikia makosa ambayo yanajitokeza kwenye jamii.

Lakini hapa sikusudii kuzama undani wa adabu za Uislamu kwenye mazingira kama haya yanayotajwa kwenye vidio hiyo, bali kuonesha namna usambazaji wa vidio yenyewe na maoni yanayotolewa na wachangiaji wake wanavyoitumia kama mbinu ya kipumbavu ya kutaka kuulaumu Uislamu wenyewe kwa vitendo vya kishenzi walivyovifanya vijana hao.

https://m.youtube.com/watch?v=pn8VGqxGWh0

Iwe wanaotumia mbinu hii ya kila siku wanajiita waumini wa Uislamu au Ukristo, ukweli ni kuwa hawafuati mafundisho yoyote ya Mitume yao – si Muhammad (S.A.W) wala Yesu (A.S). Yote haya hayatokani na Uislamu wala Ukristo wa kweli. Ni ushenzi tu.

Sehemu ya wachangiaji wa vidio yenyewe wanaonekana kuashiria kuwa mlevi aliyemo kwenye vidio hii ni Mkristo na anatendewa anayotendewa hayo na Waislamu kwa sababu ya Ukristo wake.

Lakini nani aliyekuambieni kuwa huyo mlevi alikuwa ni Mkristo? Kwa ushahidi upi? Inawezekana kuwa mlevi si Mzanzibari, lakini zaidi ya hapo hatujui ana imani gani. Kwa nini mnalazimisha lazima alikuwa Mkristo? Kwani Tanganyika hakuna dini za kienyeji ila kuna Waislamu na Wakristo peke yao?

Kulalamika kuwa anayeonewa ni Mkristo ni moja katika mbinu za kutaka kuonesha kuwa Waislamu wanawaonea Wakristo visiwani Zanzibar. Na hili si la kweli. Hawakuonewa walipokuwa wakitawala Masultani wala hawakuonewa alipotawala Muingereza. Wala hawaonewi leo, wakitawala Watanganyika.

Hebu tuambizane ukweli mtupu kama kweli tunataka kuusikia ukweli. Haya aliyofanziwa mlevi ni ushenzi tu. Na ushenzi huu, hata kama unaonekana kutendeka ndani ya ardhi ya Zanzibar kwenye vichochoro vya Mji Mkongwe, asili yake hasa unatokea Tanganyika. Ni Tanganyika ambako hivi leo ukimnadi mtu tu: “Mwizi huyoo!”, basi hapo hapo huyo mtu hupigwa mpaka akauwawa, tena kwa kuchomwa moto. Salama yake watokee polisi na kumchukua kituo cha polisi.

Huu ndio ushenzi wa kweli kweli duniani. Humo humo mtandaoni muna vidio ya mwanamke aliyenadiwa wizi na akapigwa kwa mawe mpaka akaanguka taabani na mwishowe, kwa ushenzi wao hao, wakamchoma moto na kuumuuwa. Huu ndio ushenzi wa kweli.

La kustaajabisha sana kabisa ni kuwa katika kundi kubwa kama hilo la mamia ya watu, na hapana shaka palikuwepo na watu wanaojigamba kuwa ni Waislamu na Wakristo, na hapajatokea hata mtu mmoja aliyenadi kuwa haya mfanyayo si ya Kiislamu wala ya Kikristo, bali ama waliingia nao “ngomani” na kumpiga mawe na kumchoma moto huyo mwanamke au walisherehekea kitendo hicho cha kishenzi.

Vidio nyengine ya karibuni ni ya mwanamke aliyevaa nguo fupi katika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, ambapo anaonekana akizongwa kwa maneno na kuvutwa huku na kule na vijana wa eneo hilo, hadi naye walipokuja polisi kumuokoa.

Ushenzi huu wa Tanganyika ndio waliouleta Zanzibar leo. Tumeishi Zanzibar siku za ukoloni na hatukuyaona haya ya mtu kuingiliwa katika uhuru wake wa kibinafsi. Uonevu umeanza katika utawala wa wafalme Karume na Nyerere. Na mifano mingi sasa sana tunayo. Msituchokoze!

La kustaajabisha pia ni kuona Oman inatiwa kati bila ya sababu yoyote ile. Imehusu nini hapa hata kuitaja Oman! Mzushi mmoja ameandika eti: “Mbona wanaleta sharia za Oman?” Sharia gani za Oman? Unazijua sharia na kanuni za Omani au ndio unabobojoka tu ili uendeleze propaganda za ‘Mfumo Tapakaza Chuki’ mlionao? Mfumo ambao hauangalii ukweli ulivyo?

Kama hamujui, basi ndio muelewe kuwa sharia za Oman haziruhusu ushenzi kama huu. Hao vijana wangeliyafanya hayo Oman, wangelikamatwa, kushtakiwa na kupelekwa mahkamani. Oman ni nchi inayosifika kabisa duniani kwa usalama na uhuru wa kibinafsi na uhuru wa kidini. Hakuna watu wa dini au madhehebu yoyote wanaosumbuliwa Oman.

Kuinyooshea kidole cha lawama Oman bila ya sababu ni moja katika tabia ya kishenzi kabisa. Kisa nini, hivyo ndivyo mlivyojazwa propaganda tokea utotoni mwao na watapakaza chuki. Someni na tumieni akili zenu muujuwe ukweli, si vyema kutapakaza chuki za uwongo.

Tanbihi: Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kwa jina la Mbaraka Mwadini 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.