Kuna taarifa kwamba watu wanaoshukiwa kuwa maafisa wa vyombo vya dola wanaendelea na operesheni ya kimyakimya ikiwalenga mahsusi viongozi wa ngazi za chini wa Chama cha Wananchi (CUF) mkoani Pwani. 

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya chama hicho, Julius Mtatiro, hadi usiku wa jana (Ijumaa, Juni 9), kiongozi mwengine wa serikali ya mtaa alikumbwa na zoazoa hiyo. 

“Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kilumike, Ikwiriri – Rufiji (CUF), amechukuliwa na vyombo vya dola kwa staili ile ile ya utekaji na hajulikani yuko wapi”, anaandika Mtatiro kwenye ukurasa wake Facebook, akiongeza kwamba jana hiyo hiyo, wenyeviti wengine wawili wa kata tafauti walichukuliwa na vyombo vya dola na hadi sasa hawajulikani waliko. 

Juhudi za ndugu na viongozi wenzao kwenye mkoa huo kuwatafuta kwenye vitu vyote vya polisi vya Rufiji hadi sasa hazijafanikiwa.  

“Bado natoa wito kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama, kwamba viongozi hawa wapatikane wakiwa salama, lakini pia wasiteswe kama wale wengine 25, wahojiwe kwa njia sahihi na kama kuna ushahidi wowote muhimu wapelekwe mahakamani,” amesema mwenyekiti huyo wa CUF Taifa. 
SOMA TAARIFA KAMILI HAPO CHINI 

VIONGOZI WENGINE WA CUF WAMEKAMATWA JANA!

Jana Ijumaa usiku Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kilumike, Ikwiriri – Rufiji (CUF), amechukuliwa na vyombo vya dola kwa staili ile ile ya utekaji na hajulikani yuko wapi. 

Jana hiyo hiyo, viongozi wawili wa CUF (Wenyeviti wa Kata tofauti), wamechukuliwa na vyombo vya dola (hawajulikani waliko). Naposema hawajulikani walipo nina maana kuwa asubuhi hii tayari tumepata uhakika kuwa hawapo kwenye vituo vya Polisi vya Rufiji.

Bado natoa wito kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama, kwamba viongozi hawa wapatikane wakiwa salama, lakini pia wasiteswe kama wale wengine 25, wahojiwe kwa njia sahihi na kama kuna ushahidi wowote muhimu wapelekwe mahakamani. 

Kwa kweli tumechoka kuona viongozi wetu wanatekwa/kukamatwa na vyombo vya dola, wanateswa na kisha wanaachiwa. Oparesheni bubu za namna hii zinazolenga kuumiza watu wasio na hatia haziwezi kulisaidia taifa letu.

Viongozi wetu wa Rufiji/Mkuranga/Kibiti wote wanaripoti kuwa hivi sasa wale wenzao wa CCM ndiyo wanavielekeza vyombo vya dola viwakamate. Na wanaokamatwa ni viongozi wa kiserikali waliochaguliwa kupitia CUF pamoja na wale viongozi wa CUF (Matawi na Kata) wanaotoka maeneo ambayo CUF ina nguvu kisiasa.

Chama chetu kinataka Oparesheni ya kuwasaka wauaji na makundi mabaya katika wilaya hizi iendelee, lakini hatukubaliani na APPROACH ya kukamata viongozi wa kiserikali wa CUF kila mahali ambako CUF ina nguvu. Oparesheni ikiendelea kwa mtindo huu itaanza kuchukua mkondo wa kisiasa na itapoteza maana. Ukizungumza na raia wa Rufiji/Kibiti/Mkuranga – wanakueleza dhahiri kuwa mauaji ya viongozi zaidi ya 30 wa CCM hayakufanywa wala kupangwa na viongozi wa chama chochote cha siasa.

Sasa leo wanapokamatwa viongozi wa CUF wa kuchaguliwa almost kila mahali, tunasema kwa uwazi kuwa oparesheni hii itapoteza mashiko. Na Polisi haijiulizi kwa nini tangu ianze kukamata viongozi wa CUF haijawakuta na chochote? Kwa nini hadi jana iendelee kuwakamata? Ndugu zangu, hali hii haikubaliki kabisa. Vyombo vyetu vya Usalama hebu vifanye kazi zake kwa weledi na utaratibu unaozingatia haki, sheria na wajibu.

#Mtatiro J.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.