Urithi wa kitamaduni (cultural heritage) ni eneo ambalo linapotea kwa kasi katika visiwa vya Zanzibar. Kumekuwa na ushajiishaji mdogo mno kwa Wazanzibari kuendeleza mapishi ya asili hasa yatokanayo na vyakula vya ardhini kama vile mihogo, viazi vikuu, majimbi na kadhalika.

Hali hii iwapo itaachiwa iendelee, tena bila ya kutengenezwa mikakati madhubuti, huenda ikaiwacha Zanzibar bila ya urithi huu hapo mbele. Waraka huu unalenga kujenga hoja ya kutetea mapishi ya vyakula asili vya Zanzibar pamoja na kuonesha umuhimu miongoni mwa vijana wa Kizanzibari katika kuyaenzi na kuyadumisha.

Kwa mujibu wa muongozo wa kimataifa juu ya utalii wa kitamaduni na umuhimu wa urithi wa mwaka 2002 (ICOMOS 2002), urithi wa kitamaduni unaweza kutafsiriwa kama namna ya jamii inavyoishi kwa mujibu wa ilivyorithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi chengine. Urithi huu unajumuisha desturi, matendo, maeneo, vitu, sanaa, na tunu za sehemu husika.

Kimsingi, urithi wa kitamaduni umegawika katika maeneo mawili: ule ulio dhahiri (tangible cultural heritage) usio dhahiri (intangible cultural heritage). Mifano ya urithi ulio dhahiri ni kama vile majumba ya kihistoria, ngoma za asili, kazi za mikono, mapishi na kadhalika. Kwa upande mwengine, urithi usio dhahiri ni kama vile mila, desturi, hadithi za kale, ujuzi wa kijadi na kadhalika.

Mitazamo na hoja tafauti za urithi wa utamaduni

Kiujumla, linapozungumzwa suala la urithi wa kitamaduni kwa hapa Zanzibar, mawazo ya wengi hulenga moja kwa moja kwenye Mji Mkongwe ambao umepewa hadhi ya urithi wa kimataifa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) mwaka 2000.

Ngome Kongwe, moja ya majengo makongwe kabisa katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Kiukweli, Mji Mkongwe si urithi pekee wa kitamaduni uliopo hapa Zanzibar. Mavazi ya Kizanzibari, lugha ya Kiswahili na lahaja zake, ngoma za kiasili, tiba za kijadi na mapishi ya Kizanzibari, ni miongoni mwa mifano mingi ambayo yamerithiwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi chengine.

Kumekuwa na mitizamo tafauti kwenye suala la ama kutunza au kuachia mambo yaende kama yanavyokwenda. Kwa kiasi kikubwa kumekuwa na mitizamo miwili juu ya hili, ambapo ule mtazamo uitwao wa kikale unahimiza kwenye utunzaji, mtazamo wa kisasa hauoni haja ya utunzaji wa urithi wa kitamaduni.

Kwa mtazamo wa kisasa,  urithi wa kitamaduni hauwezi kushindana na nguvu za utandawazi ambazo zinapelekea uhamaji wa watu kutoka eneo moja kwenda eneo jengine kirahisi tafauti na hali ilivyokuwa zamani.

Hata hivyo, mtazamo wa kikale ambao ndio msimamo wa UNESCO na wataalamu wingi wa mambo ya tamaduni na utalii unalenga zaidi kwenye utunzaji wa urithi wa kitamaduni kwa lengo la kulinda utambulisho (identity) na historia ya eneo ama nchi husika. Kwa mfano, watu wa utalii mara nyingi huathiriwa na mitizamo ya kikale kutunza urithi wa kitamaduni kwa ajili ya kuongeza ajira kwenye sekta ya utalii, kuongeza idadi ya vivutio vilivyopo, na kuwa na utaliii endelevu kwa ujumla.

Kwenye hili, mitizamo ya kiutalii kwa mfano haiwezi kuwa sawa kabisa na mitizamo ya kidaktari, ambayo hutizama zaidi athari za urithi wa kitamaduni kwa afya za wanajamii. Kwenye suala la mapishi, kwa mfano, mtazamo wa kidaktari hutizama zaidi namna gani mapishi yanaathiri afya ya mlaji.

Ndizi mbivu iliyopikwa kwa nazi na viungo kama vile hiliiki, zabibu na mdalasini ni miongoni mwa vyakula asilia vya Zanzibar.

Kwa hapa Zanzibar, ni dhahiri kwamba hakujafanyika tafiti nyingi zinazobainisha sababu zinazopelekea kupendwa kwa aina mpya za mapishi hasa miongoni mwa vijana wa mijini na athari zake kwa urithi wa kiutamaduni.

Kuna mtazamo mwengine kwamba mapishi ya asili hayawagusi baadhi ya jamii zinazoishi Zanzibar kama vile Wahindi, Washihiri, Waarabu, Wangazija, Mabohora na wengineo ambao mapishi yao kiasili yapo tafauti na mapishi ya jamii nyengine za Kizanzibari. Binafsi kula au kutokuwa vyakula kama vile mihogo, maji mbili na viazi vikuu ni suala ambalo linashangaza.

Kwa mfano, ikiwa badia zinaliwa na jamii za Kizanzibari za mjini, nga’mbo, na hata mashamba na kukubalika kuwa ni mapishi ya Kizanzibari, inatia shaka kwamba jamii za Kihindi, Kibohora na Kiarabu zisile mihogo na majimbi!?

Kilicho dhahiri kwenye hili, ni kwamba asilimia kubwa mno ya Wazanzibari bila ya kujali asili zao imekulia kwenye vyakula vya asili vya Zanzibar.

Hoja nyengine zitolewazo kwamba hakuna haja ya kutunza urithi wa kitamaduni kwa sababu Zanzibar ni mchanganyiko wa watu (cosmopolitan), kwa hivyo hakuwezi kuwa na urithi wa kitamaduni unaowakilisha jamii yote ya Zanzibar. Hii nayo ni hoja dhaifu.

Kwa kweli, hakuna asiyejuwa kuwa majimbi, mihogo, viazi vikuu na kadhalika ni vyakula vyenye asili ya Zanzibar na kwamba hakuna hata jamii moja katika jamii za Kizanzibari iwe ya Kihindi, Kingazija, Kisomali, Kikojani ama Kishihiri ya mjini ama vijijini kwa asili na asili isiyokula kwa uchache kimoja kati ya vyakula vilivyotajwa hapo juu.

Maana yake ni kwamba pamoja na aina nyingine nyingi za mapishi kutoka katika jamii tafauti za Kizanzibari, ni suala lililo wazi kwamba mapishi ya jamii tofauti zinazoishi Zanzibar yaliingizwa kwa karne na karne na kuwa sehemu ya urithi wa kitamaduni wa Kizanzibari.

Muhogo na ndizi ni katika vyakula ambavyo vinaitambulisha Zanzibar.

Katika ufafanuzi wa hili na kwa kutumia mifano mingine iliyo nje ya mapishi, kwa mfano, Wakristo wa Zanzibar wanatowa salaam ya “asalaam aleykum”, wakivaa mitandio kwa sababu tu ni sehemu ya utamaduni wa Zanzibar na sio sababu za kidini. Hivyo hakuna ajabu kwa Mzanzibari mwenye asili ya Kiarabu, Kihindi na Kingazija kula mihogo, viazi vikuu, majimbi na vyakula vyengine vya asili.

Wenye hoja hii, ni sawa na wale wanaoshajiisha kuvunjwa kwa Mji Mkongwe ili ujengwe mji mwengine mpya kwa sababu hawajuwi thamani ya urithi wa kitamaduni kwa nchi husika. Athari hii huchangiwa zaidi na kundi la mitizamo ya usasa. Ni sawa na wale wanaoyatizama maendeleo ya nchi kwa kigezo cha urefu wa majumba kama vile wanavyoitizama Dubai dhidi ya Uingereza ama nchi nyengine za Ulaya Magharibi.

Kuna hoja ya kupanda bei za vyakula ambayo inatolewa na baadhi ya wananchi. Hivi sasa, kumekuwa na mlala mikononi kwamba vyakula vya asili ni ghali ikilinganishwa na vyakula vyengine jambo ambalo linawafanya Wazanzibari kutopika mapishi ya asili. Kuhusu hoja hii, kuna ukweli wa kiasi fulani, lakini pia kuna kuzidisha mambo. Kwa mfano, wakati fungu la majimbi au viazi vikuu likiuzwa shilingi 5,000, boga au muhogo linauzwa kwa wastani wa shilingi 2,000 tu, huku njugu mawe nazo hazizidi shilingi 4,000 kwa kilo.

Cha ajabu ni kuwa mtu huyo huyo anayelalamikia ughali wa majimbi na mihogo, anakula chipsi na kuku zinazogharimu wastani wa shilingi 10,000! Hivyo, hapo ndipo suala la mapenzi ya vyakula, ambalo limeelezwa, linapothibitika.

Hoja nyengine inatolewa kuhusu misimu ya vyakula. Ni kweli kwamba mapishi yatokayo na vyakula vya ardhini mingi yao hupikwa kwenye mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Ama vyakula kama pilau na biriani navyo huonekana zaidi katika nyakati na mahala fulani kama vile maharusini, siku za sikukuuu na siku nyengine maalum. Hata hivyo, hali ilivyo hivi sasa haioneshi mapenzi makubwa kwenye vyakula vya asili.

Umuhimu wa kutunza na kuenzi mapishi ya asili

Mwaka 2013, UNESCO walitoa baadhi ya faida za kutunza na kusimamia urithi, ikiwemo urithi wa kitamaduni, kama inavyojadiliwa katika waraka huu.

Baadhi ya faida ni kama hizi zifuatazo:

Mosi, kutunza ukale na kutoa hifadhi ya ukale dhidi ya usasa. Urithi wa kitamaduni kwa kiasi kikubwa unatowa hifadhi ya ukale dhidi ya usasa. Kwenye mjadala wetu wa mapishi, kwa mfano, kuendeleza mapishi ya asili kunahifadhi athari zinazoweza kutokezea kutokana na mapishi mapya yanayokuja. Iwapo watu wote wa Zanzibar watapika mapishi ya kisasa, basi mapishi ya kizamani yatapotea moja kwa moja.

Kamba wa pwani na mbogamboga sio tu nii chakula cha asili, lakini pia kina faida kubwa kwa afya.

Pili, kutunza na kuenzi mapishi ya asili kunaongeza kiwango cha kujitambuwa. Kwa mfano jamii za Kihindi, Kiarabu, Kingazija, Kimakunduchi na nyengine za Zanzibar zinaweza kuishi pamoja na vizazi vyao vikatambuwa kwamba Zanzibar ni nchi iliyo na mchanganyiko mkubwa wa watu, na kuvifanya vizazi hivyo kuishi bila kubaguwana kwa sababu hata mapishi yao yanathibitisha tafauti hizo.

Kwa mfano, badia ambayo asili yake ni Wahindi, itasaidia kuengeza utambuzi kwa Wazanzibari kwamba Wahindi wa Zanzibar ni Wazanzibari na si wageni kama inavyoweza kufikiriwa na baadhi ya watu wasioijuwa historia ya Zanzibar. Halikadhalika, uwepo wa muhogo unasaidia Wazanzibari kujitambuwa kwamba kulipita Wareno ambao kimsingi ndio waliouleta huo hapa Zanzibar.

Tatu, utunzaji wa urithi wa kitamaduni unasaidia kutatuwa matatizo yaliyopo sasa. Hivi sasa, kwa mfano, kuna tatizo la chakula cha chipsi, burger na sausage ambazo zimeingizwa hivi karibuni na kufanywa kuwa ndio vyakula adhimu na baadhi ya Wazanzibari ambao hawajitambuwi.

Iwapo kungeenziwa vyakula vya asili vya Zanzibar, japo kuwa chipsi na burger zingeendelea kuwepo, lakini zisingechukuliwa kama ilivyo hivi sasa kuwa ndo vyakula vya walioendelea!

Mbali ya faida zilizotajwa na UNESCO, kuna faida nyengine kadhaa za kutunza na kuendeleza mapishi ya asili ambayo kimsingi ni sehemu ya urithi wa kitamaduni. Zifuatazo ni baadhi ya faida hizo:

Utunzaji na uenziji wa mapishi ya asili unaongeza fursa za ajira hasa katika sekta ya utalii. Kwa mfano, hivi sasa kumekuwa na safari zinazouzwa kwa watalii juu ya mapishi ya Kizanzibari (cooking tours) ambazo zinasaidia sana kutowa ajira kwa kinamama wanaopika mapishi hayo, watembezaji watalii na wauzaji wa bidhaa zenyewe. Bila ya uwepo wa vyakula hivi vya asili, isingewezekana kufanya haya ati kuwaonesha wageni chipsi kuku ambazo kwao pia zipo.

Mapishi ya asili pia husaidia nchi kujitangaza kiutalii. Takwimu zilizokusanywa na S. I. Salim wakati akifanya utafiti kwa ajili ya shahada yake ya uzamifu juu ya uhusiano kati ya utalii na vyakula asilia zinathibitisha kwamba zaidi ya asilimia 67 ya wageni wote wanaoitembelea Zanzibar wanavutika na utalii wa kitamaduni, ambao umekuwa ni kivutio kikubwa duniani hivi sasa na kwa hapa kwetu bado hatujawa sawa kwenye eneo hili.

Chipsi na urithi wa kitamaduni wa Zanzibar

Vyakula kama hivi hata kama vinaonekana vizuri machoni havina asili ya Zanzibar.

 

Kwa mujibu wa tafsiri, urithi wa kitamaduni ni lazima uwe umerithiwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi chengine. Hivyo, linapokuja suala la chipsi ama, burger na wenzao, historia inatuonesha kwamba ni vyakula vilivyokuja Zanzibar miaka ya hivi karibuni ikiwa ni chini ya miaka thalathini. Kwa mtazamo wa urithi wa kitamaduni, basi vyakula hivyo  haviwezi kuwa sehemu ya urithi wa kitamaduni wa Zanzibar.

Vile vile, asili ya chipsi ilivyokuja hapa Zanzibar zilikuwa sehemu ya vyakula vya mitaani tu (junk food) na bado haziwezi kuchukuliwa kama ni miongoni mwa vyakula adhimu ambavyo mtu anaweza kumkaribisha mgeni nyumbani kwake. Ni bahati mbaya kuwa leo hii chipsi zimefanywa kuwa sehemu ya vyakula vya majumbani na watu kuacha kula vyakula vyao.

Cha ajabu ni kuwa mikahawa mingi katika kila kona ya mitaa utakayopita Zanzibar, ukiwacha michache kama vile Lukman, katika siku za karibuni imekuwa ikiuza chipsi kuku na burger tu!

Hii kwa kweli inaondosha haiba ya Zanzibar ile iliyokuwa ikisifika kwa ustaarabu. Vyakula vya ovyo ovyo leo vimepewa kipaumbele na kupoteza haiba nzima ya Zanzibar ambayo ikisifika sio tu kwa ustaarabu, bali pia mapishi ya namna tafauti.

Nihitimishe makala hii kwa kusema kwamba kuna ulazima na haja ya kuenzi na kudumisha mapishi ya asili ya Zanzibar. Kama tulivyoona, kuna mitizamo miwili mikuu juu ya urithi wa kitamaduni, mtazamo wa kikale na mtazamo wa kisasa. Vile vile kutokana na umuhimu wa kutunza na kuenzi urithi wa kitamaduni, kuhifadhi ukale dhidi ya usasa, kuongeza kiwango cha kujitambuwa, utatuzi wa matatizo yaliyopo, ongezeko la ajira na kuitangaza nchi kiutalii.

Hivyo ni wajibu wetu sote kuyaendeleza na kuyatunza mapishi ya asili ya Zanzibar ili turejeshe hadhi ya Zanzibar inayoanza kupotea kwenye upande huu.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Mohammed Juma Abdullah. Imechukuliwa na kuhaririwa kutoka ukurasa wake wa Facebook.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.