Ilikuwa ni asubuhi ya siku ya Jumapili ya Mei mwaka huu, ndipo nilipopokea barua-pepe kutoka kwa mwanahistori na gwiji wa fasihi ya Kiswahili na msomi wa sanaa, Professa Ibrahim Noor, mzaliwa wa Zanzibar ambaye kwa sasa anafundisha katika Chuo Kikuu cha Mfalme Qaboos nchini Oman, ikiniunganisha na tovuti moja ambayo baada ya kusoma, nilikutana na mstari usemao: “Kufikia mwaka 1906, vichochoro vya Mji Mkongwe vilikuwa na taa za umeme muda mrefu, kabla hata ya London”.

Hiyo ni tafsiri laini na rahisi kwa wenzangu ambao Kizungu chetu ni kichanga cha sentensi isemayo: “By 1906, long before even London obtained them, Stone Town had electric street lights”, kwenye tovuti hiyo.

Hakika, unaposoma tarikh (historia) ya Zanzibar kisha unakutana na mstari mithili ya huu, inabidi urudie kusoma kwa uwangalifu zaidi huku ukikaza macho na kutayarisha ubongo wako kuelewa. Ufupi  wa historia hiyo ni kuwa sio tu kuwa katika suala la umeme, Zanzibar ilikuwa ya mwanzo zaidi ya mataifa mengi ya Afrika, bali pia ilikuwa ya mwanzo kwa ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na usafiri wa treni.

Ni maendeleo ambayo yalitia matumaini sana, wapo wanahistoria wanaokubali hata uchumi wa Zanzibar kwa karne zilizopita ulikuwa mkubwa na wa kupigiwa mfano mbele ya mataifa mengi ya Afrika.

Na Rashid Abdallah

Lakini sasa yote hayo, na mengine mengi ambayo yalikuwepo Zanzibar kabla ya mahali pengine, yanabakia tu katika vichwa vya wanahistoria, tovuti za kihistoria na karatasi za vitabu, sio katika uhalisia, ambako mengine yakiwa hayapo kabisa (kama vile usafiri wa treni), au yakiwepo katika namna ya kusuasua.

Historia hiyo sasa imebaki kama hekaya za paukwa-pakawa na, hapana shaka, wengine wanapata ukakasi wa moyo hata kuziamini kwa sababu ya hali ya sasa ya visiwa vya Zanzibar haiakisi kabisa na historia ya kuwa eti ilikuwa kuwa na uchumi imara kuliko mataifa mengine ya Afrika na hata Arabuni.

Miaka zaidi ya 100 tangu Zanzibar itajwe na sifa hizo lukuki, hivi leo inakumbwa na umasikini sawa na mataifa mengine ya Afrika, huku maendeleo tunaendelea kuyaona kwenye televisheni za kimataifa. Hata yale maendeleo yaliyoachwa karne iliyopita, nayo yamekufa na kufifia. Kwetu sisi yamekuwa mwiko kuyafikia.

Ajabu ni kuwa kila baada ya miaka mitano, wanasiasa hutujia na kauli za matarajio ya kuinawirisha Zanzibar katika kampeni za uchaguzi. Mara ya mwisho ni katika uchaguzi wa 2015, ambapo Katibu Mkuu wa Chama cha Wanachi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, aliwahidi Wazanzibari kuwa angeifanya nchi yao iwe kama Singapore.

Kwa kuwa hadi sasa hajatawazwa kuwa rais wa Zanzibar, licha ya imani ya chama chake kuwa yeye ndiye aliyeshinda uchaguzi huo uliokuja kufutwa baadaye kimizengwe, basi ahadi yake hiyo inaning’inia katika vichwa vya wafuasi wake hadi leo, miaka miwili baada ya uchaguzi huo.

Kinachoonekana sasa ni hadithi tu za wenye tamaa, wakiamini kabla ya mwaka 2020 watachukuwa nchi na Maalim Seif kuwa rais wa Zanzibar. Hizi ni hadithi za sadiki-ukipenda, wakati mwengine wasimuliaji huwa hawana mashiko ila tamaa ni maumbile yetu.

Sijui ikiwa alikuwa na uwezo kweli wa kuifanya Zanzibar kuwa kama Singapore, kama angekuwa rais? Sielewi ikiwa miaka mitano au kumi ingemtosha kufanikisha ahadi yake, lakini kwa kuwa ndiyo hajakabidhiwa hayo madaraka ya kufanya hivyo, unaweza kuhukumu kwamba ahadi yake ya kuifanya Zanzibar kuwa kama Singapore nayo imekwama kwa sababu hiyo..

Pia hajawahi kuiyongoza Zanzibar kama kiongozi mkuu wa nchi, hivyo hatuelewi aina ya uongozi wake ungekuwa wa namna gani, hasa kuelekea katika uchumi ambao ungeisukuma Zanzibar kuwa  Singapore, lakini siku alizoshikilia nafasi za juu kidogo kwenye maamuzi na utendaji kazi, akiwa Waziri Kiongozi katika miaka ya ’80, ushahidi unaonesha kuwa alishirikiana na Rais wa wakati huo wa Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi, kuleta unafuu wa maisha kwa walio wengi.

Kwa upande mwengine, naye Dk. Ali Mohammed Shein aliahidi wakati wa kampeni kuifanya Zanzibar kuwa kama Dubai. Aliyasema hayo, wakati tayari alishapewa dhamana ya kuiongoza Zanzibar akiwa kiongozi wa juu kabisa baina ya 2010 na 2015. Ukiyapima aliyoyafanya ndani ya kipindi hicho cha mwanzo cha utawala wake, unagundua kabisa kuwa maneno yake haya yalikuwa ya kuwapiga watu kamba ili tu wampe kura.

Dubai ya kweli ilivyo, kisha ukilinganisha na hali uchumi wa Zanzibar ulivyo na aina ya uongozi wa Dk Shein, hata angelipewa miaka mingine kumi, basi hatokuwa na uwezo wa kuifanya Zanzibar kuwa kama Dubai.

Dubai? Dubai hii tuiyona kwenye televisheni? Labda miaka kumi atayopewa iwe ya kubadilika kwa kiwango kikubwa mno, huenda anaweza kuona mwanga wa anachokiota. Lakini kwa mwendo huu alionao, hana uwezo wa kuifanya Zanzibar kuwa Dubai.

Alikuwa tu anaongopea watu ili wampe kura. Ndio sifa za wanasiasa kwa siku hizi: kudanganya, unafiki, ndimi mbili, ahadi zisizotekelezeka na mifano mengine mengi, ambayo huashiria undumilakuwili wao.

Siasa za namna hiyo ziko pande zote. Mwanasiasa kukuongopea kwa ajili ya maslahi ya kupata madaraka ni jambo dogo sana kwake. Sio ajabu akasikitika sana akilia ili umpe kura, akipata ushindi pengine hata usimuone akisogea tena mitaa ile kama awali.

Dk. Shein kabakiwa na takriban miaka mitatu na nusu kabla hajaondoka madarakani na kulipisha wimbi la uchaguzi ambalo litaipatia Zanzibar rais mpya. Kiudhati hatujui hapa katikati kabla ya 2020 patatokea nini.

Ila chochote kitakachotokea, kisichowezekana kutokea ni Zanzibar kuwa kama Dubai. Sina uhakika hata huyo Maalim ikiwa ataweza kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ikiwa atapewa nchi kesho.

Muda uliobaki sasa ni mdogo sana kwa maendeleo yaliyo katika nchi ambazo wanadi sera kutoka vyama viwili tofauti walizotaja.

Dk. Shein ndio hawezi kabisa kwa muda uliobaki, na Maalim Seif hata akipewa kesho, basi kuna walakini mkubwa wa kufanikisha kile alichokiahidi, ingawa kwake yeye, tunaweza bado kujenga matumaini kwa sababu hajapata nafasi ya kutimiza ahadi aliyoiweka.

Ikiwa kuna siku atapata hiyo nafasi, ndipo tutakapokuwa na hamu na ghamu ya kuisubiri Singapore ya Afrika Mashariki. Ikiwa itashindikana hata akiwa madarakani, basi tutaelewa kumbe naye ni wale wale tu – wapiga kamba za kisiasa.

Vile vichochoro vya Mji Mkongwe ambavyo huko awali vilikuwa vinavutia sana kwa kupambika na majumba yaliyotulizana, kwa sasa ni tofauti sana. Kuna chochoro ukipita inabidi kwanza urefushe hatua pia ukazanishe mwendo huku macho yako yote yakiwa yanaangalia juu, kwa sababu unapita katika baadhi ya chochoro hatari sana, ambazo zimepambwa na majumba yaliyochoka, yasiyotabirika muda gani yanaweza kuporomoka na kukusaga saga chini.

Unapata picha kuwa ni kama vile Zanzibar inarudi nyuma baada ya kwenda mbele.  Zipo nchi ambazo zilipata uhuru majira sawa na Zanzibar na sasa zimesonga mbele na kuviacha visiwa vyetu pale pale, huku vikiendelea kumasikinika katika baadhi ya mambo.

Tanbihi: Makala hii imechapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Mwelekeo la tarehe 6 Juni 2017.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.