Siku zote dhulma huzaa chuki, chuki ikazaa visasi na visasi vikazaa vifo au ulemavu. Lakini pia inapostawi dhulma, barka hutoweka kwani kimaumbile barka ni tunda la haki. Amani ni miongoni mwa barka ambazo huletwa na uwepo wa haki. Je, wakati Watanzania tukililia amani, tumekumbuka kupigania uwepo wa haki kwa mtu mmoja mmoja au kikundi, iwe cha kijamii au kisiasa? Jibu ni hapana, tumechaguwa kujitia pambani nakukumbuka umuhimu wa amani pale tu, tunaposikia milio ya bunduki.

Leo nimechaguwa kuzungumza moja kwa moja na mkuu wa polisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, IGP Simon Sirro. Nimelichaguwa hili kwa mapenzi yangu kwake na nchi yangu. Nimeamuwa kumpa zawadi na msingi imara ambao kama akiuzingatia, inaweza kuwa sababu ya kuibuka msingi mpya wa kulirejeshea imani iliyopotea jeshi letu la polisi kwenye mioyo ya wengi nchini mwetu. Kupotea huko kwa imani za watu si jambo la bahati mbaya, bali kunatokana na jeshi letu kukithirisha dhulma kwa wale ambao lilipaswa kuwaletea usalama wao na wa mali zao. Ushahidi wa hili hauhitaji tume ya uchunguzi bali hikma na busara ya kawaida sana inatosha kumfanya mtu apate majibu ya uoza huo.

Mitaani tunamoishi muna masahibu na madhila mengi, miongoni mwao ni hatari sana kwa kizazi chenye kuibukia na kukulia humo. Mengi ambayo kizazi hiki hushuhudia kutoka kucha kwa jua hadi kuchwa kwake, kunakifanya kujengeka saikolijia ya kihalifu kuliko kuwa raia wema wenye kutumia akili zao kujitafutia vilivyo vya halali. Je, mtoto ambaye hafiki shuleni, madrassa au kanisani kabla hajakutana na walevi, wacheza kamari, wauza miili (machangudoa), wavuta bangi na unga, unamtarajia aweje? Wala si kwamba polisi hawaioni hali hii, ila kwa vile humu kwenye uhalifu huu ndimo wanamokula, mambo huzidi badala ya kupunguwa, na hapa nitaeleza kwa faida na msaada wangu kwa IGP Sirro.

Na Ahmad Abu Faris

Miezi miwili iliyopita, kuna jirani yangu alifika nyumbani kwangu kunitembelea. Ilikuwa muda wa saa 11:30 jioni, ambapo tulikaa ndani kwa mazungumzo yaliyotuchukuwa kama nusu saa hivi. Tulinyanyuka na kutoka nje kwa lengo la kwenda kumuona jamaa yetu mmoja, ambaye alipata ajali ya pikipiki. Ilibidi tuanze safari yetu toka Buguruni kuelekea Vingunguti Kidarajani. Ghafla mbele yangu nikamuona kijana mfupi mweupe akija kwa kasi ya ajabu. Kutokana na wembamba wa njia, tulilazimika kumpisha apite. Hata hivyo, nilishangaa kijana yule kumvamia mwenzangu ambaye tumekuwa wote ndani kwa zaidi ya nusu saa huku akimwambiya kwamba kamkuta akivuta bangi. Afanaleki!

Madai ya mgambo huyu yalinifanya kuduwaa kidogo kabla ya kumuandama kwa masuali. Aliburuzana na mgeni wangu hadi nilipolazimika kuingilia kati, huku bwana mgambo kijasho na kipovu kikimfufurika mdomo tele! Nilijaribu kumuelewesha mgambo yule bila mafanikio na aliendelea kumburuza mwenzangu kama kwamba amemkamata kwenye tukio la ujambazi. Hali ile iliamsha hasira za raia wema ambao wanamjuwa vizuri kijana aliyekamatwa na wakaanza kumzonga bwana mgambo. Miongoni mwa watu ambao hawakuikubali hali ya kudhalilishwa yule kijana na huyu mgambo ni kaka wa kijana yule ambaye kwa bahati mbaya anauguwa ugonjwa la Kifuwa Kikuu.

Varangati baina ya raia na mgambo lilikuwa kubwa kiasi cha kumfanya mgambo asalimu amri mbele ya umma wenye hasira. Aliondoka na akaahidi kwa kusema “subirini mutaona.” Mimi na yule kijana tukaondoka kwa lengo la kwenda kule tulikokusudia kwenda. Lakini ghafla tukaona kundi kubwa la polisi wenye bunduki wamerejea tena pale raia walipomzonga mgambo na kumkuta kaka wa yule kijana na raia wengine wakijadili tabia mbaya za mgambo wa kituo kidogo cha Buguruni Mnyamani.

Polisi hao wenye bunduki walipofika tu uwanjani pale, wakaanza kumpiga ngumi, mateke kaka wa kijana aliyedaiwa kukutwa akivuta bangi na huku wakijaribu kutishia raia kwa bunduki! Hali ile ilinihuzunisha sana, kwani tukio lile halikuwa na uhalali kwa polisi kufanya waliyokuwa wakiyafanya kwenye macho ya raia, wakiwemo watoto wadogo! Hawa ni polisi toka kituo kikubwa cha Buguruni ambao walishirikiana na mgambo wa kituo kidogo cha Buguruni Mnyamani. Je, nani anawalipa mshahara mgambo hawa au matukio ya kufinyanga kama hili ndio huzaa mishahara yao?

Kipigo dhidi ya kijana yule mgonjwa kiliamsha utungu wa kijana ambaye tulikuwa safarini na ghafla akaanza kukimbilia waliko polisi wale kumuokowa kaka yake. Nilimzuwia lakini hakuzuwilika na kama niliyejuwa, naye alipigwa sana na baadaye wakatiwa pingu hadi Buguruni Polisi. Je, ni lipi kosa lao hadi wafikishwe na kufanyiwa kile walichofanyiwa na polisi kwa uongo wa mgambo? Na je, kweli polisi wetu wapo kwa usalama wetu?

Bahati njema tukio hili lilitokea mbele ya nyumba za wajumbe wetu wawili wa nyumba kumi wa chama tawala. Walishuhudia kadhia ile mwanzo hadi mwisho na bahati njema kwamba wanazijuwa tabia za vijana wale toka utandu hadi ukoko. Hawakuficha hisia za maudhi waliyoyapata na bila kukawia, wakaitana na raia wengine kufanya juhudi za kwenda kuwadhamini wakitilia maanani kwamba mmoja ni mgonjwa ambaye anatumia dozi ya Kifua Kikuu. Baada ya polisi kupewa pesa walizotaka, mabwana wale waliachiwa! Hili ndilo jeshi lako la polisi, IGP Sirro

Mara nyingi tumekuwa tukishuhudia polisi wetu wakipita kwenye maeneo ya kihalifu wakiwa na bunduki zao. Hata hivyo, tunashuhudia pia urafiki wa karibu sana baina ya polisi na watu wanaofanya biashara hizo haramu. Kulikoni!? Hapa niweke wazi kwamba upo ushirikiano wa kutisha baina ya wakuu wa vituo na wauza pombe za kienyeji, bangi, waendesha madanguro na wacheza kamari ambao hufanya jinai hizi mitaani tunamoishi na huku watoto wetu wadogo wakiona uchafu huu. IGP tusaidie.

Haya niliyoeleza ni chembe tu ya dhulma ambazo wengi hufanyiwa, lakini ndio taswira halisi yenye kuakisi uhalisia wa jeshi la polisi kwa wananchi walio wengi. Je, tumekosea wapi hadi kufikia hatua hii ya dhulma ya chombo cha dola kwa raia ambao walipaswa kuwalinda nakuwa na urafiki wa karibu? Inakuwaje leo polisi hapendezi kwa raia mnyonge? Inakuwaje leo polisi anakuwa na urafiki wa kwenda kufata posho kila mwezi kama sio wiki kwa muuza gongo, bangi au dawa za kulevya? Iko wapi amani ikiwa leo polisi anamsingizia raia mwema kesi ili apate pesa!

Kwa kweli, IGP Sirro, dhulma ni nyingi na ndio sababu ya kuibuka mambo mengi ambayo leo twayashuhudia. Gunia hili la misumari umetwishwa wewe sio kwa bahati mbaya bali kutokana na rikodi za utendaji wako. Ushauri wangu kwako ni huu, jiweke karibu kwa raia na weka mlango wazi waje wakueleze matendo maovu ya polisi wetu dhidi ya raia na ukaribu wao na wahalifu. Na kama haitoshi shirikiana sana na wanataaluma kama waandishi wa habari, kwao utavuna mengi ambayo yatakupa mwanga wakumjuwa yupi kondoo na yupi chui. Pia kuna siku polisi wako walinikamata usiku nikiwa nimekaa kwa jirani yangu baada yakutoka kumpeleka mtoto wangu hospitali. Walinifunga pingu kisha wakanifungia kwenye buti la gari yao hadi Buguruni Polisi. Walinong’onezana kisha sikuhojiwa bali niliulizwa nitatowa shilingi ngapi ili niachiwe! Bahati mbaya kwamba niliiwacha familia yangu ikiwa haijuwi kuhusu kukamatwa kwangu na polisi wako wa kanichukulia elfu ishirini yangu. Naomba waulize mwandishi Ahmad Juma anauliza, alifanya kosa gani hadi akamatwe au kukaa kwa jirani kwao ni uhalifu wa kumfikisha mtu mahakamani?

Waakati nikiwa pale kwenye kaunta ya kituo cha polisi Buguruni, nilishuhudia polisi wako wakiuliza “nani ana pesa aachiwe?” Naomba waulize polisi wa Buguruni, wanakamata raia wasio hatia ili wafanye biashara au wanapambana na wahalifu?  Na kama wanapambana nao mbona huingia vibandani mwao nakukuta watu wakinywa gongo lakini wanatoka wao tu huku wakipeana namba za simu na wauza gongo hao au ndio utandawazi wakurushiana kupitia mitandao ya simu?

Na kabla sijaweka kalamu chini, nina kasuali kadogo kuhusu hawa mgambo ambao hukaa kwenye vituo vya polisi nakufanya kazi za kipolisi, jee, mshahara wao wanalipwa na nani, wizara ya mambo ya ndani au ndio kupitia mifuko ya wanyonge wanao wabambikizia kesi. Nakuamini kamanda, shirikiana na raia wema ili kurejesha heshma ya jeshi la polisi. Mungu akuwezeshe.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.