Chimbuko hasa la makala hii ya leo ni tukio la hivi karibuni kisiwani Pemba, ambako mwanafunzi wa miaka 11, Saleh Abdullah Masoud, alifariki dunia siku tatu baada ya kupigwa na kuadhibiwa vikali na walimu wake katika skuli ya msingi ya Laurent International.

Naandika kwa hishima ya Saleh ambaye, kwa mujibu wa mama yake Bi Maryam Saleh Mbarouk, kauli yake ya mwisho ilikuwa ni swali: “Kawaulize walimu wangu niliwakosea nini hasa hata wakanipiga vyote hivi!?”

Maisha yana sadfa nyingi. Wakati stori hii inasambaa mitandaoni na kwenye vyombo rasmi vya habari, ilikuwa naiona ikiwa na machache ya kuhusiana nami, yaani ule mguso wake wa kibinaadamu na ukaribu wake kwangu kwa kuwa imetokea kwenye kisiwa nilichozaliwa na kukulia, Pemba.

Ni baada ya kuona picha ya mama mwenyewe akisimulia na kuhusisha na majina, ndipo nikatanabahi kuwa Saleh huyu ni mjukuu wangu kiukoo, maana mimi na babu yake mzalia mama, Marehemu Saleh Mbarouk, ni ndugu huko kwetu, Shengejuu. Katika uhai wake wote, Saleh Mbarouk akiniiita mimi ‘kaka’, ingawa nilikuwa mdogo sana kwa umri kwake, nami nikimuita hivyo hivyo ‘kaka’.

Kwa hivyo, kuliko mara nyengine zote, safari hii naandika makala ambayo inanihusu binafsi. Mbali ya kuwa mtoto wangu kama walivyo watoto wote wa Kizanzibari, Saleh pia ni mjukuu wangu kwa uhusiano wa kidamu kabisa.

Kifo chake kimetukumbusha ukweli mmoja mchungu sana tunaoishi nao. Ni bahati mbaya sana kwamba yetu ni jamii inayoamini kwenye kutiana maumivu ya kimwili kama moja ya njia za kufunza, kukomesha na au kukomoa. Hili huanza tangu ngazi ya chini kabisa ya kifamilia hadi ngazi ya juu kabisa ya serikali.

Ndani ya nyumba, wazazi huamini kuwa bila mkwaju, watoto hawawezi kukaa sawa. Skuli nako, walimu huamini hivyo hivyo, kwamba bila kuwa na bakora madhubuti mkononi, basi wanafunzi hawatafahamu masomo yao na kuwa na watoto wema. Nao watoto hulichukuwa wazo hilo vichwani mwao, wanapokuwa mitaani, tafauti ndogo kati yao, utakuta inamalizwa kwa kuingiana mwilini. Ngumi zinaruka.

Tabia hii inakuwa hivyo. Imezoeleka. Imekuwa sehemu yetu. Yamekuwa maisha ya kila siku. Sasa hadi tuna serikali ambazo zinaamini kuwa njia bora ya kuwadhibiti wananchi na ‘kuwanyoosha’ – kwa kutumia msamiati wao – ni hiyo hiyo ya kutumia bakora, virungu, mabuti na bunduki.

Ndilo chimbuko la kuwa na makundi ya Janjaweed, Masoksi, Mazombi n ahata vikosi rasmi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na hata utendaji kazi wa vyombo vyengine vya ulinzi na usalama kama vile polisi na jeshi letu. Wote wamejengwa kwenye imani kuwa kutia adabu kimwili na kiakili ndio njia ya kuweka nidhamu na amani kwenye nchi.

Nimekulia kwenye mfumo huu. Nimepigwa tangu nikiwa mdogo kila nilipofanya kile ambacho kilihisabiwa na wakubwa wangu nyumbani, skuli na chuoni kuwa ni jambo baya, au nilipokataa kufanya waliloliona wao kuwa jambo zuri.

Nimepigana na watoto wenzangu wakati wa utoto wangu. Baadhi ya alama za kupigana huko ninazo hadi leo mwilini mwangu. Nimewahi kutumia bakora pia dhidi ya walio chini yangu, wadogo zangu nyumbani.

Hata katika maisha ya kitaaluma, nakumbuka, wakati huo nikiwa mwalimu-mwanafunzi katika skuli za Vikokotoni na Haile Selassie baina ya mwaka 1997 na 2000, aidha nilitumia bakora moja kwa moja mimi mwenyewe au niliwapeleka wanafunzi nilioamini kuwa ni ‘watovu wa adabu’ kwa viongozi wangu wa juu, ambako waliadhibiwa kwa bakora.

Nimeitumia bakora pia katika siku za mwanzo mwanzo za kuwa kwangu kiongozi wa familia, kabla sijaamua kabisa kuiwacha. Watoto wangu ninaowapenda sana, nishawahi kuwapiga mikwaju, wakati huo nikiamini kuwa ndio nawafunza, nawarekebisha, ‘nawanyoosha’.

Kwa hivyo, hapa nazungumzia kitu ambacho nina uzoefu nacho kwa kukitenda na kutendewa kwenye sehemu kubwa ya maisha yangu. Hivi leo naamini kwamba haikuwa sahihi kupigwa mikwaju wakati huo nikijaribu kuuelewa ulimwengu ninaokulia nyumbani kwetu na hata skuli na wala haikuwa sawa kwangu kutumia mikwaju kwa wanafunzi na kwa wanangu.

Wakati simlaumu mzazi wala mwalimu wangu yeyote kwa kutumia bakora kwangu, nikiamini kuwa alifanya hivyo kwa nia njema ya kunitaka nikuwe nikiwa mwana mwenye nidhamu, mimi binafsi natanguliza kuwaomba radhi wanafunzi na wanangu ambao niliwahi kutumia mikwaju kwao kama njia ya ‘kuwanyoosha’.

Huenda, kutokana na malezi waliyopata wao na kunipatia mimi, wazazi na walimu wangu hawakuwa wakijuwa kuwa nidhamu na adabu iliwezekana bila ya bakora. Lakini mimi ninayeishi leo katika karne hii ya 21, natambua kuwa bakora hailei mwana wala haimfanyi mwanafunzi kuwa bora zaidi.

Maisha yamenipa fursa ya kuona na kujifunza mengi yanayothibitisha ukweli huo, na kwa hivyo ninao uwezo wa kubadilika na kuwasaidia wengine kubadilisha fikra zao. Nipige mfano wa somo la Hisabati, ambalo hadi naingia darasa la nane, lilikuwa somo ninalolimudu vyema. Lakini kuanzia darasa la tisa kwenda mbele, nilianguka vibaya kiasi cha kwamba kufikia mtihani wa Kidato cha Nne, hata mtihani wake sikuufanya. Nilijaza namba, nikatoka, na nikaletewa alama ya “F”. Sababu kubwa ni kuwa walimu wa somo hilo kuanzia darasa hilo, walikuwa walimu wakali na wapigaji sana.

Naamini sikuwa peke yangu. Wanafunzi wengi wa miaka ya 1990 hadi 1994 katika skuli za Pandani na Utaani, Pemba, walikutwa na fadhaa hii. Hapana shaka, wako ambao mikwaju waliyocharazwa iliwasaidia kuwanyoosha kwa lazima, lakini kwenye mifano mingi niijuwayo, hali ilikuwa kinyume chake.

Adhabu kali kwa watoto, kama ambavyo imejiri kwa Marehemu Saleh, haiwezi hata kuingia akilini kwamba ilikuwa adhabu ya kumfundisha mtoto mdogo adabu au hata ya kumnyoosha. Hii ni adhabu ya kumkomoa mtoto na kumkomesha kabisa.

Lakini, kama alivyo kwa daktari, mwalimu hana jukumu la kumkomoa mwanafunzi wake. Jukumu lake kubwa na kumtayarisha mwanafunzi huyo kuwa kijana mwema kwake binafsi na kwa jamii yake.

Ukizingatia muda ambao mwanafunzi anautumia akiwa mikononi mwa mwalimu na ule anaoutumia akiwa mikononi mwa wazazi, ni wazi kuwa muda wa mwalimu ni mkubwa zaidi.

Ndani ya muda huo, anapaswa kufundishwa kweli kuwa na nidhamu kwa ajili ya maisha yake, bali hastahili kukomeshwa.

Utumiaji wa bakora na adhabu nyengine ambazo zinakiumiza kiwiliwili cha mtoto hauwezi kamwe kuwa mbadala wa ujenzi wa moyo wa uwajibikaji na nidhamu ndani ya mtoto huyo. Skuli zetu hazipaswi kugeuzwa kuwa kambi za mateso au mafunzo ya kijeshi. Wanafunzi hawapaswi kufanywa mahabusu wala makruta.

Wakati tukiomboleza kifo cha mvulana Saleh kama familia na kama jamii, tunapaswa kuhakiki upya mifumo yetu ya malezi majumbani na mafunzo maskulini. Kama ambavyo siamini kuwa wauguzi na madaktari wetu hufunzwa ujuba wanapokuwa vyuoni kusomea taaluma zao, ndivyo ambavyo siamini ikiwa kwenye vyuo vya ualimu, walimu wanafunzwa kupiga na kuadhibu kama njia ya kuwaweka sawa wanafunzi wao.

Nimesomea ualimu na sikumbuki kwenye mada ya “Kujifunza na Adhabu” kama bakora ilikuwa sehemu ya mbinu tulizofundishwa na walimu wetu.

Sasa ikiwa vyuoni, walimu hawafundishwi kupiga wala kutesa wanafunzi kama ambavyo wauguzi na madaktari hawafundishwi dharau na ujuba kwa wagonjwa, nini basi kinatokea hadi hayo yakawa ndiyo yaongozayo kazi zao wawapo makazini mwao?

Jibu ni kwamba kuna mahala mkufu wa falsafa na nadharia za mafunzo unakatika na kujiunga na vikuku vya shinikizo la kijamii, na jamii ikachomeka nadharia zake kwenye taaluma.

Misemo kama “Punda haendi ila kwa magongo” na hapo punda akafananishwa na mtoto, au “Ng’ombe mkali huchongea kichwache” na hapo ng’ombe kwa mara nyengine akawa ni mwanafunzi, ndiyo inayotumiwa kuhalalisha haya.

Ni kweli kuwa wahenga wetu walituasa kuwa “ukicha mwana kuliya, utalia weye” na “udongo upatize ungali maji”, lakini kuogopea mwanao kulia si kwa kumpagaza korja za mikwaju mgongoni, wala kuupatiza udongo ungali maji, si kwa kumvunja viungo mtoto huyo kwa magongo.

Watoto wetu, kama walivyo watoto wote wa kibinaadamu, ni waelewa. Wana hisia. Wana maumivu. Wana akili. Wana maarifa. Ikiwa lazima kuwaadhibu kwa makosa madogo madogo wanayoyafanya kutokana na utoto wao, basi kuna njia za busara zaidi za kuwanyoosha huko, na sio kuwapiga kama ngoma.

Kifo cha Saleh kiwe sababu ya kukomesha moja kwa moja adhabu za kinyama na mateso dhidi ya watoto wetu. Hata bila ya bakora, bado malezi yetu yanaweza kuwa bora!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.