Kwanza ningetetea yote yatendwayo na utawala wa nchi yangu, tena kwa mitusi yote, vitisho na kejeli, kwa kujikweza wakati tumboni hamuna hali. Ningegombana na kuhasimiana na yeyote ili nionekane nami pengine wanifikirie pakuniwekani.

Ningekuwa kada, ningeuvua utu, nikayajua matusi yote ya dunia, nimtukane kila kiongozi wa upinzani na chipukizi wao. Niwabaguwe wote wenye msimamo tafauti nami kwa rangi zao, aila zao na hata urefu au ufupi wao. Ili uwe kada lazima macho uyaweke utosoni, moyo uugeuze barafu na huruma uziweke kandoni. 

Ningekuwa kada, nisingejuwa cha halali au cha haramu ilimradi tu mkono unakwenda kinywani. Ningelijivesha mabendera na kujizonga mwili mzima, nionekane. Waniogope jirani, rafiki na kila mwenye upeo wa kufikiri akaye kimya akiniona,  asifurukute kichwani. Si unajua kunyea ndooni ndicho kiburi kilicho kifuani!? 
Ningelikuwa kada, ningezidi unafiki. Siko huku, siko kule,  ilimradi tu kama fisi nasubiri nami langu pande nipumue jua la mnazini. Jana mpinzani leo ukadani, nanunulika kwa fungu hadi mkiani. Ukada ni maslahi kwanza, huna rafiki wa kudumu na adui ni yeyote mwenye mawazo huru, mwenye hoja na uwezo wa kufikiri. 

Usingenijua kama ndiye mimi nilielewa na kukuzwa katika Uislam kwa jinsi ya uchafu wa kinywa changu. Nisingechaguwa wa kumtumia. Kwani Mungu ni nani? Nipande kiririni kuna jabari kama mimi? Mibwege inanijuwa kwa kuseka watu ndani.
Ningekuwa kada, basi adui mkubwa wangu angekuwa Mpemba, tena niwatukane hasa kama hayawani na wale machotara hasa wa damu ya Hizbu. Ningebeba bango kumpokea Mtukufu, nikimkumbusha kuwa ni mimi Bakari Upinde nisiyependa yoyote, mwenye gubu la roho, choyo, hasadi kwa yoyote mwenye nuru ya mawazo na ukweli. Tena ningemshauri Bwana Mkubwa tukatengeneza hasa kiwanda cha mbata tukatumbukiza hawa wanaotunyima kura waliozidi mjini.

Ningekuwa kada, ningefurahi wanapofukuzwa makazini nisiowapenda kwa sababu ya uhuru wao wa mawazo. Ala! Si wanajitia kutaka demokrasia, wakati sisi tulipindua tufanye tuyatakayo!? Ningevunja kila kipembe chenye biashara za mahasimu hawa wa upinzani na kama ninaweza ningewafukuza hawa marangirangi, machotara, magabacholi wote visiwani na kuwatupa huko mchangani, nanibaki hasarani.

Ningekuwa kada, ama ningejitahidi kula nisishibe hasa. Sina kizibo kama pakacha na maji. Halijazwi likajaa. Na ahoji mtu rekodi yangu safi ya ulaji, aone kama atakaa tena nchini. 

Kwani hawajui ukada ni leseni ya kufanya nitakalo? Uniseme kwa kula kwani tumbo si langu mwenyewe? Ningekula mpaka nikadidimia hasa kama kibwengo cha Mkamandume au cha Kizingo au kule Ngazimia kwa Baniani.

Ningekuwa kada, ningefanya nami nionekane, adui wangu ni wale wadogo walionizidi hasa kwa elimu, uwezo wa kufikiri na kipaji cha kusema ukweli. 

Ningewachukia walioko Ulaya hasa hata kama wamejazana tena barazani na Jumba la Mtukufu wakiwa sogani. Ala! Wao wale bure huko watokako kwa Wazungu halafu watuulize siye tunashiba vipi? 

Ningekuwa kada, ningekuwa na roho ya korosho. Ukiniona, nimekunyaa kwa chuki, hasadi na shari, nikipanga hasa nani wa kumdhuru mara hii ima kwa roketi au guruneti. 

Ningekuwa kada, haki nisingeitambua japo nasali mara ihdaa wa ishirini. Ningekuwa mbele kufuta matumaini ya walio wengi hasa kwa chaguo lao la kuwaongoza ili kuonyesha tu ladha ya ubabe na umakini wa shari iliyo moyoni. Ndani ya roho yangu, Mzungu huniita ‘coward’, yaani jitu joga lisilo mithali. 

Tena basi, huumia hasa nikiambiwa ukweli, lakini kinachoniweka mjini ni mitusi tu niliyoibeba kwa sababu tu ya chuki za rohoni. 

Ningekuwa kada, nisingeridhika na chochote zaidi ya kuwaona watu wote Masikini. Niwashinde tu, hata kwa kubadhi la msikitini langu liwe la jivujivu wengine miguu chini. Nisingepumzika kwa roho yangu mbaya. Ningeumia kwa maradhi ya moyo kwa sababu tu ukada ni maradhi makubwa zaidi ya roho na nafsini. 

Ningekuwa miongoni mwa madhalili wakubwa wasiofahamu ihsani. Kila nimuonapo Mwalim Seif kanawiri, basi sawa na jiti lililo rohoni, ningezuia TV, redio na kuomba kuzima hili balaa la mitandao inayonikaa rohoni. 

Ningekuwa kada… 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.