Familia ya kijana Salum Mohammed Almasi aliyeuawa na jeshi la polisi jijini Dar es Salaam katikati ya mwezi uliopita kwa tuhuma za ujambazi, imeendelea kumuandama Mkuu wa Polisi, IGP Simon Sirro, wakimtaka kuchukuwa hatua za haraka kulisafisha jina la ndugu yao kabla hawajamzika, kumuwajibisha askari aliyefanya mauaji hayo, sambamba na kuchukuwa hatua za kurekebisha kile wanachokiona kama tabia ya jeshi hilo kuwalenga watu kwa “sababu ya mavazi na sura zao.”

Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana, mjomba wa marehemu, Thulayha Mohammed Abdulrahman, amesema kwamba familia yao haikubaliani na maelezo ya tukio iliyotolewa na IGP Sirro, wakati huo akiwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ambayo yalijaribu kumtia hatiani ndugu yao na kuwavua lawama askari waliohusika na mauaji hayo.

Hadi sasa, maiti ya Salum Mohammed Almasi imeendelea kusalia kwenye chumba cha kuhifadhia maiti na familia yake imegoma kumzika hadi uchunguzi huru utakapofanyika na jina la kijana huyo aliyekuwa msaidizi wa imamu, mwalimu wa dini ya Kiislamu na pia mwanafunzi wa Diploma ya Teknolojia ya Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, litakaposafishwa.

“Hatuwezi kumzika Salum kama jambazi, kwa kuwa huyu si jambazi. Tunataka kumzika Salum kama mtoto wetu, mcha Mungu na kijana aliye safi,” inasema taarifa ya familia hiyo.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.