Hakuna mtu mwenye  akili timamu ataunga mkono tukio la hivi karibuni mjini Unguja ambapo watu sita walichomwa visu. Haihitajiki nguvu nyingi za kufikiria ili uelewe kuwa kilichofanywa sio sahihi.

Licha ya tukio lile kuumiza, pia mapokezi ya tukio yanasikitisha na kuumiza vile vile. Wapo ambao mara moja walianza kuichoma visu vya udini Zanzibar, wakiilaumu imani ya wengi wa watu wa Zanzibar kuwa ndio chanzo.

Wengine wakaja na hekaya ya ajabu sana, wakisema; ndio madhara ya kulazimisha watu kufunga.

Ni kauli ya ajabu, mtoa povu wa namna hii unapata shida kumuelewa ikiwa kaelewa kilichotokea au uwezo wake wa kufikiri ni mdogo,  ni maneno ya  uongo ndani ya uongo.

Kwanza hakuna mtu kalazimishwa kufunga Zanzibar. Pia majira ya tukio lilipotokea (saa moja za jioni) katika mgahawa wa Lukman Mkunazini, halina kabisa uhusiano na kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani.

Na Rashid Abdallah

Nilipitia ukurasa mmoja wa habari nikakutana na maoni mengi yasiyoingia akilini,baada ya ukurasa huo kuiweka habari ile, mtu mmoja anasema: “Kwani wenzetu Zanzibar hawana upendo kwa wenzao wa dini zingine mbona bara kuko shwari”.

Kwani nani kamwambia  tukio la watu kuchomwa visu ila uhusiano wa chuki za kidini? Mtu aliyechoma visu usiku, tena akachoma visu raia wa kigeni na raia wa ndani. Mbona uhusiano wa dini na tukio hili haupo!

Unaweza kuhisi mtoa maneno hayo , ni mpinga udini lakini ukweli sio mpinga udini ila ni ‘mdini’, kwa sababu hakuna njia yoyote ya kuhusisha tukio la kihalifu na imani ya watu wengine, ikiwa huna chuki na imani hiyo.

Nimekutana na watu katika kutoa maoni yao wanausukumia lawama Uislamu moja kwa moja. Pengine wanaelewa dini ya mtuhumiwa, sawa.

Lakini swali la msingi linakuja; mtuhumiwa ndivyo alivyodai kuwa ameshambulia kwa visu kwa sababu ya imani yake? Jawabu rahisi ni kuwa hajasema hivyo, sasa ukijitokeza wewe mhusishaji wa tukio lile na dini, ndio naanza kuziona chuki zao.

Walimwengu wanaelewa mauaji ya kutisha aliyoyafanya Adolt Hilter kiongozi wa Kinazi wa Ujerumani, huko Ulaya, pia inaeleweka alikuwa mfuasi wa dini gani, lakini ni ujinga kuhusisha dini ya Hitler na unyama alioufanya.

Si yeye tu, hata Mfalme Leopold II wa Ubelgiji ambaye aliendesha mauaji ya Waafrika wasiopungua milioni 10 na meteso ya watu kuachwa mikono vibutu katika taifa la Congo, pia walimwengu wanaelewa alitokea dini gani. Lakini vile vile ni ujinga kuhusisha imani yake na unyama alioufanya.

Kuna mambo mawili hapa ni lazima tuyaelewe. Moja: Kuna watu hutumia imani ya dini kufanya vitendo viovu katika jamii zetu. Watu hawa wako katika dini zote, hufanya kwa sababu ya chuki ama ujinga na kuzitumia dini kama  kisingizio.

Ukienda India utakutana na Wahindu wa misimamo mikali, ukila tu Ng’ombe wanakutoa uhai, kwao Ng’ombe wanamuabudu. Mnyanmari wapo Mabudha wa siasa kali wanachinja na kuuwa jamii ya Rohingya, wanaisafisha ardhi yao ili isiwe na wafuasi wa dini nyengine isipokuwa wao tu. Mashariki ya Kati yapo makundi ya Kiislamu wanachinja na kuuwa pia nao kisingizio kikiwa ni dini.

Ukisogea kwa majirani zetu hapo, nchi za Afrika ya kati utakutana na makundi ya Kikristo yanafanya unyama wa kutisha kwa kisingizio cha dini yao.

Hata Mayahudi-Mazayuni wa siasa kali wapo, ndio hao wanaonyanyasa na kupora ardhi, sababu yao kubwa ni kuwa kitabu cha dini yao ndio kinawapa nguvu.

Jambo la msingi kuelewa kuwa katika imani zote kuna watu wakorofi, ambao huzitumia imani kama ngazi ya kutendea maovu. Mara nyingi hutokana na uelewa mbovu au hata chuki tu ambazo mtu hujifunza kutoka kwa viongozi wake.

Ukiwa unaelewa kuwa dunia iko hivyo, wala hupati tabu ya kumuoneshea kidole mwenzako, wakati imani yako unaelewa wazi kuna watu wanaitumia vibaya.

Pili: Kuna watu ambao ni wafuasi wa dini fulani, hutenda maovu lakini hawatoi madai kuwa imani ndio zimewasukuma kutenda hayo.

Ikiwa vikosi vyetu vya usalama vinarikodi wahalifu  na ufuasi wa dini zao, naamini utakutana na wahalifu wa dini zote.

Kundi hili la pili  tunao wengi katika jamii zetu, na ndio sawa na kile kilichotokea Zanzibar. Aliyefanya tukio la kuchoma watu visu, hakueleta madai kuwa dini yake ndio imemsukuma kufanya hivyo.

Jambo la ajabu na la kusikitisha ni kuzuka baadhi ya Watanzania wenzetu wakaanza kupiga zumari za udini. Wakati tukio halihusiani na imani, kipi sasa kikufanyacho kulipigia chapuo la udini; kama si chuki dhidi ya imani ya wengine?

Kuhusisha imani ya mamilioni ya watu kwa tukio la mtu mmoja ambaye amefanya kwa sababu zake binafsi, mimi sioni usahihi wa kufanya hivyo!

Eti kwa sababu anatokea sehemu fulani, kule kuna watu wengi wa imani fulani na kipindi hiki ni cha Ramadhani, basi moja kwa moja ni dini yake tu ndio iliyomsukuma. Fikra kama hizo ni za kijinga , narudia tena ni za kijinga!

Na huo ndio udini kabisa, tena ni udini wa mwenywe chuki na dini ya wengine. Hatuwezi kupambana na wahalifu kwa kuanza kutengenezea hukumu za ajabu ajabu kama hizi, kuhukumu matukio kwa sababu za kieneo na kiimani?

Katika hali kama hii, jambo kubwa na la msingi ni wapenda amani kuwa kitu kimoja, sio kubuni vitu vya uongo ambavyo havina faida kwako wala jamii.

Ambaye anatumia imani kufanya ukorofi ni lazima kusimama pamoja kupingana naye, pia yule ambaye hatumii imani kufanya ukorofi basi kusitokee watu wakaanza kutengeneza hadithi za kusisimua za kuhusisha imani yake na unyama anaoufanya.

Tusianze kuyaangalia mambo kwa macho ya chuki za kibaguzi na udini, kwani tukianza kuiyona imani fulani ni tatizo katika jami, ikae akilini kitakachofuata ni kuwachukia wafuasi wa imani ile.

Na katu hutojenga jamii yenye mtangamano na mahusiano mazuri ikiwa unawaona wengine ni tatizo kwa sababu ya imani zao, hata mapenzi na utulivu wao huujali tena. Tusifike huko jamani!

Tukio la kihalifu libaki kuwa la kihalifu bila kulipamba na imani ya mamilioni ya watu.

La muhimu ni polisi kuimarisha ulinzi na mbinu za kisasa kupambana na wahalifu, ili hawa wachoma visu vya vyuma wadhibitiwe, pia jamii yetu iwe pamoja kupambana na hawa wachomaji visu vya udini kwenye migongo ya imani za wengine.

TANBIHI: Makala hii imechapishwa kwa mara ya kwanza nagazeti la MwanaHalisi la tarehe 5 Juni 2017

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.