Kuna video inasambaa kwenye mitandao ya kijamii tangu katikati ya mwezi Mei mwaka huu, ikimuonesha Mmanga (Mwarabu) anampiga mwanamke kwa sapatu, lakini hatuelezwi na hiyo video huyo mwanamke ni nani, ni wa kabila gani, ana jisia gani, wala amefanya kosa gani hadi kupigwa, na wala hatuelezwi ana uhusiano gani na huyo Mmanga. Hatujui kama ni mfanyakazi wake au ni mwanawe wa kumzaa.

Tunachokiona kwa dhahiri ni kuwa huyo mzee wa Kimanga amepandwa na hamaki na anampiga kijana wa kike kwa sapatu. Hakuna mtu yeyote mwenye moyo wa huruma anayependezewa kuona kitendo kama hicho kutendwa hadharani na hata kwa siri. Wala hakuna anayeweza kukanusha kuwa mambo kama haya hayatokei duniani. Ni nini basi kinachopingwa na watu waadilifu wenye uwezo wa kutumia akili zao na wanaojua nyuma ya mijadala ya aina hii kuna nani hasa?

Miongoni mwa wasambazaji wa video hiyo katika mtandao wa kijamii wa Facebook, ameandika “Mukiambiwa wamanga munakataa na kusema uwongo wakati video inajieleza!” Na mwengine, ambaye inaonekana video yenyewe ndiko kwanza ilikokuwa imetumwa, ameiambatanisha na maneno haya: “Hasbialwah waneemal wakeel. Nyie baadhi ya waarabu kesho kwa Allah mtapata adhabu kubwa Sana Wallah! VP unampiga mtumzima kiasi hivi km MTT mdogo wallah na Tena unamdhalilisha mbele ya wtt wadogo kiasi mi mfanyakazi wa ndani Tu? Allah atawapa adhabu zenu Wallah.”

Kwa ujumla, wote wawili, pamoja na baadhi ya wanaochangia kwenye video hiyo, wanawanyooshea Waarabu peke yao duniani kuwa ndio walio watu waovu kabisa wenye kutenda matendo kama haya na kuendelea kwa kuwalaani na kuwabashiria moto Siku ya Kiyama.

Ukiwa ni Mwarabu na unakhofu kutiwa motoni, huna budi kumshukuru mwandishi kuwa ametumia maneno “baadhi ya waarabu”, kwani asaa baadhi ya Waarabu wakanusurika na huo moto. Juu ya utumiaji wa maneno “baadhi ya Waarabu” aliyoyasema mchangiaji mmoja yanabakia kuwa “Nyie baadhi ya waarabu kesho kwa Allah mtapata adhabu kubwa Sana Wallah!” kama kwamba hakuna watu wowote wengineo duniani wanaotenda ya ukatili na maovu mengineyo watakaotiwa motoni ila “baadhi yenu Waarabu”. Hili ndilo linalopingwa na wasomaji wengi kabisa wenye kutumia akili zao na ni watu waadilifu.

Lakini tusistaajabu kwa nini mwenzetu naye amefika hadi ya kuona hakuna watu waovu duniani ila ni Waarabu peke yao, kwani tokea utotoni na kwa makusudi shule za Tanzania husomesha propaganda za udini dhidi ya Waarabu. Pitia vitabu vya historia vinavyosomeshwa shuleni huko na utazikuta propaganda hizo zimejaa, na kama walivyonena wazee wetu kuwa “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.” Tumepikwa katika propaganda hizi na tumepikika vibaya sana.

Vitendo viovu haviwezi kuhalalishwa na mtu yoyote mahala popote duniani. Mwenye kujaribu kufanya hivyo huwa yeye mwenyewe ni katika waovu. Wala hatuna haki ya kuvichukua vitendo hivyo vilivyotendwa na mtu mmoja au watu wachache na kusema hivyo ndivyo watu wote wa nchi hiyo au umma huo walivyo. Hili la kuwatupia lawama Waarabu wote kwa vitendi vya wahalifu wachache ndilo linalopingwa na wenye kuweza kutumia akili zao. Wala hawasemi kuwa Arabuni hakuna wanaotenda maovu.

Propaganda kali sana inayotumika ni kuwa hakuna watu waovu duniani kuwashinda Waarabu kama kwamba Afrika na Ulaya na kwingineko hayatendwi maovu kama hayo na zaidi ya hayo. Na nini hasa lengo la propaganda hizi? Ukifanya utafiti mdogo tu, kwa kutumia akili yako, utagundua mara moja kuwa kinachotaka kusulubiwa hasa wala si Waarabu bali ni dini ya Kiislamu waliyoileta Afrika. Msikilize vizuri nini amesema Mhishimiwa William Lukuvi alipohubiria kanisani na wahishimiwa wengineo wa Kikristo utazisikia chuki zao dhidi ya Uislamu waziwazi.

Hapa naweka video nne, ambazo licha ya kuwa watendaji uovu ndani yake ni Waafrika na Wazungu, hatusikii kuhusishwa Waafrika wala Wazungu wote na uovu huo.

Video ya Kwanza:  Mfanyakazi wa ndani nchini Uganda akimtesa mtoto mdogo 

Video ya Pili: Mwafrika kutoka Ethiopia aliyemchinja mwajiri wake mwanamke wa Kiarabu aliyekuwa na mimba

.

Je, tuna haki ya kuwatupia lawama Waafrika wote duniani kwa kosa la mtu mmoja au watu wachache? Jawabu ya kiuadilifu ni kuwa: Hatuna haki hiyo. Lakini hivyo ndivyo wafanyavo wanapropaganda za udini na wale waliotekwa kiakili na propaganda hizo katika kuwatupia lawama Waarabu wote kwa kitendo cha mtu mmoja.

Video ya Tatu: Kundi la Watanzania lachukuwa sheria mikononi kwa mwanamke anayetuhumiwa kushirikiana na majambazi

Katika video hii iliyochukuliwa Tanzania Bara inaonesha vipi umma ulivyotokwa na utu na ubinadamu. Si kuwa wanamchukua mwanamke na kumpeleka polisi au wanamchapa tu, bali wanampiga mawe na mwishowe wanamchoma moto.

Hakuna hata mmoja aliyesimama na kusema “mfanyayo si sawa wala si haki.” Wote waliokuwepo ama walisherehekea au walishiriki katika unyama huu. Kisa nini? Eti alishiriki katika wizi. Sielewi vipi Mtanzania yeyote mwenye akili timamu anaweza kuwa na ujinga wa kuwanyoshea wengine kidole cha lawama na kujigamba kama kwamba kwao wanaishishi malaika watupu!

Video ya Nne: Mwanamke wa Kiafrika ashambuliwa kwa bilauri ya bia Marekani kwa kuzungumza Kiswahili

 

Kwa mifano hii na mingine mingi zaidi ya hii, hatuwasikii wanapropaganda kuyazungumzia wala kuwapaka Wakristo wote kwa kosa la mtu mmoja. Sawa kabisa. Hivyo basi, ikiwa hili wanaliona ni sawa, basi haki hiyo hiyo ya kutokuwalaumu wote kwa kosa la mtu mmoja waitumie pia wanapozungumza juu ya Waarabu na Waislamu.

Tukumbuke pia kuwa kwa kila video moja ya ubaya uliotendwa na Mmanga mmoja tunaweza kusambaza video mia na moja za ubaya uliotendwa na Waafrika, Wazungu na wengineo.

Sasa, ilivyokuwa tunaelewa vizuri sana kuwa wema na waovu wako kila mahala, tunaelewa pia kuwa kuwalenga Waarabu kama kwamba ndio peke yao waliokuwa watu waovu duniani, ni siasa chafu sana za kutaka kutufitinisha na ndugu zetu kwa makusudi.

Kwa wenye akili na kuelewa undani wa hizi fitina wanajua fika kuwa kinachotaka kusulubiwa hasa wala si Waarabu, bali ni Uislamu. Lakini wenye kutapakaza chuki ni mijoga kweli. Hawatoki waziwazi na kusema “Waislamu watu waovu sana” bali wanajificha nyuma ya pazia la kuwasulubu Waarabu.

Tumeshawatambua. Lakini hawatafuzu katika siasa zao chafu zilizojaa fitina zenye kutaka kutugombanisha na kutufarikisha ndugu kwa ndugu. Inasikitisha pia kuwa kuna ndugu zetu waliokuwa bado hawajazitambua siasa za hawa mashetani zikoje.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Mbaraka Mwadini. 

One thought on “Wacheni propaganda, ukatili hauna kabila wala dini”

  1. Hapo Darisalama yapo matukio kaa yanayowaripoti mama wenye nymba wakiwatesa wasichana wao hakazi, wengine hadi kuwaunguza kwa pasi na kuwafuma kwa njiti za fyagi. Lakini hisikii kuchanganywa jamii ya watu fulani kuwa ni makatili.
    Ila akufanya mmanga mmoja Waarabu, na itakuzwa hiyo mpaka ionekane kanakwamba katika jamii ya waarabu hakuna mwema.
    Lakini utashangaa tusivyo na haya wala vibaya mabaya yote tunayowasukumia Waarabu, kidogo utaona tushapanda dege kwenda kutoa nyuso zetu mbaya kuomba

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.