Anuani ya mjadala huu inalazimika kuwa refu kutokana na haja iliyopo ya kufafanua na kuweka wazi utata uliopo katika jamii na siasa za Zanzibar ambazo zimefanywa kuwa na utamaduni wa kuakisi utata huo.

Mchanganyiko na au muingiliano wa kijamii wa watu wa visiwa vya Zanzibar ni matokeo ya hali yake ya kieneo, ambapo pepo za msimu ziliziwezesha mara kwa mara jamii za Waarabu kutoka Bara Arabu na Wahindi kutoka India kuvuuka kwa kutumia Bahari ya Hindi na kufika Zanzibar kwa ajili ya shughuli za kibiashara, kilimo na hata kuowana na wenyeji na wakaazi wa visiwa hivi karne nyingi zilizopita. Suala la maingiliano ya kindoa lilitiliwa mkazo sana na jamii za Waarabu kuliko jamii ya Wahindi ambao mara nyingi walibaki kuwa na ukaribu mkubwa na jamii zao za asili.

Mabadiliko ya kijamii na kiuchumi katika makundi mbalimbali ya kijamii visiwani Zanzibar yalikwenda sambamba na mabadiliko ya kijamii kutoka katika jamii za wakulima waliofuata mfumo wa ujima na kuwa katika jamii zilizofuata mfumo wa utumwa, ambazo kwa umaarufu zilikuja kutambulika kama jamii za miji ya Waswahili katika maeneo ya upwa wa Afrika Mashariki, na kupelekea mabadiliko makubwa kutoka katika jamii za kijadi au ujima kuelekea katika jamii za matabaka yaliyoibuka katika visiwa vya Zanzibar kama yanavyoelezwa na mtaalamu wa historia, Bwana Fredrick Enge, katika uchunguzi wake kuhusu maisha ya binaadamu. Jamii hizi za mwambao wa Afika Mashariki hatimaye zikabadilika na kujikita katika mifumo ya kibwanyeye, ambayo ilihusisha mabanyenye wenye asili ya Kiarabu waliofungamana  na utawala wa Kisultani wa Kiomani.

Kuanzishwa na kuamarika kwa utawala wa Kiomani dhidi ya mabwanyenye na madai yake ya baadaye kutaka kujinyakulia maeneo ya Mwambao wa Afrika Mashariki na maeneo mengine ya misafara ya kibiashara hadi katika maeno ya Manyema, mashariki mwa Kongo, katika karne ya 19, ni maeneo muhimu katika mjadala wetu huu, hasa kutokana na utata ulioibuka na kuendelea hadi leo.

Utata na au ubishi upo baina ya Wanzibari ambao wanachukulia uwepo wa Waomani katika Zanzibar kama aina ya ukoloni uliokuwepo kabla ya kuja kwa wakoloni wa Kizungu kutoka Ulaya ambao hatimaye waliunganisha nguvu na Muingereza kuanzisha aina fulani ya ushirika wa kiukoloni dhidi ya Zanzibar na wenyeji wengine wa visiwa hivi wanaohoji kuwa utawala wa kifalme wa Zanzibar ulikuwa tayari umefanana sana na utamaduni wa Kizanzibari pamoja jamii yake katika miaka ya 1960.

Kundi linaloamini mtazamo huu linasisitiza kuwa utawala wa Kiomani ulimalizika ramsi mwaka 1890 wakati Zanzibar ilipofanywa kuwa Mahamiya na serikali ya Kiingereza ambapo Usultani ulikuwa tayari umepunguziwa mamlaka na nguvu za kiutawala. Huu ni mtazamo wa muungano wa vyama vya ZNP/ZPPP ambavyo vilipinduliwa katika Mapinduzi ya 1964.

Matokeo ya msuguano huu yalikuwa ni kukataa kwa sehemu kubwa ya Wazanzibari walioongozwa na Mzee Abeid Karume katika kuukubali na kuutambua uhuru wa Zanzibar wa tarehe 10 Disemba ulitolewa na Uingereza. Msimamo huu wa wafuasi wa ASP uliungwa mkono vikali na kwa haraka na Mwalimu Julius Nyerere na chama chake cha TANU, ambao walichukulia Usultani wa Zanzibar kama masalia ya Ukoloni wa Kiarabu.

Ukiongozwa na fikra hizi, uongozi wa Tanganyika wa chama cha TANU ulitoa kila aina ya msaada kuunga mkono mtazamo wa ASP ulioshikilia dhana ya Jamhuri ya Waafrika  Weusi. Mwandishi, Dk. Harith Ghassany, ameonesha kuwa msaada wa Tanganyika ulihusisha nguvu kazi ya wafanyakazi wa mashamba ya Mkonge kutoka mkoa wa Tanga katika kufanikisha Mapinduzi ya Zanzibar. Utafiti wa  hivi karibuni unaonesha kuwa askari wachache wa jeshi la Tanganyika (King African Rifles) walitumwa kutoka Dar es Salaam kufankisha jaribio la kuipindua serikali ya Zanzibar.

Nadharia ya utatu wa utaifa unaodokezwa katika muktadha huu inahusisha utaifa wa Jumuiya ya Waafrika na mshirika wake Jumuiya ya Washirazi wanaounda chama cha ASP na utaifa wa washindani wao, chini ya mwamvuli wa muungano wa ZNP/ZPPP, ambao pia unahusisha katika moja ya matawi yake Jumuiya ya Waarabu pamoja na tabaka la Washirazi kutoka Unguja na Pemba katika mtiririko wake.

Wakati tawi la Washirazi na lile la Waafrika wa ASP yakiunganishwa na hisia zao za kumpinga Sultani (Utawala wa Kiarabu), Washirazi wao, hata hivyo, walikuwa na hofu na mashaka juu ya msukumo na ushawishi wa Wazanzibari wenye asili ya Tanganyika katika uongozi wa Zanzibar. Walijiona wao kama vile ni wakaazi halisi wa Zanzibar, licha ya kudaiwa kuwa kwao kuwa na uhusiano na vizazi vyao vya Kishirazi.

Matabaka haya mawili ndani ya ASP baadaye yalipelekea kujenga chuki zilizovuka mipaka baina yao,  ambapo ilipelekea kuchukuliwa kwa hatua kali kwa Washirazi waliotuhumwa kumuunga Othman Shariff ndani ya Serikali ya Mapinduzi. Othman aliunda Tawi lake la Vijana (YASU) ndani ya ASP miaka mingi iliyopita kabla ya Mapinduzi. Umoja huu uliwaunganisha vijana na ulitoa changamoto na ukosowaji mkubwa kwa uongozi wa Mzee Karume ndani ya ASP,  jambo ambalo hatimaye lilipelekea migogoro mikubwa.

Licha ya ukweli kuwa ASP kilikuwa chama kilichoungwa mkono sana na wafanyakazi visiwani Zanzibar, chama hicho kilipoteza mwelekeo baada ya kushikilia mitazamo ya kiubaguzi wa rangi iliyoegemea zaidi chuki dhidi ya Waarabu chini ya kivuli cha kuupinga Usultani.  Ilipofika miaka ya ’50, misimamo hii ilikipelekea chama hicho kutoa upinzani mkali kwa utawala wa Kiingereza kwa kudai kuwa utawala wa Kiarabu wa Sultani ulikuwa wa kiuadui sana kwa Wazanzibari. Ni kwa msingi huu huu, ASP ilianzisha mahusiano ya karibu sana na utawala wa Kizayuni na kupelekea viongozi weengi wa ASP kupelekwa Israel kwa ajili ya kuandaliwa na kupikwa kisiasa.

Katika muktadha huu, Mwalimu Nyerere na chama chake cha TANU alikumbwa na aibu na ukosoaji mkubwa katika kongamano la PAFMECA na Jukwaa la Waarabu wa Asia walipohoji kwa nini ASP walianzisha kampeni ya kupinga kutolewa uhuru wa Zanzibar chini ya kauli mbiu ya “Uhuru Zuia” kwa madai kuwa Zanzibar haijawa tayari kupokea uhuru mpaka pale itakapokuwa na wasomi watakaokuja kuiongoza Dola ya Zanzibar.

Nyerere alijibu tuhuma hizo kwa kupendekeza mkataba maarufu wa TANU/ASP mwaka 1959 chini ya usimamizi na uangalizi wa PAFMECA kusaidia ASP kwa nguvu kazi ya wasomi na makada weledi, wakati pande hizo mbili zikiahidi kuziunganisha nchi mara tu baada ya kushika hatamu za dola kupitia njia ya chaguzi.

Hata hivyo, historia ilichukua mkondo tofauti baada ya madai kuwa ASP haikutakiwa kuchukua uongozi katika serikali ya Zanzibar kutokana na udangannyifu uliofanywa katika chaguzi ambao ulidaiwa kutoa upendeleo kwa muungano wa ZNP/ZPPP.

Vile vile, Abdulrahman Babu aliwahi kuulizwa kwa nini alijiunga na ZNP badala ya ASP alipowasili Zanzibar akitokea Uingereza mwaka 1957, naye akaeleza kuwa hakuweza kujiunga na ASP kwa wakati huo ASP ilikuwa ikiunga mkono madai ya kupinga kupatikana kwa uhuru, jambo ambalo lilipingana na shabaha ya harakati za kumkomboa mtu mweusi ambazo alikuwa akishiriki nchini Uingereza na wanaharakati maarufu waliopinga ubaguzi dhidi ya watu weusi kama vile George Padmore and W.W. DuBois, ambao alifanya nao kazi pamoja katika Kamati ya Kupigania Uhuru. Suala la muhimu zaidi ni kuwa mtazamo wa Babu ulikuwa ikipinga zaidi matabaka ya kijamii kuliko tofauti ya rangi na asili zilikuwepo katika jamii ya mchanganyiko ya Zanzibar.

Wakati tunaelekea tena kuadhimisha tukio la Mapinduzi ya Zanzibar,  hatuna budi kuelewa uhusianoa wa Mapinduzi ya Zanzibar na dhana nzima ya utatu wa utaifa ambao umeharibu na kuigawa jamii ya Zanzibar kiasi ambacho imeshindwa kufikia mardhiano kuhusu matokeo matatu ya dhana nzima ya utatu katika utaifa wetu ambayo ni Uhuru wa Disemba 1963, Mapinduzi ya 1964, na Muungano wa Tanganyika wa Apili 1964.

Kwa kumalizia, mtu anaweza kuona jinsi gani watawala hawako tayari kukubali matokeo halali ya chaguzi za kidemokrasia visiwani Zanzibar na badala yake kuchukua hatua ya kujiweka madarakani kama ithibati ya kutokukubali kuelewa dhana ya utatu wa utaifa wetu ambayo imeingiza misukosuko na historia chafu katika siasa yetu.

TANBIHI: Hii ni tafsiri isiyo rasmi ya makala ya Bwana Salim Msoma aliyoiita “Tripple Nationalism”. Bwana Msoma ni Mzanzibari ambaye amewahi kuhudumu kama afisa wa ngazi za juu katika Serikali ya Tanzania.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.