Panza ni moja ya visiwa vinavyounda nchi nzima ya Zanzibar, ambayo ni mkusanyiko wa visiwa vingi, vikubwa vikiwa ni Pemba na Unguja. Kisiwa hiki kipo karibu zaidi na kisiwa cha Pemba kwa upande wa kusini.

Ikiwa si kwa helikopta, kwa sababu hakuna uwanja wa ndege, njia iliyozoeleka kufika Panza ni kutumia madau au boti ndogo ndogo. Binafsi nimewahi kufika Panza si chini ya mara tatu.

Ni dakika zisizo fika hata kumi kutoka eneo la Chokocho, lililo kwenye kisiwa kikuu cha Pemba, hadi Panza, kwa dau la mashine au boti.

Shughuli nyingi za watu wa Kisiwa Panza zinategemea kisiwa kikuu cha Pemba. Kila siku, watu hutoka na kwenda Pemba kuuza, kununua, kufanya shughuli za kiofisi, ama hata matembezi na nyenginezo. Kwa hakika, chenyewe Kisiwa Panza ni sehemu ya Pemba, kwa kila maana kutokana na muingiliano wa pande hizo mbili.

Fikiria sasa unakaribia ufukweni upande huu wa kisiwa kikuu cha Pemba, huku jua likizama na kiza ndio hicho kinaifunika miale ya jua taratibu, nawe unasubiri dau la kukupeleka Panza, mara baada ya shughuli zako za kutwa nzima.

Ngozi ikinyamata kwa jasho, viungo vimeachana kwa machofu, huku utumbo ukiwasha kwa njaa, unafika pale unakutana na bwana ambaye ni mvuushaji, anakwambia: “Aaaa weye ndiye ujifanyaye kun’kunywa maji ya bendera. Basi dau langu utaliona tu ivi ivi. Hulipandi.”

Wala usidhani ni utani. Anageuza dau lake na kuelekea Kisiwa Panza ima akiwa na wafuasi wa chama chake tu au bila ya mtu lakini wewe wa chama chengine kakuacha pale na kiza kinaingia.

Sio ajabu kuwa mumezoea kuonana msikitini na kwenye shughuli za kijamii, ukiwa hukumbuki ugomvi wowote kati yako na yeye, ila mawimbi ya siasa ndiyo yamemfanya akuache ufukweni akijuwa wazi nyumbani una mke na watoto, wakikusubiri  kukuona baba yao. Tuache hapo kwanza!

Zanzibar ni jamii kubwa inayounganishwa zaidi na  imani moja kubwa ya Uislamu, lugha ya Kiswahili tuliyozaliwa nayo, na utamaduni wenyeladha nyingi – kama si zote – zinazofanana.

Hata nilipokuwa nikimtembelea Professa Abdalla Bujra, ambaye ni mzaliwa wa Malindi, Kenya, na Mkurugenzi wa Taasisi ya Urithi na Utamaduni ya Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro katika  ofisi yake pale chuoni, alipata kuniambia kuwa: “Zanzibar ni nchi ambayo utamaduni wake unaweza ukawa wa aina moja, kwa tafsiri kuwa, kutafuta vazi la Kizanzibari au chakula cha Kizanzibari si jambo gumu kama kutafuta chakula au vazi litakaloendana na utamaduni wa Watanzania Bara wote.”

Hata hivyo, licha ya ukweli huo wa Wazanzibari kufafana kwa kila namna, siri iliyo wazi ni kuwa siasa ndio hutugawa na kufika hatua ndugu akamchukia ndugu yake wa damu.

Sijafanya utafiti, ila yawezekana Zanzibar ni sehemu pekee au miongoni mwa nchi chache ambapo jirani anaweza kususia mazishi ya jirani yake mpenzi kwa sababu ya mpasuko wa kisiasa utokeapo kila baada ya uchaguzi mkuu.

Ama rafiki akagoma kuhudhuria harusi ya rafiki yake wa karibu kwa sababu chama chake  sicho chama cha bwana harusi.

Mparaganyiko huu haupo kabisa katika maisha ya kawaida ya Wazanzbari, ila huzuka baada tu ya uchaguzi tu, pale mbinu chafu na nguvu zinapotumika kukwapua haki ya wengi.

Mkasa wa Kisiwa Panza ni mojawapo ya mifano mingi. Kuna visa vyengine vingi vya kusikitisha; mfano wa mtu kuandaa chakula kingi kwa ajili ya kuwalisha watu siku ya harusi ya mwanawe kipenzi, watu nao wakashiriki katika harusi ile kwa hatua zote, lakini unapofika wakati wa kula, watu wale hutoweka kama kundi la ndege lililoona hatari inawajia, mwenye harusi akaachwa na masufuria yake makubwa ya wali akishindwa hata vya kuyafanya.

Nakumbuka siku moja ya Machi 2016, nikiwa mkoani Morogoro nilipokea simu kutoka nyumbani Zanzibar, nikielezwa jirani yetu mmoja anafunga ndoa. Ilikuwa habari njema hapana shaka, lakini kizazaa kilichotokea ni kuwa kuna vijana wamefunga njia kwa kuweka magogo ili msafara wa kumpeleka bwana harusi kuchukua mke wake usiende, sababu ikiwa katika msafara ule kulikuw na gari ambayo inamilikuwa na mtu ambaye ni chama tofauti na kundi kubwa la watu wale.

Hata niliporudi nyumbani mwezi Septemba, hali bado ilikuwa si shuwari, na ilikuwa si ajabu kusikia Mzee Fulani kazomewa na kundi la vijana na watoto wakati anapita mtaa fulani, sababu ikiwa ni ile ile ya yeye kuwa mfuasi wa chama kingine na hali ya hewa imeshachafuka.

Kwa maneno mengine ni kusema siasa ina nafasi kubwa katika jamii ya Zanzibar katika kuondosha mapenzi, mtangamano na ustaarabu uliokita mizizi katika visiwa hivi.

Kwa sasa, hali inaonekana kutengemaa taratibu, hata wale ambao waliingia hasara kwa maduka yao kukosa wateja, kwa sasa roho za wasusiaji zimeanza kurudi, yumkini wakiakisi msemo kuwa: “Zimwi likujualo halikwili likakwisha!”

Lakini huo wote ambao nimeulezea hadi sasa, ni upande mmoja tu wa shilingi hii. Huenda mpaka hapo msomaji umeshawatia hatiani wagomaji na wasuasiaji, huku sio tu ukiwaonelea huruma waliogomewa na kususiwa bali hata kuwavua hatia ya aina yoyote. Ukweli ni mwengine kabisa. Sababu ya adha hii kiundani ni kwamba si kweli kuwa chuki hizi husababishwa tu na utofauti vya vyama tu peke yake. Niweke kumbukumbu sawa kuwa Zanzibar inao mfumo wa vyama vingi na watu wanaishi vizuri tu tangu awali.

Matatizo haya huzuka punde tu inapoonekana haki kutotendeka katika uchaguzi mkuu wa kila baada ya miaka mitano. Athari mbaya ya hasira za wanaoamini wamedhulumiwa huishia katika mabega ya masikini wenzao wanaoishi mtaa mmoja.

Tukihesabu kutofaa kwa chuki hizi, pia tusisahau kwanza kuwahesabu wale ambao wanasababisha chuki hizi kuzuka, ambao wao hawaamini kwenye kushindwa. Ndio maana siku zote washindwapo, hawakosi mbinu za kubadili mambo. Tukio la kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 2015, ambao wasimamizi wa nje na ndani waliridhia ulikuwa huru na haki, ilikuwa ni sehemu  ya mbinu ya kubadilisha matokeo halali, na hasira zake kwa wananchi zikawa ni kuwagomea wale wote waliowaona wanaunga mkono uhuni huo.

Wakati huu vumbi la ghadhabu dhidi ya uhuni huo likianza kupoa, haitoshi kufurahia tu jamii inarudi taratibu katika mapenzi yake ya kawaida, wala kuweka matangazo redio na kwenye televisheni kusisitiza umoja wa Wazanzibari. Bali jambo jema zaidi ni kwa hawa wasioamini kushindwa  kuanzisha huo mtangamano kwa kujali haki ya aliyeshinda, ili matukio ya kusikitisha kama ya Kisiwa Panza yasijirudie tena.

TANBIHI: Makala hii kwa mara ya kwanza ilichapishwa katika gazeti la Raia Tanzania la tarehe 10 Machi 2017

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.