Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapoteza kati ya Shilingi bilioni 829.4 na shilingi trilioni 1.439 kutokana na kusafirisha mchanga wenye madini nje ya nchi, kwa mujibu wa mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kuchunguza Mchanga wa Madini hayo, Profesa Abdulkarim Hamis Mruma, alipokuwa akiwasilisha ripoti yake kwa Rais John Magufuli hivi leo Ikulu.

Kwa mujibu wa Profesa Mruma, kamati yake imebaini kiwango kikubwa cha dhahabu kwenye mchanga huo uitwao kitaalamu makinikia, ambapo ndani za makontena 277 yaliyozuiliwa awali bandarini na Rais Magufuli kulikuwa na tani saba za dhahabu yenye thamani zaidi ya shilingi trilioni 1.47.

Sio tu madini za dhahabu, bali kamati hiyo imegundua pia kuwepo kwa shaba, fedha na chuma, ambapo shaba pekee ilikuwa ya thamani ya shilingi bilioni 23.3, tafauti na ripoti ya awali ya serikali iliyosema kuwa ni bilioni 13.

Kutokana na hayo, kamati hiyo imeshauri serikali isitishe mara moja usafirishaji wa mchanga nje ya nchi, sambamba na hatua nyengine kama vile kuhakikisha mitambo ya kusafishia makinikia inafungwa na kufanya kazi nchini.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.