TAIMUR Saleh Juma ameaga dunia leo Jumatatu ya tarehe 22 Mei 2017. Inna lillahi wa Inna Ilayhi Raajiun. Tunamuomba Mola wetu amsamehe makosa yake yote na amfanyie wepesi katika safari ya khera – Aamin. 

Nakumbuka mwazoni mwa miaka ya 80 alishika vyeo vikubwa katika Serikali ya Zanzibar (SMZ). Aliwahi kuwa Meneja Mkuu wa Bank ya Watu wa Zanzibar (PBZ) na baadaye akawa Waziri wa Fedha wa Zanzibar.

Hii, ilikuwa awamu ya pili katika utawala wa Aboud Jumbe. Ni kipindi hichi ambacho Jumbe, aliwaweka kando baadhi ya mawaziri wa tangu 1964, akina Said Washoto. Alijaribu kuwapa vyeo vya juu watu wenye elimu na taaluma. 

Taimur, aliwahi kuwa mwakilishi wa Jimbo la Makadara, Unguja (CCM) katika awamu ya 5 ya utawala wa Dk Salmin Amour. Aliamua kuacha siasa kutokana na chuki za wazi wazi za Dk Salmin, dhidi ya wa-Pemba.

Taimur, baraza yake kubwa ya mazungumzo baada ya sala ya Al-ASR ilikuwa kwa Salim Juma Jabir – Darajani/Malindi, karibu na bekari ya Kokoni. Ilikuwa ni baraza mashuhuri sana lakini, ya watu maalumu.

Nawakumbuka baadhi, akina Maalim Shioni Mzee, Maalim Abdalla Mzee, Sk Salim Mzee na wengineo wenye rika hilo. 

Baraza ya Salim Jabir, ilikuwa ni tofauti na maskani za sasa za siasa. Ilikuwa ni baraza ya watu na heshima na adabu zao. Takriban wengi wameshatangulia mbele ya haki.

Nilikutana na Taimur Saleh, ama Desemba 1999 ama Januari mwaka 2000 ‘Victoria Station – London’ upande wa coach. Ilikuwa ni jioni sana komba msituni washanza kulia.

Mke wangu akanambia: “Mzee Taimur huyo hapo nyuma yetu.” Kugeuza uso ndiye kweli. Baada ya kusalimiana nilimuuliza mbona uko hapa, unaelekea wapi?.

“Nimefika leo kutoka Zanzibar…nakwenda Liverpool katika ‘graduation’ ya mwanangu kesho-kutwa, BUS letu litaondoka saa mbili (8pm)”. Aljibu na akaendelea:
“Nyie mnakwenda wapi?…alituuliza”: Nilimjibu kuwa tunakwenda Canterbury, karibu na Dover, tunakwenda kumtembelea rafiki yetu. Sisi tunakaa hapa London.
Hapo hapo, nilimuuliza…safari hii umegombea?. “Nimeshaacha siasa zamani sana, siasa za Unguja, ni ngumu sana,” alijibu akaishia hapo. Tukaagana. Allah amsamehe makosa yake.

Tanbihi: Ta’azia hii imeandikwa na Rushyd Ahmed kwenye ukurasa wake wa Facebook tarehe 22 Mei 2017

One thought on “Kwaheri Taimur Saleh Juma”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.