KATIKA siasa za Tanzania kuna kupakaziana kwa kila aina, walio madarakani huwakazia wa upande ule wanaoitwa wapinzani. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiliitwa chama cha Wachaga kwa sababu mwaasisi wake ni Eddwin Mtei.

Hawakusema lolote kwa aliyekuwa Makamu wake, Bob Makani (marehemu) ambaye ni Msukuma wa Shinyanga. Baadaye siku zilivyokuwa zinasogea na Chadema kushika moto Kanda ya Kaskazini, wa upande wa pili wakasema chama cha ukanda kupitia Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, Mwenyekiti Freeman Mbowe.

Ujio wa waliokuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, ukatafsiriwa, wakipewa nchi ni hatari na kwamba wataigawa nchi kikanda. Nadhani ni kutokana na mtazamo huo, Freeman Mbowe akamteua Dk. Mashinji Msukuma kutoka Kanda ya Ziwa, ili kuifuta ile dhana ya Chadema kuwa chama cha Ukanda wa Kaskazini.

Kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF), wa upande ule wakadai kuwa ni chama chenye udini; chama cha Waislamu, huku wakijua fika kwamba Sheria ya Vyama vya Siasa inakataza na katika katiba ya chama hicho, hakuna mahali unatajwa uislamu.

Kule Unguja wa upande ule wakasema CUF ni chama cha Wapemba. Ninavyojua mimi hakuna kabila hapa Tanzania linaloitwa Wapemba. Mbona hakuna Wambeya!

Kama hiyo haitoshi, wakaongeza sifa mbaya nyingine kwamba CUF kikipewa kushika madaraka Zanzibar, kitarudisha usultani eti CUF kina nasaba na uwarabu na ikasanifiwa kwamba Waarabu walioikimbia Zanzibar, ndio wanaotoa fedha za kuendesha chama hicho.

Mwaka 2015 kuelekea Uchaguzi Mkuu, vyama vya upinzani vilijiunga pamoja na kuazimia kumsimamisha mgombea mmoja kama mkakati wa kukiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi (CCM), ikazaliwa Ukawa (Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi), umoja ambao uliundwa kutokana na kupinga jinsi Bunge la Katiba lilivyokuwa likiendeshwa na Spika Samuel Sitta (marehemu), alikuwa anapendelea wajumbe wa chama tawala. Vyama vya upinzani vikaamua kususa Bunge na imeelezwa jina la Ukawa aliliibua Profesa Ibrahim Lipumba ambaye pia alikuwa mjumbe kwa tiketi ya CUF na alikuwa na kofia ya Mwenyekiti wa chama hicho.

Viongozi wakuu wa Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD), wakaita mkutano mkubwa uliofanyika pale Jangwani, Dar es Salaam na wakatiliana saini ya kuungana kuipinga CCM. Prof Lipumba ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa wenyeviti na alishiriki kikamilifu katika mazungumzo ya kumkaribisha Lowassa Ukawa.

Ujio wa Lowassa na kuteuliwa kwake kuwa mgombea wa nafasi ya urais, kulizima ndoto ya Prof Lipumba ambaye tayari chama chake cha CUF kilikuwa kimemteua kugombea urais. Yako mengi yaliyosemwa kwamba Lipumba na Dk. Slaa walirubuniwa na kuahidiwa kula vinono kama watajiuzulu uongozi. Mkakati huu ulifanikiwa, lakini haukudhoofisha dhamira ya Ukawa. Lipumba na Slaa waliondoka nchini; mmoja akadai anaenda kufanya utafiti Rwanda, mwingine akaenda Marekani na baadaye Canada.

Prof Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu nafasi yake ya Mwenyekiti na aliondokea hotelini alipofanyia mkutano na wanahabari kwenda kupanda ndege Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Ukawa wakapata pigo jingine kubwa kwa kuondokewa na Mwenyekiti wa NLD, Dk. Emmanuel Makaidi, lakini waliendelea kupigana na kukamilisha ‘vita’ vya Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka 2015.

Miezi minane baadaye, Lipumba akarejea nchini. Akawashangaza wenzake aliposema hataunga mkono Ukawa, umoja alioshiriki kuunda. Kama hiyo haikutosha, akaenda Ikulu kumwona Rais John Magufuli na kumpongeza kwa ushindi, ingawaje CUF kama chama walikuwa wanapinga kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi Zanzibar. Walioelewa hili walielewa.

Miezi michache baadaye, Lipumba akaandika barua kwa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, akieleza kwamba anafuta barua yake ya kujiuzulu na anataka kurejea kwenye nafasi yake ya uwenyekiti. Barua yake ya awali ilikuwa haijajibiwa kwa sababu chama kilikuwa kwenye harakati za uchaguzi, yeye akachukulia kwamba kwa vile hakujibiwa, basi ana haki ya kuendelea kuwa Mwenyekiti!

Walioelewa wameelewa baada ya Lipumba kuvamia mkutano mkuu na kujisimika uwenyekiti. Hapo ndipo mimi nasema sitaki ulipumba, unadumaza demokrasia na watu wote wenye uelewa hawapendi ulipumba, unavuruga chama ambacho umetoka nacho mbali, unashirikiana na polisi ambao kabla ya Uchaguzi Mkuu walikupiga virungu, wakakusweka ndani na kukufungulia kesi katika Mahakama ya Kisutu. Leo ndio maswahiba wako, wanakupa jeuri ya kuvamia ofisi za chama, kuwapiga na kuwajeruhi wale ambao hawakubaliani na ulipumba wako!

Hili liwe fundisho kwa viongozi wa vyama vingine kwamba visifanye ajizi ya kumwaminisha mtu mmoja kwamba bila yeye mambo hayaendi. Anzeni kupeana kijiti cha uongozi kama wanavyofanya wale wa chama cha dola. Chama ni cha wanachama, hata kama wewe ndiye uliyekianzisha na viongozi wasimilikishe uongozi. Kuna vyama vina viongozi wale wale toka vianzishwe na vimekwishapoteza uhalali wa kuitwa vyama vya siasa, lakini vinalelewa tu kwa sababu iko sababu ya kuviacha vidumae na kudumaza demokrasia.

Na hivi ndivyo ilivyo kwamba  chama tawala kinafurahia wapinzani wakivurugana. Kuna chama hakina hata mwakilishi ngazi ya kijiji/kitongoji. Chama kiko mfukoni hakina hata ofisi na kimeshindwa kupata hata diwani mmoja, lakini vinatoa matamko ya kuvipinga vyama vyenye uwakilishi bungeni!

Tanbihi: Makala hii ya Balinagwe Mwambungu imechukuliwa kutoka mtandao wa gazeti la Mtanzania kupitia kiungo: http://mtanzania.co.tz/ulipumba-unadumaza-demokrasia/

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.