Ni jambo la kawaida viongozi wetu kula viapo vya kuulinda Mungano wa Zanzibar na Tanganyika na huyu Rais John Pombe Magufuli viapo vyake huwa vikali zaidi kwa sababu ya khulka yake ya kujifanya si mtu wa maneno laini.

Wiki kadhaa nyuma katika maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa nchi hizi mbili yaliyofanyika Dodoma, Rais Magufuli alisema: “Nataka niwahakikishie kuwa tutaulinda Muungano kwa nguvu  zote, na kamwe asijitokeze mtu yeyote atakaye jitahidi au kujarbu kuuvunja muungano, atavunjika yeye.”

Kauli hizi usidhani ni za masikhara. Kisa cha viongozi wa Uamsho kuendelea kusota ndani ni kutumia haki yao ya kisheria kuuhoji  uhalali wa Muungano, kupinga na kuukataa unyonyaji ulio katika Muungano huo, wakiamini hauna maana bora tu uvunjike.

Kilichofuata ni kubambikiziwa kesi ya ugaidi isiyo na kichwa wala miguu, ikikosa ushahidi kwa miaka minne sasa, imekuwa ni hadithi ya kupigwa dana dana kila siku.

Na Rashid Abdallah

Kwa hiyo, hata ukihoji Muungano kwa kutumia haki yako ya kikatiba, matokeo yake utavunjika, utateketea, uvurugike na kuumia. Ukiacha yanayowakumba Uamsho, mifano hai mingine ipo mingi tu.

Jambo moja linaloumiza na kushanganza mno na ambalo ndio msingi wa makala hii ni kwa nini viapo visiwe kutatua hizi shida, matatizo, na unyonyaji ambavyo vipo katika Muungano?

Ningemuona Magufuli ana nia njema na Muungano kama angekula kiapo akisema: “Nataka niwahakikishie  tutaondoa unyonyaji na kero zilizo katika Muungano huu kwa nguvu zetu zote, na kamwe asijitokeze mtu kuvunja juhudi zetu kwa sababu atavunjika yeye.”

Kipi cha msingi kati ya kula viapo na kulinda Muungano wenye chungu ya malalamiko na kero au kutumia gharama zote kufuta hizi kero na matatizo ya Muungano huo?

Kuulinda Muungano, ambao unajuwa wazi una unyonyaji ndani yake, ni sawa na kumshinikiza mwanamke aishi na wewe kama mke na mume wakati ndoa yenu imejaa matatizo na hasara na mmeshindwa kuyaondosha kwa nusu karne ya ndoa yenu.

Ukimuuliza mwanandoa yeyote, lipi bora kati ya kulinda kwa nguvu zote ndoa yenye matatizo au kutumia nguvu zote kuondoa matatizo, ni wazi kila mwenye akili atatumia nguvu kufuta matatizo yaliyo kwenye ndoa, kwa sababu ndoa isiyo na unyonyaji na manyanyaso haihitaji viapo, kutishana wala nguvu za ziada kuilinda.

Hapa maana yake ni kuwa Muungano wa usawa kwa pande zote, wala hauna haja ya vitisho au vifaru na mitutu kuulinda. Wananchi  wa pande zote wataulinda, kuuenzi na kuupenda kwa sababu hauwanyonyi, wala rais hatokuwa na kazi ya kula viapo na kutisha majukwaani kuulinda.

Muungano unaolindwa kwa maneno makali na vifaru na majeshi, ni kiashiria kuwa wananchi hawatendewi haki katika kuamua lipi wanalitaka na lipi hawalitaki, hulazimishwa kulitii hata lile wasilolifurahia.

Husikii viongozi wakila viapo kutumia nguvu  kufuta unyonyaji ulio katika Muungano, bali wote kipau mbele chao kuulinda Muungano wenye unyonyaji.

Ndio maana kero za kufyonzana katika Muungano zimebaki kwa nusu karne sasa, ambapo Mambo ya Muungano yalikuwa kidogo sana lakini yakaongezwa kinyemela hadi yakawa mengi, na ndipo unyonyaji ukazidi kukuwa.

Kwa nusu karne hii, kama kila viongozi wangekuwa wanatumia nguvu zao kuhakikisha Muungano haunyonyi upande wowote,naamini leo tungekuwa na Muungano unaopendwa na kila upande, au ambao ungechukiwa na wachache sana kama wangekuwepo.

Awadh Ali Said, mwanasheria kutoka Zanzibar anapozungumzia matatizo ya Muungano katika muktadha wa mapato anasema suala la mapato “linaingia  katika suala la uchumi, lakini uchumi si suala la Muungano.”

Kichekesho ni kuwa kila mmoja kati ya Tanganyika na Zanzibar ina uchumi wake na mzigo wa kushughulikia, ikiwemo miundombinu, umeme, elimu, maji safi, “lakini nyenzo kuu za uchumi ambazo ni sera za fedha, sera za kodi, benki kuu, yote hayo yako upande mmoja (Tanzania Bara)”, anasema mwanasheria huyo.

Hii ni sawa na kuiambia Zanzibar kuwa: “Uchumi ni wako lakni huna udhibiti wa sarafu yako, huna udhibiti wa sera za kodi na huna uwezo hata wa kukopa lakin mwenzako muliyeungana amedhibiti yote hayo”, kwa mujibu wa mjumbe huyo wa zamani wa Tume ya Katiba, maarufu kama Tume ya Warioba.

Unyonyaji wa Muungano hata wakereketwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM)  hulalamika wanapoona maji yamezidi unga. Mwezi Mei mwaka jana, Mbunge wa CCM wa Jimbo la Kijito Upele, Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, alilalamika Bungeni akisema:

“Tumezungumza kwa muda mrefu suala la kugawana mapato kati ya serekali ya mapinduzi Zanzibar na ya Muungano…naomba suala hili lifike mwisho limalizwe.”

Unagundua kuwa kumbe ni Muungano ambao kwa muda mwingi umekuwa ukinyonya upande mmoja. Mbunge wa Singida Mjini, Tundu Lissu, amekuwa mara kwa mara akiulalamikia muungano huu wa kinyonyaji hadi kufikia kusema kuwa “Zanzibar imegeuzwa kuwa koloni la Tanganyika.”

Suala la kila nchi kuwa na nyenzo zake kamili za mapato ambalo Awadh alilizungumzia, lilikuwa limewekwa sawa katika Rasimu ya Katiba Mpya iliyopendekezwa.

Bahati mbaya katika Bunge Maalum la Katiba kujadili rasimu ile, wabunge wengi wakiwa wa CCM na wengine kutoka makundi tofauti ya kijamii, wakageuza mambo na hali ikarudi kama mwanzo (unyonyaji).

Kila kitu ambacho kilionekana kinaleta ukakasi katika Muungano kiliwekwa sawa kwa mujibu wa maoni ya wananchi, lakini bahati mbaya hata ule mfumo wa serikali tatu uliopendekezwa nao wakaukata roho.

Kwa nusu karne yote hii, ni wazi kuwa watawala wanalazimisha tu Muungano hu uendelee kubaki.

Tangu awali ilishaonekana wazi kuwa Rais Magufuli hakuwa na nia njema na maridhiano kwenye Muungano, hasa pale aliyekuwa waziri wake wa katiba nba sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alipoutambulisha umma kuwa mchakato wa upatikanaji wa  Katiba Mpya hakikuwa kipaumbele kwa Rais Magufuli.

Wakati akiondoa uwezekano wa kusaka maridhiano kwenye muundo wa Muungano, Rais Magufuli anazidisha vitisho, akipuuzia ukweli kuwa  Muungano wenye ridhaa utalindwa na wananchi wenyewe. Hakuna anayeweza kuizuwia hasa nguvu ya wananchi hao, endapo wataamua kiudhati na kiukweli kuwa wanataka kuuvunja.

Ili kuufanya Muungano huu kuwa na afya na ubaki imara kwa pande zote, la muhimu ni kuutoharisha ili usiwe na harufu ya dhulma za upande mmoja dhidi ya mwengine.

Ili Magufuli aonekane na nia njema na Muungano, basi kwanza airudishe rasimu ya katiba mpya, tena ile ambayo wananchi waliipendekeza. Kwa hatua hiyo, panaweza kupatikana katiba itayofuta kero zote, kwa sababu kutisha watu na kuwasweka ndani wanaousema Muungano huu, hakuuimarishi Muungano wenyewe.

Makala hii kwa mara ya kwanza ilichapishwa katika gazeti la MwanaHalisi la Jumatatu, Mei 8 -14, 2017. Hapa imehaririwa upya.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.