Serikali ya China imezipangua operesheni za upelelezi za Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ndani ya China kuanzia mwishoni mwa mwaka 2010 na kuwauwa au kuwafunga jela zaidi ya mashushushu 20 wa Marekani ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita, linaripoti gazeti la The New York Times.

Gazeti hilo limewanukulu maafisa 10 wa sasa na wa zamani wa Marekani waliolezea kutambulika na kupanguliwa huko kwa operesheni za CIA kuwa ni tukio baya sana kuwahi kutokea kwa kipindi kirefu. Maafisa hao walizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina.

Ripoti hiyo inasema vyombo vya usalama na vya sheria nchini Marekani vilipambana kupunguza hasara ya hatua hizo za China, lakini vilijikuta vimegawanyika vibaya juu ya sababu za kujuilikana kwa kazi zao.

Baadhi ya wachunguzi walikuwa wamejitosheleza kuwa ndani ya CIA mulikuwa na mtu anayetumiwa na China, huku wengine wakiamini kuwa China ilifanikiwa kudukuwa mawasiliano ya siri ya CIA wakati wakizungumza na mashushu wao wa kigeni.

Hadi sasa, suala hilo halijapatiwa ufumbuzi, linasema gazeti la The Times.

Idadi ya mali za CIA zilizopotea nchini China zinawiana na zile ambazo shirika hilo la kijasusi limezipoteza nchini Urusi kutokana na usaliti wa afisa wa CIA, Aldrich Ames, na yule wa FBI, Robert Hanssen, ambao walikamatwa mwaka 1994 na 2001.

Mwaka 2013, mashirika ya FBI na CIA yalifikia suluhisho kwamba China haikuwa tena na uwezo wa kuwatambua mashushushu wa Kimarekani, linasema gazeti hilo, jambo ambalo linapingana na hiki ambacho sasa kimetokezea.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.