Unaweza kuwa unamjuwa Bill Gates kuwa ndiye tajiri kubwa pekee kwa sasa, akimiliki mali zenye thamani ya dola bilioni 100, ama hata John D. Rockefeller aliyewahi kumiliki utajiri wa dola bilioni 250, na wote wawili wakiwa ni Wamarekani. Lakini usichokijuwa ni kuwa tajiri mkubwa kabisa kuliko wote hao ni Mwafrika aliyeitwa Mansa Musa.

Mfalme Musa Keita wa Kwanza anaaminika kuwa mtu tajiri kabisa duniani tangu enzi za uhai wake hadi leo, huku jarida la Time likimtaja kuwa “alikuwa tajiri kuliko mtu yeyote unayeweza kumuelezea”. Utajiri ulikuwa haukadiriki.

Musa Keita wa Kwanza aliingia madarakani mwaka 1312, ambapo alitunukiwa jina la Mansa likimaanisha Mfalme. Inasemwa kuwa Mansa Musa aliiteka miji 24, kila mmoja ukiwa umezungukwa na wilaya na vijiji wakati wa utawala wake.

Mansa Musa alikuwa anamiliki ardhi kubwa sana, kwani alizitawala sehemu zote ambazo hivi leo ni Mauritania, Senegal, Gambia, Guinea, Burkina Faso, Mali, Niger, Nigeria na Chad.

Dunia ilikuja kuujuwa utajiri wake wakati alipokwenda kuhiji Makka mnamo mwaka 1324, akitembea masafa ya takribani maili 4,000. Msafara wake unaripotiwa kuwa ulihusisha watu 60,000 wakiwemo watumwa 12,000 ambao kila mmoja alibeba paundi nne za vinoo vya dhahabu na nguo za hariri zilizotaraziwa kwa michovyo ya dhahabu, farasi waliopewa mafunzo maalum na mabegi makubwa ya ngozi.

Musa aligharamikia kila kitu kwenye safari hiyo yeye mwenyewe, ikiwemo kuwalisha binaadamu na wanyama wote. Miongoni mwa wanyama hao walikuwa ni ngamia 80 ambao kila mmoja alibeba baina ya paundi 50 na 300 za mchanga wa dhahabu. Njiani alimopita, Musa alikuwa akizawadia masikini anaowakuta vinoo vya dhahabu.

Sio tu kwamba aliikirimu miji aliyoipitia akielekea Makka, ikiwemo ya Cairo (Misri) na Madina (Saudi Arabia), bali pia alifanya biashara ya kubadilisha dhahabu kwa vitu vya kale. Inaripotiwa kuwa alikuwa akijenga msikiti mmoja kila Ijumaa.

Hata hivyo, ukarimu huu wa kupindukia wa Musa ulikuja ukauporomoa uchumik wa maeneo aliyokuwa akipita. Katika miji ya Cairo, Madina na Makka kwenyewe, mmiminiko wa ghafla wa dhahabu ulishusha thamani ya chuma kwa muongo mzima baada ya yeye kuondoka. Bei ya dhahabu na vitu vya thamani nayo pia ikashuka vibaya sana.

Ili kurejesha thamani ya dhahabu kwenye soko, alipokuwa akirejea kutoka Makka, Musa aliikopa dhahabu yote kadiri alivyoweza na kuipata kutoka kwa maduka ya fedha mjini Cairo kwa gharama ya juu. Huu ndio wakati pekee kwenye historia ya mwanaadamu, ambapo mtu mmoja pekee aliweza kudhibiti bei ya dhahabu kwenye eneo la Bahari ya Kati.

Baada ya kutawala kwa miaka 25, Mansa Musa alifariki dunia mwaka 1337, akiacha utawala kwa mwanawe wa kiume, Maghan wa Kwanza. Alama ya utajiri wake iliendelea kuonekana kwa vizazi kadhaa na hadi hivi leo kuna maktaba, majengo ya mikutano, na misikiti iliyobakia kama ushuhuda wa zama hizo za neema kwenye historia ya Mali.

Inakisiwa kuwa utajiri wake ulikuwa sawa na dola bilioni 400 kwa thamani ya sasa.

TANBIHI: Makala hii imetafsiriwa kutoka mtandao wa HowAfrica.Com  

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.